Help Children
Love them
Saidia Watoto

Sunday, March 3, 2013

Wadau wa elimu wahoji muda wa wiki sita kufuatilia kufeli kwa kidato cha nne




UTEUZI wa Tume ya Kuchunguza Matokeo ya Kidato cha Nne, umeamsha mjadala kuhusu muda uliotolewa kukamilisha kazi hiyo na aina ya wajumbe wanaopaswa kutekeleza majukumu yake.

Wakizungumza na gazeti hili jana, baadhi ya wasomi walisifu hatua ya Serikali kuteua Tume hiyo ili kuondoa mkanganyiko uliopo, kuhusu chanzo cha matokeo mabaya ya kidato cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni. 

Mhadhiri wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Ayub Rioba, alisema wazo la Serikali ni zuri kwa kuwa litaondoa mkanganyiko huo. 
 
“Kama alivyosema Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake na pia Waziri Mkuu Mizengo Pinda, matokeo ya Tume yatasaidia kuondoa watu wanaoongea ovyo bila uhakika. Kila jambo lina sababu, mambo hayatokei hivi hivi lazima kuna chanzo,” alisema Dk Rioba.

Hata hivyo, alionesha wasiwasi wake kuhusu muda wa wiki sita uliotolewa kwa Tume hiyo ya wajumbe 15, wakiongozwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Profesa Sifuni Mchome na kupendekeza usingekuwa chini ya miezi miwili.

“Ili kupata matokeo ya kina, ni wazi muda waliopewa ni mdogo, maana ukiangalia hadidu za rejea wanahitaji kwenda mbali zaidi, si kuangalia matokeo ya mwaka huu pekee bali zaidi ya hapo, ila pengine kwa sababu utafiti mbalimbali upo, wanaweza kuutumia na muda ukatosha,” alisema Dk Rioba.

Kuhusu wajumbe wa Tume hiyo iliyoteuliwa na Pinda juzi, Dk Rioba alisema hana shaka nao, ni watu wenye weledi na uzoefu mkubwa wa masuala ya elimu. Alitoa mfano Profesa Mchome, kuwa ni msomi na Mwanasheria aliyebobea na mwenye weledi.

Dk Rioba pia alisifu hatua ya Serikali kuchanganya wajumbe wa Tume na kuwaweka wanaotoka asasi za kiraia ikiwemo Twaweza, inayowakilishwa na Mwenyekiti wake, Rakesh Rajab, kwa kuwa ni watu wanaojihusisha na utafiti mbalimbali kuhusu elimu hapa nchini.

“Sina wasiwasi kabisa na wajumbe wa Tume walioteuliwa, wengi ni wazoefu na wanawakilisha jamii, ninavyoelewa maana ya Tume ni mkusanyiko wa watu wenye mchango na uelewa fulani katika eneo linalohitajika.

“Si lazima wawe moja kwa moja wahusika wa eneo hilo,   wanachotakiwa ni kupata maoni ya walimu wakongwe wa sekondari na shule za msingi,” alisema Dk Rioba.

Dk Bana na wajumbe

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Dk Benson Bana, naye aliipongeza Serikali kwa hatua hiyo na wazo zuri la kutafuta suluhu ya tatizo la kushuka kwa elimu nchini.

Hata hivyo, Dk Bana alisema wazi kuwa pamoja na kwamba muda hautoshi, hana imani na baadhi ya wajumbe.

 “Ni hatua nzuri Serikali imechukua ili ituridhishe wananchi, lakini binafsi sijaridhika na uteuzi na weledi wa wajumbe, ilipaswa iwe na walimu waliobobea katika elimu ya sekondari nchini, sioni kama wana uzoefu na uchungu wa elimu ya sekondari, hawatakuja na jipya.   

 “Baadhi ya wajumbe ni wanaharakati, unawekaje mwanaharakati kama Mbatia (James, Mbunge Mteule na Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi) au Rakesh (Mwenyekiti-Taasisi ya Twaweza)?

“Pia hii si tume ya maprofesa na madokta wa vyuo vikuu, kuna tofauti ya mhadhiri na mwalimu, sina hakika kama Mwenyekiti, Profesa Mchome amewahi kufundisha sekondari,” alisema Dk Bana.

Kuhusu muda, Dk Bana alisema wiki sita zilizotolewa kwa Tume hiyo aliyoiita ‘Tume ya Mitihani’,  hautoshi hata kupata jawabu la matokeo mabaya mwaka huu.
Alisema tatizo la elimu halipo katika shule za msingi na sekondari pekee, bali mpaka vyuo vikuu kuna madudu makubwa.

Msomi huyo alipendekeza Tume hiyo ifanye kazi kwa miaka miwili na si vinginevyo kama ilivyokuwa Tume ya Elimu ya Makwetta (marehemu Jackson), aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali, ikiwemo Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu kati ya 1995-1998.

Waliopata sifuri



Mbatia jana alipotafutwa kueleza hatima yake katika Tume hiyo baada ya kuonekana kajitoa katika Tume, alisema leo atakutana na waandishi wa habari kueleza kila kitu.

Tume



“Tumepokea uteuzi, kuna kazi kubwa mbele yetu, tutawashirikisha watu wengi kadiri iwezekanavyo ila ni mapema kusema tutakaozungumza nao, hilo la muda tuachwe tuanze kazi kwanza ndipo tutajua huko mbele, sina wasiwasi na wajumbe, tutafanya kazi pamoja,” alisema Mushashu.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu hakutofautiana na wasomi kuhusu muda kuwa mdogo na kuitaka Tume kufika mpaka vijijini waliko walimu wazoefu zaidi ya miaka 25 hadi 30, ili kupata maoni yao kuhusu elimu ya sasa.

“Isiishie katika matokeo, binafsi naomba wafike vijijini kuliko na matatizo ya miundombinu na kwenye uhaba wa walimu hasa wa Sayansi, ipo shule hapa mwanafunzi anatembea kilometa 24 kwenda na kurudi, huyu unataka afaulu kweli?” Alihoji Muhingo ambaye kitaaluma ni mwalimu na mwandishi wa habari.

Muhingo aliiomba Tume iangalie upya utaratibu wa ufundishaji wa walimu vyuoni, hasa wanaochukua shahada ambao alidai wengi wanalalamikiwa kutokuwa na maadili, wala uchungu na elimu ya watoto wanaowafundisha.

Mbali na Profesa Mchome na Mushashu, Tume hiyo imeshirikisha wajumbe kutoka Zanzibar na Tanzania Bara kutoka taasisi binafsi, serikalini na vyuo vya elimu ambao wote ni wadau katika elimu nchini.
Mwisho.

0 comments:

Post a Comment