Help Children
Love them
Saidia Watoto

Thursday, April 2, 2015

Ebu someni harakati za dada huyu katika kuendeleza fani ya Mitindo kwa kutoa elimu bure







Na Evance Ng'ingo
KILA kukicha sekta ya sanaa kwa hapa nchini inaendelea kukua huku kukiwa na aina mpya mbalimbali za sanaa ambazo zinajitokeza na kuongeza ajira kwa jamii.
Fani ya Uanamitindo ni moja kati ya fani kubwa ambazo zinazidi kuwavutia vijana wengi kujitokeza na kujiajili katika fani hiyo.
Uanamitindo ni fani ambayo inaendelea kukua kila kukicha huku kukiwa na makampuni mbalimbali hapa nchini nayo yakitangaza bidhaa zao kupitia fani wanamitindo hao.
Aj Mynah ni moja kati ya wanamitindo mahiri hapa nchini ambao wameanzisha harakati za kuwaendeleza wanamitindo wengine hasa vijana kutoka sehemu mbalimbali hapa nchini.
Aj mwenyewe akiwa ni mwanamitindo ambae amefanya shughuli zake hizo nje ya Tanzania kwa muda kwa sasa aanasema kuwa Tanzania ni nchi ambayo inakua kwenye tasnia ya uanamitindo na kuna haja ya kuwekeza zaidi kwa vijana katika kuwaandaa kuifikisha mbali tasnia hiyo.
Alisema kuwa kwa nchi zilizoendelea hiyo ni fani ambayo inawapatia vijana wengi ajira kubwa huku wengi wao wakipata mikataba minono ya kutangaza bidhaa za makampuni makubwa makubwa.
Alisema kuwa kwa hapa nchini hilo linawezekana kwa kuwa wapo vijana wenye sifa kubwa za kutangaza matangazo kwa kupitia fani hiyo ya uanamitindo.
Anaongeza kuwa kwa kutambua hilo ameamua kuanzisha mpango wa kutoa mafunzo ya bure kwa vijana mbalimbali wenye vigezo vya kuwa wanamitindo katika klabu ya Paparazi iliyopo Sleep Way Masaki. 
Aj ambae ni anatoa mafunzo hayo kupitia kampuni yake ya Black Fox  Model ambapo akizungumzia kuhusiana na sababu zilizopelekea kuanzisha mafunzo hayo alisema kuwa kampuni yake hiyo imeamua kutoa mafunzo hayo bure kwa vijana baada ya kutoridhishwa na maendeleo ya fani hiyo hapa nchini.
"Kinachotakiwa kwa sasa ni mikakati ya kuona ni kwa kiasi gani fanii hii inaweza kuendelezwa zaidi na zaidi na kwa kuanzia mimi kama mdau nimeona nianze kwa kutoa mafunzo bure kwanza kabla ya kuja kuanza kuendelea na mengineo"anasema Aj.
Anaongeza kuwa " baada ya miaka kadhaa anataka kuona kuwa kuna watanzania wanashiriki katika maonesho makubwa makubwa ya mavazi ndani na nje ya Ulaya na kuitangaza nchi".
Anaongeza kuwa anaona kuwa vijana wa kitanzania wakijihusisha na fani hiyo wanaweza kufika mbali pia hata kufikia hatua ya kuiwakilisha Tanzania kimataifa zaidi.
Anafafanua zaidi kuwa  "Unaweza kuwaona wadada au wakaka ambao wanavutia kuwa wanamitindo na ukiwauliza kama wamewahi kufikiria kujihusisha na fani hiyo utakuta labda hata wazo hawana na wengine hawaoni fursa za zitokanazo na fani hiyo"
Pia anasema "Kwa sasa nimeamua kuanzisha kampuni hii kwa lengo la kuhakikisha kuwa vijana wanaandaliwa vema na kuja kuwa wanamitindo wakubwa ambao wanaweza kutangaza bidhaa mbalimbali za ndani na nje ya nchi na kila Jumapili tunakuwapo hapa klabu ya Paparazi, Sleep Way Masaki na ni bure kabisa kwa vijana kuja kujifunza".
Kampuni hiyo ina mpango wa kuzunguka nje ya mkoa wa Dar es salaam kutafuta vipaji zaidi kwa vijana na kisha kuanza mpango wa kuwaendeleza huku akiendelea kusisitiza kuwa vijana wenyewe kwanza wanatakiwa kujitambua na kuipenda kazi hiyo.
Aj ambae ni mwanadada mrembo, mrefu, mwembamba na mwenye kila sifa ya kuwa mwanamitindo, anawataka vijana kujitokeza na kujiunga kwenye harakati zake hizo huku akisisitiza kuwa anapokea vijana wa kila aina.
Anasema kuwa katika kampuni yake haangalii wale wembamba tu kwa kuwa anaamini kuwa kwa hapa nchini wapo wabunifu wa mavazi ambao wanatengeneza nguo za wateja wao wanene na hivyo wangehitaji kuwatumia wanamitindo wenye miiili pia.
Kwa kuwa kazi hiyo ya uanamitindo ina uhusiano wa karibu zaidi na mavazi, mnmoja kati ya wabunifu wakubwa wa mavazi hapa nchini Ally Remtulah anasema kuwa wanamitindo wanahitaji elimu zaidi ya fani hiyo.
Anasema kwa elimu inayotakiwa kutolewa ni pamoja na ile inayohusiana na suala nidhamu, utambuzi wa fursa katika kazi hiyo ikiwa pamoja na kujitangaza kwa wabunifu husika.
"Najua katika kazi hi kikubwa zaidi kinachotakiwa kufanyika ni kujitangaza kwa wanamitindo wenyewe ili kufahamika ndani na nje ya Tanzania huku akisisitiza zaidi matumizi ya mitandao ya kijamii"anasema Ally.
Kwa sasa hapa nchini kuna maonesho ya mavazi takribani saba ambayo hufanyika kila mwaka lakini kwa yale ambayo ni lazima kufanyika huwa ni pamoja na Swahili Fashion, Ally Remtulah Fashion Extragavanza, Lady in Red na mengineo mengi.
Lakini kwa upande wake Mwanamitindo chipukizi Monalisa Singano anasema kuwa mafunzo ya mapema kwa wanamitindo ni muhimu kwa kuwa yanawajengea hali ya kujiamini na kuipenda kazi hiyo.
Anaongeza kuwa wapo vijana ambao kwa upande wao wanakuwa na sifa za kazi hiyo lakini hawajajitambua na iwapo kukiwa na hamasa na elimu itasaidia kwa vijana kujiunga na fani hiyo.
==============