Help Children
Love them
Saidia Watoto

Sunday, July 28, 2013

Wanafunzi wakijitokeza kwenye usaili wa EBSS Dar es salaam

Wasichana hawa ni mapacha ambao walijitokeza kwenye usaili wa shindano la Epiq Bongo Star Search (EBSS) uliofanyika kwenye uwanja wa taifa Dar es salaam, walilazimika kuimba pamoja na ni tukio la kwanza kwa washiriki wawili kuimba pamoja kwenye usaili

Madam Ritha akiwapatia wadada hao namba yakle ya simu ili wamtafute
Hawa wadada ni wa mapacha ambao elimju yao iliishia darasa la saba na kutaka kujifunza kuimba lakini hata hivyo hawakukidhi viwango na Madama Ritha aliamua kuchukua namba zao ili kuangalia uwezeknao wa kuwasaidia
Mwanafunzi wa kidato cha nne katika sejkondari ya Yusuph Makamba, Dar es salaam akifurahi baada ya kupita awamu ya kwanza ya shindano la EBBS 2013.

Saturday, July 27, 2013

Vyuo vikuu vya afya kutoa elimu ya tiba asilia

Na Mwandishi
WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema ipo haja siku zijazo kuanzishwa kwa vyuo vya elimu ya tiba ya asili na tiba mbadala ili kuwasaidia wananchi kupata huduma za afya kwa usalama zaidi.

Aidha, imewataka waganga wa tiba asili kuandika historian a taarifa za wagonjwa wanaowahudumia kwa lengo la kuwezesha kupata takwimu za kweli za wanaohudumiwa na maendeleo ya afya zao kupitia tiba hizo.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Tiba Asili na Tiba Mbadala, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Paulo Mhame aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akitoa semina kwa waandishi wa habari za afya jijini Dar es Salaam kuhusu hali ya tiba asili na tiba mbadala nchini.

Dk Mhame alisema Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala namba 29 ya mwaka 2002 iliwezesha kuundwa kwa Baraza la tiba hizo mwaka 2005 na mwaka 2010 fomu za usajili wa wanaotoa huduma hizo zikaanza kutolewa nchini ili kurasimisha huduma baada ya kuwepo waganga matapeli.

Kwa mujibu wa takwimu, mpaka sasa nchini kuna waganga 2,221 wa tiba asili waliosajiliwa, wengi wakiwa wamerithishwa tiba za kiutamaduni kutoka kwa jamii zao na waganga wasiozidi 12 wa tiba mbadala ambao hutumia vifaa kama vya hospitali.

“Nchi za wenzetu tiba za asili zinafundishwa vyuoni na kwa upande wa tiba mbadala, zipo ngazi za vyeti, stashahada na shahada ambapo mtu mwenye shahada ndio anayepaswa kupewa hadhi ya daktari lakini huku kwetu, vibao vimetapakaa kila kona vikieleza kuhusu madaktari bingwa wa tiba hizi, si sawa,” alisema Dk Mhame.

Alisema ni matarajio na dhamira ya serikali kuhakikisha kuwa, tiba inakuwa huduma kwa mwananchi na sio biashara, hivyo matarajio ya baadae ni kuona kuna vyuo vya kufundisha tiba mbadala na zile za asili, ili kukwepa madhara yanayoikumba jamii kwa sasa.

Kwa mujibu wa Dk Mhame, hivi sasa nchi za mashariki ya mbali na Asia, wanasoma darasani kuhusu tiba asili na zipo tiba zilizo rasmi kwa jamii ambazo zinatumiwa hata ngazi za kimataifa. Alisema ikiwa kwa maandishi ni rahisi kufuatilia matokeo ya tiba na afya ya mhudumiwa tofauti na ilivyo sasa.

“Natambua mnajua kila kitu kinachoitwa dawa, kina madhara, nimewahi kusikia watu wanapewa dawa za maji mpaka lita tano wakatumie, hii ni kosa kubwa kitabibu, hakuna daktari anayeweza kukupa dawa zaidi ya nusu lita, hasa hizi za kienyeji maana itachacha na kukuletea madhara, zile za kisasa zimewekewa kinga, nawaomba Watanzania muwe macho,” alisisitiza Dk Mhame.

