Help Children
Love them
Saidia Watoto

Sunday, March 24, 2013

Mwalimu aingia mkutanoni akiwa na nguo za kike


KATIKA hali ya kushangaza, mwalimu wa kiume katika shule ya msingi Chididimo Kata ya Zuzu katika Manispaa ya Dodoma (jina tunalo),  juzi alitinga mkutanoni akiwa amevalia sketi na blauzi ya kitenge huku akiwa amesuka nywele za bandia na kuzua gumzo mkutanoni hapo.

Licha ya mwalimu huyo kuvaa viatu vya kiume na soksi fupi, alikuwa akitembea mwendo wa kiume huku mikanda ya sidiria aliyokuwa ameivaa kujitokeza mara kwa mara.

Haya yalitokea katika kijiji cha Chididimo wakati wa Wiki ya Maji kimkoa, ambapo pamoja na mambo mengine kulikuwa na uzinduzi wa mradi wa maji.

Mwalimu huyo alikuwa kati ya wacheza ngoma wa kikundi cha Mpango Kazi Chididimo, lakini ilikuwa ni vigumu watu wasiomfahamu kumtambua. Hata hivyo watu walianza kupata wasiwasi kuwa hakuwa mwanamke wakati kikundi hicho kilipoingia uwanjani, ambapo alikuwa akiimba kwa sauti nzito.

Lakini, maswali ya wageni waliohudhuria mkutano huo, yalipata majibu mara baada ya mwalimu huyo kupanda jukwaani akiwa na mwenzake kwa ajili ya kuimba shairi.
Kutokana na hilo ndipo wanakijiji walipoanza kutoa siri kuwa alikuwa ni mwanaume na ni mwalimu wa shule ya msingi kijijini hapo.

Kutokana na utata na minong’ono iliyosambaa mkutanoni hapo,  mwongozaji wa sherehe hizo alimfuata mwalimu huyo na kuzungumza naye kwa muda na aliporudi alikuwa tayari na jina la mwalimu huyo na kusema kuwa mwenye nywele ndefu ameshalifahamu jina lake kisha kulitaja.

Mshereheshaji huyo alisema hata  nyimbo na shairi ambalo wanafunzi waliimba, alitunga mwalimu huyo ambaye ni mahiri katika sanaa.
Mwalimu huyo alikiri kuwa sanaa ipo kwenye damu yake na alifanya hivyo kama msanii.

Shule ya wasichana ya Henry Gogarty yatembelewa na Lowassa


WAZIRI Mkuu mstaafu, Edward Lowassa amepongeza wazazi wa wanafunzi wa shule ya wasichana ya masista wa Kikatoliki  Henry Gogarty iliyopo wilayani Arumeru kwa jitihada za kujenga majengo ya shule hiyo kwa hiari.

 Alisema mfano huo unapaswa kuigwa na wazazi wa shule nyingine.
 
Lowassa alisema hayo juzi kabla ya harambee ya ujenzi wa maabara na mabweni ya shule hiyo. Alisema kuwa wazazi wengine wanapaswa kuiga mfano huo.
 
 Alisema pongezi  anazotoa ni za dhati, zinazopaswa kuigwa na wazazi wengine kwani katika harambee nyingi alizowahi kufanya, hajawahi kuona wazazi wanaoweza kujitoa kwa kiasi kikubwa kuchangia harambee na maendeleo ya shule.
 
 "Hawa wazazi wanapaswa kupongezwa na mfano huu unapaswa kuigwa katika shule zingine, kwani wengi wamekuwa wakitaka kuchangiwa tu, tofauti na hapa wazazi wanachanga wenyewe hivyo wanapaswa kupewa nguvu kubwa,’’alisema.
 
 Pia, Lowassa alilisifu shirika la masista wa Mkoa wa Kilimanjaro kwa jitihada zake za kuendeleza elimu hapa nchini na nje ya nchi.
 
  Alisema na kuisifu shule hiyo katika kufanya vizuri katika mitihani yake ya Taifa. Aliwataka walimu kuendelea na moyo huo ili shule hiyo iweze kuongoza kitaifa.
 
 Mkuu wa Shule hiyo, Bernada Moshi alisema shule hiyo ilianzishwa mwaka 2011 na inakabiliwa na changamoto kubwa za uhaba wa mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike na maabara.
 
 Moshi alisema lengo ni kukusanya Sh milioni 250 kwa kujenga majengo ya mabweni na maabara. Alisema lengo kuu la shule hiyo ni kutoa elimu bora na maadili kwa mtoto wa kike, ambaye ni nguzo muhimu katika maendeleo ya familia na jamii.  

Katika harambee hiyo, jumla ya Sh196,493,350 zilichangwa, huku fedha taslimu zikiwa Sh 120,863,350 na ahadi Sh 75,630,000.
 
 Lowassa pamoja na rafiki zake walitoa Sh milioni 10 na kompyuta mbili.

Tuesday, March 19, 2013

Wanawake saba wapanda Mlima Kilimanjaro na kutembelea shule mbalimbali hapa nchini

Huyu ni mmoja kati ya wanawake waliopanda Mlima Kilimanjaro yeye ni Mtanzania
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Utalii ya nchini Nepal  Subash Niroula akimkabidhi zawadi Mkurugenzi wa Utalii wa Wizara ya Maliasili na Utalii Ibrahim Mussa wakati wa hafla ya kuwaaga wanawake saba kutoka nchini Nepal waliopanda Mlima Kilimanjaro katioka maadhimisho ya siku ya wanawake duniani
Mkurugenzi wa Utalii wa Wizara ya Maliasili na Utalii Ibrahim Mussa akizungumza katika hafla hiyo
                       
Picha ya pamoja na wanawake waliopanda mlima huo

Musa na mkewe huyo wa katikati

Mimi pia nilipiga picha na wanawake hao

                                                              
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Aloyce Nzuki na Mkurugenzi wa Utalii wa Wizara ya Maliasili na Utalii Ibrahim Mussa wakiwa katika picha ya pamoja katikati ni Mrs Mussa  



KIONGOZI wa kundi la Wanawake Saba kutoka nchini Nepal waliopanda mlima Kilimanjaro, Shailee Basnet, ameitaka serikali pamoja na wanajamii kusaidia kupambana na manyanyaso dhidi ya wanawake nchini.

Alisema kuwa katika kusaidia kampeni dhidi ya manyanyaso ya wanawake duniani wamekuwa na utamaduni wa kupanda milima mirefu duniani na kufikisha ujumbe wa kutetea haki za wanawake ambapo wameshapanda milima Everest na Mlima Kilimanjaro.

Alisema kuwa wakiwa hapa nchini wametembelea shule mbalimbali kutoa elimu ya kujiamini na kujitambua kwa wanafunzi wa shule mbalimbali.
 
Wakati huohuo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Utalii ya nchini Nepal Subash Niroula alisema kuwa tayari wamenza kukutana na wamiliki wa kampuni za Utalii za hapa nchini.

Niroula alisema kuwa Tanzania kuna vivutio vingi vya utalii ambavyo vinatakiwa kutangazwa nchini Nepal na sehemu nyingine duniani.

Alisema kuwa ili kufanikisha utangazwaji wa utalii huo kunahitajika kuwepo kwa juhudi binafsi kutoka kwa wadau wa utalii wa Nepal na Tanzania kushirikiana pamoja ili kufanikisha ukuaji wa utalii huo.

Alisema kuwa Mlima Kilimanjaro unafahamika zaidi nchini Nepal na unaweza kutangazwa kikamilifu zaidi ili kuongeza idadi ya watalii wanafika Tanzania.


Mwisho