Help Children
Love them
Saidia Watoto

Thursday, May 2, 2013

Wanafunzi ombeni mikopo kwa kufuata utaratibu

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza kuanza kupokea maombi ya mikopo kwa wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na vyuo vikuu pamoja na wanafunzi wanaoendelea kwa mwaka wa masomo 2013/2014.

Heslb imetoa mwezi mmoja kwa wanafunzi kuomba mikopo kuanzia keshokutwa hadi Juni 30 mwaka huu.


Wakati  katika mwaka wa masomo wa 2012/13 wanafunzi 94,703 ndiyo walionufaika na mkopo huo wa elimu ya juu, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Bodi hiyo Cosmas Mwaisobwa aliliambia gazeti hili haba kwamba kwa sasa haijajulikana ni wangapi watanufaika.


Idadi ya wanafunzi watakaonufaika sanjari na kiasi cha fedha kwa ajili ya mikopo hiyo, havijajulikana kutokana na kile Mwaisobwa alichosema ni mpaka bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itakaposomwa.

“Bajeti ya elimu bado haijapitishwa, hatujui kiasi kitakachopitishwa. Ikishapita, ndipo tutaweza kueleza ni wanafunzi wangapi watapata mkopo,” alisema Mwaisobwa.


Awali akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwaisobwa alisema mwombaji wa mkopo huo anapaswa kuwa na sifa ambazo zimetajwa katika kifungu cha 17 cha Sheria Na 9 ya mwaka 2004 ambazo ni pamoja na kuwa raia wa Tanzania.


Sifa nyingine ni kudahiliwa katika chuo cha elimu ya juu, kutokuwa na njia nyingine ya kugharimia elimu ya juu, kufaulu mitihani ya mwaka uliotangulia kwa waombaji wanaoendelea na masomo pamoja na kuwa mhitaji.


"Bodi inasisitiza kwamba waombaji wa mikopo wazingatie muda uliopangwa na pia kufuata kwa umakini taratibu zote zilizoainishwa katika uombaji wa mikopo," alisema na kusisitiza kuwa hakutakuwa na muda wa ziada baada ya muda uliopangwa kupita.


Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa Mawasiliano wa bodi, alisema maombi yatafanyika kwa njia ya mtandao kupitia anuani ya bodi http://olas.heslb.go.tz.


Mwaisobwa alisema vipeperushi maalumu vyenye maelezo ya jinsi ya kuomba mkopo kwa njia ya mtandao vinapatikana kwenye vyuo vya elimu ya juu, ofisi za elimu za wilaya,watoa huduma ya intaneti, Makao Makuu ya Bodi ya Mikopo na Ofisi za Bodi ya Mikopo za Kanda.


Waombaji wapya wanatakiwa kulipa ada ya maombi ya mikopo ya shilingi 30,000 huku wanafunzi walio katika mwaka wa masomo wa tano au wa sita wa masomo wataendelea kulipa ada ya maombi ya sh 10,000.


Hata hivyo wanafunzi wa mwaka wa pili, tatu na nne ambao walilipa ada ya maombi ya sh 30,000 katika miaka ya masomo ya 2009/2010, 2010/2011 na 2011/2012 hawatakiwi kulipa tena ada hiyo ya maombi ya mikopo.
mwisho

0 comments:

Post a Comment