Help Children
Love them
Saidia Watoto

Saturday, March 17, 2012

THT, watekelezaji wakuu wa Mradi wa Zinduka waendeleza elimu ya Malaria Kanda ya Ziwa kwa sasa wanamalizia mkoani Shinyanga


Na Mwandishi Wetu
KWA muda mrefu sekta ya sanaa nchini imekuwa ikichukuliwa kuwa ni sekta isiyokuwa na tija kubwa kwa maendeleo ya nchi.
Sekta hii imekuwa ikionekana kuwa ni kama vile sekta ambayo ina umuhimu wa kuburudisha tu kwa njia ya nyimbo katika majukwaa na tena sio kufikia kwa kiwango cha kushiriki kikamilifu katika miradi ya elimu kwa njia ya sanaa.

Kwa sasa dhana hiyo imeanza kufutika kufuatia wasanii wanaoshiriki katika muziki wa kizazi kipya wameanza kushiriki katika miradi mbalimbali ya elimu kwa jamii.

Miradi hiyo ni kama vile ya utoaji elimu kwa njia ya Malaria unaotekelezwa na wasanii wa Tanzania House of Talent (THT) ambao ni watekelezaji wakuu wa mradi wa Zinduka.

THT imeweza kuifikia jamii nyingi za kitanzania na kuzielimisha kwa kuzingatia  mahitaji na mazingira waliyomo katika jamii inayowazunguka.

Kwa kutumia sanaa ya maigizo THT imeweza kuwaelimisha kirahisi wanafunzi pamoja na walimu pia na hata wanajamii na hivyo kuweza kudhihirisha kuwa muziki ni kiungo muhimu katika elimu.

Hayo yanajidhihirisha katika ziara yao ambayo inaendelea katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ambapo wasanii hao kwa pamoja wameweza kushirikiana na Mgodi wa Afrika Barick kuwalinda wananchi dhidi ya ugonjwa wa Malaria.
Nguvu iliyopo katika sanaa ni kubwa mno kwa kuwa licha ya kuwaelimisha wananchi lakini pia wananchi wanapata burudani ambayo inawapa moyo wa kuendelea kusikiliza ujumbe lakini pia hata kukumbuka kirahisi yale waliyofundishwa.

Katibu Mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Ghonche Materego aliwahi kusisitiza umuhimu wa ngoma za asili, maigizo na hata nyimbo za kizazi kipya katika kuifikia jamii na kuielimisha.

Anafafanua kuwa muziki unaweza kuwa na ujumbe zaidi ya mmoja kwa kuwa wanamuziki wanaweza kufikisha ujumbe kwa kutumia miili yao na hata kwa kutumia sauti na njia nyingine muhimu.

Wasanii wa THT wameweza kuifikia mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera na Shinyanga ambapo wasanii hao wa THT wametembelea sekondari katika mikoa hiyo na kuimarisha klabu za Malaria kwa wanafunzi.
Martini Genos ni mratibu wa elimu ya Malari aya THT shuleni anasema kuwa kwa sasa wamemaliza ziara yao katika Mkoa wa Kagera na wameshaingia Shinyanga ambapo walianzia mkoa wa Mara na baadae wakafuata Mwanza.

Anasema kuwa kupitia muziki wameweza kuhamasisha wanafunzi pamoja na watu wengine katika jamii na kuwafundisha masuala mbalimbali kupitia ngoma, nyimbo za asili na za kisasa pamoja na maigizo.

Anasema kuwa nguvu iliyopo katika sanaa za maigizo na nyimbo ni kubwa kwa kuwa imewaweka karibu na wanajamii na wanafunzi wa mikoa hiyo kiukaribu zaidi na kuwapatia elimu.

Anatolea mfano kuwa katika mkoa wa Mara waliwafikia wanafunzi 7500 huku wanajamii wanaohudhuria matamasha yao nao pia wakiwa 2000 ambapo wasanii nane kutoka THT walishiriki kikamilifu katika kutumia vipaji vyao kubadilisha mitazamo potofu ya wannachi kuhusiana na asili ya ugonjwa wa Malaria kuanzia maambukizi yake mpaka namna ya kuutibu.

“ Kwa kawaida tunawauliza wanaliza wanafunzi maswali mbalimbali kwa lengo la kupima uelewa wao katika masuala ya Malaria na kuanzia hapo ndio tinaona ni njia gani ya kuanza kuwaelimisha juu ya ugonjwa huu” anasema Martin.
Anasema kuwa wanatumia siku chache wanapokuwa katika jamii za mikoa hiyo kuwauliza wanafunzi kuhusiana na uelewa wao wa ugonjwa wa Malaria a kubaini kikwazo kikubwa cha ugonjwa huo na kisha kutunga igizo.

Licha ya wasanii hao kuwa na maigizo yao kuhusiana na namna ya kupambana na Malaria lakini pia wanaweza kutunga upya au kuongezea vionjo mbalimbali vinavyowaweka wanafunzi kuwa karibu zaidi na igizo hilo.

Martini anasema kuwa katika maigizo hayo wasanii wa THT wanaweza hata kuingiza maneno ya kilugha katika mikoa wanapokuwa wanatoa elimu ya Malaria ilimradi kuwaweka karibu walengwa ambao ni wanafunzi wa Sekondari katika mikoa hiyo.
Akizungumzia Sekondari ambazo wasanii wa THT wametoa elimu kwa njia ya sanaa mkoani humo anasema kuwa waliwasili katika Sekondari ya Lubondo iliyopo wilayani Biharamulo, Sekondari ya Chato iliyopo Chato, Sekondari ya Bukoba iliyopo Bukoba mjini na  sekondari ya Kishoju iliyopo Muleba.
Akizungumzia namna ambavyo THT inaweza kubadilisha mawazo kama hayo anasema kuwa wasanii hao wanaweza kutunga maigizo ya kukemea hali hiyo huku wakitumia mifano hai katika jamii kama hiyo.
Anasema kuwa ili kupambana na imani kama hizo THT licha ya kutoa elimu ya malaria lakini pia inaandaa klabu za malaria kwa wanafunzi katika kila shule ambayo imetembelea.

Akizungumzia hamasa ya wanafunzi katika kuvutiwa na sanaa za THT katika kupata elimu anasema kuwa THT mkoani Kagera wanafunzi wamekuwa hawana tofauti sana na mikoa mingine waliyokwisha kwenda kwa kuwa kwanza walionekana kuvutiwa sana na sanaa iliyotumika pia.

Pia alisema kuwa uelewa kwa wanafunzi kuhusiana na malaria ni mkubwa isipokuwa kuna masuala muhimu ambayo yalikuwa ya kuongezea katiak suala la elimu kwa wanafunzi.

kazi ya uelimishaji ilianzia Mara katika Sekondari ya Dk Nchimbi  iliyopo wilaya ya Bunda na ndipo walipoanza kujipanga na kujua ni nini zaidi wanatakiwa kuwapatia wananchi.Kundi hilo la THT pia lilielimisha na kuburudisha Sekondari za Buhita ya Musoma vijijini, Nkende ya Tarime Malenge ya Musoma vijijini na Nyandega iliyopo wilaya ya Rolya.

0 comments:

Post a Comment