Help Children
Love them
Saidia Watoto

Monday, June 1, 2015

Msome Waziri Kawambwa kuhusiana na elimu nchini


SEKTA  ya Elimu imefanikiwa kwa asilimia 81 na kushika nafasi ya kwanza katika utekelezaji wa awamu ya kwanza ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).

Matokeo ya utekelezaji wa mikakati iliyowekwa na BRN ni kupanda kwa ufaulu wa mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi (Darasa la Saba) na kupanda ufaulu wa mtihani wa kumaliza Elimu ya Sekondari (Kidato cha Nne).

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa aliyasema hayo bungeni jana wakati alipowasilisha Bajeti ya Mwaka 2015/16.

Dk Kawambwa alisema, “Kwa mujibu wa taarifa ya mwaka mmoja (2013/14) sekta ya elimu imefanikiwa kwa asilimia 81 na kushika nafasi ya kwanza katika utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mikakati hiyo.”

Aliyajata baadhi ya mafanikio ambayo yamehakikiwa na ‘Presidential Delivery Bureau’ ni kutoa tuzo kwa shule na wanafunzi waliofanya vizuri kwenye matokeo ya darasa la saba na kidato cha nne.

Alisema jumla ya tuzo 3,044 zilitolewa kwa shule zilizopata ufaulu uliotukuka na zile zilizopanda kwa ufaulu ikilinganishwa na mwaka 2013.

Pia alisema walimu 4,103 wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Lugha walipatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kutambua wanafunzi wenye uwezo mdogo wa kumudu masomo.


Aidha, alisema ujenzi wa miundombinu ya shule 47 za sekondari kati ya 264 zilizolengwa katika awamu ya kwanza ulikamilika. Lengo ni kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya shule 1,200 katika awamu tatu.

“Madeni ya shilingi 1,852,162,158.21 ya malimbikizo ya mishahara yalilipwa kwa watumishi 916 wa wizara,” aliongeza Dk Kawambwa.

Alisema matokeo ya utekelezaji wa mikakati hiyo ni kupanda kwa ufaulu wa darasa la saba kutoka asilimia 50.6 mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 56.99 mwaka 2014.

“Na kupanda kwa ufaulu wa Mtihani wa kumaliza Elimu ya Sekondari (Kidato cha Nne) kutoka asilimia 57.09 mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 69.76 mwaka 2014,” alieleza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Akizungumzia utungaji wa Sera za Elimu, alisema rasimu ya andiko la uanzishwaji wa Bodi ya Kitaalamu ya Walimu imekamilika, na kuwasilishwa katika mamlaka husika.

Aidha, alisema katika mwaka 2014/15, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilitoa mikopo kwa wanafunzi 99,590 wakiwemo 2,117 wa Stashahada ya Elimu ya Ualimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati.

Alisema Bodi hiyo ilikusanya marejesho ya mikopo kiasi cha Sh 15,978,993,320.04 sawa na asilimia 45.5 ya lengo la makusanyo kwa mwaka 2014/15 na hivyo kufikia Sh 75,575,793,215 sawa na asilimia 45.45 ya Sh 165,008,246,475 za madeni yaliyoiva.

Kuhusu changamoto katika mwaka wa fedha uliopita, ilisema mojawapo ilikuwa ni kulipa madeni ya wazabuni na huduma nyingine sasa yanafikia Sh 45,855,370,632.7.

Alisema kati ya hizo, Sh 25,195,672,974.2 ni deni la wazabuni wa vyuo vya ufundi na Sh 5,148,207,930.00 ni deni la posho za wahadhiri.

Akizungumzia vipaumbele kwa mwaka 2015/16, alisema Wizara itasimamia utungaji na utekelezaji wa Sera za Elimu, ithibati ya shule na udhibiti wa ubora wa elimu.

Kwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, alisema itaendelea kuratibu na kusimamia udahili na ukaguzi wa wanafunzi 60,000 ili kufikia lengo la kuwa na wanafunzi 300,000 katika taasisi za elimu ya juu ifikapo mwaka 2016.

Kuhusu Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, alisema itakusanya Sh 51,001,034,808.24 za marejesho ya mikopo iliyotolewa kati ya mwaka 1994/95 na 2014/15.

Dk Kawambwa aliliomba Bunge liidhinishe bajeti ya Sh 989,552,542,000, ambazo kati ya hizo, Sh 478,675,159,000 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo zikiwamo Sh bilioni 446.578 za ndani ambazo Sh bilioni 348.3 zitatumika wa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.