Ingawa hakusema wazi kuwa vyuo vya elimu ya tiba asili nchini vitaanza lini, alisema ni matarajio ya mbele na kwamba jambo hilo kwa asilimia kubwa litaihusisha sekta binafsi ambayo ina waganga wengi wa tiba asili na serikali kama mtunga sera, itasimamia kama ilivyo kwa maduka ya tiba asili ambayo hivi sasa ni rasmi nchini.

Mwisho.

Serikali yatakiwa kuboresha elimu



SERIKALI imeshauriwa kuboresha mfumo wake wa utoaji elimu kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wengi kufanya vizuri katika masomo na hivyo kuondoa tatizo la vijana  wanaohitimu katika ngazi mbalimbali hasa za Sekondari kuishia mitaani.



Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu  wa Taasisi inayojishughulisha na kuwaandaa wanafunzi kusoma nje ya nchi ‘Global Education Link’ (GEL) Abduimalik Mollel, alipokuwa akizungumza na gazeti hili kuhusu maendeleo ya sekta ya elimu nchini.



Alisema mfumo wa sasa wa elimu unaotolewa nchini, kwa kiasi kikubwa umekuwa ukiwaondolea uaminifu  wazazi wengi hasa kutokana na matokeo yasiyo mazuri kwa watoto wao, suala alilosema pia linafanya wazazi hao hasa wenye uwezo kufikiria kuwapeleka watoto wao kusoma nje ya nchi.



Alisema kutokana na hali hiyo idadi ya wanafunzi kwenda kusoma nje ya nchi pia imekuwa ikiongezeka siku hadi siku tofauti na miaka ya nyuma , jambo alilosema kuwa limetokana na wazazi wao kukatishwa tamaa na mfumo huo.



“Hata hivyo siyo wazazi wote wana uwezo wa kuwapeleka watoto wao nje ya nchi kwa ajili ya kuendelea na masomo,cha muhimu ni  Serikali kuangalia upya mfumo wake wa elimu ili kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi na kuondoa tatizo lililopo sasa” alisema Mollel



Alisema hata suala la tatizo la umri lililosababisha baadhi ya wanafunzi kukosa nafasi ya kujiunga na kidato cha tano halikuwa na msingi wowote kwa kuwa hata  kabla ya kujiunga na kidato cha kwanza tayari umri wao ulijulikana  hivyo walipaswa kuwekewa utaratibu unaotambulika tangu mapema.



Akitolea mfano wa wanafunzi waliofika katika taasisi yake kwa ajili ya kutafuta nafasi ya kwenda kusoma nje ya nchi tangu kutolewa kwa matokeo ya kidato cha nne, Mollel alisema idadi yao imeongezeka tofauti na miaka mitatu hadi minne iliyopita.



Alisema katika kipindi cha kuanzia Juni hadi sasa, taasisi yake imepokea maombi zaidi ya 800 ya wanafunzi waliomaliza kidato cha nne wanaotaka kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kuendelea na elimu katika vyuo mbalimbali.



Alisema hata idadi ya mawakala wanaohusika na utafutaji wa nafasi za vyuo nje ya nchi kwa ajili ya wanafunzi wanaotaka kwenda kujiunga pia   imeongezeka na kuwa zaidi ya 20 ikilinganishwa na mawakala wawili miaka kumi iliyopita, suala alilosema limetokana na kuongezeka kwa mahitaji ya wanafunzi.





ends


Thursday, July 25, 2013

Uhaba wa mabweni: Mwanafunzi ajiua baada ya kubakwa


MWANAFUNZI wa kidato cha nne, Flora Athanas (18) wa shule ya sekondari Mzindakaya wilayani Sumbawanga mkoani
Rukwa, amejiua kwa sumu ya panya, baada ya kubakwa na mtu asiyefahamika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda, alisema jana kuwa mwanafunzi huyo alibakwa usiku wa kuamkia Jumanne ya wiki hii yeye na mwenzake mmoja, katika chumba kimoja walichopanga, kutokana na kukosekana kwa mabweni katika shule hiyo.

Kwa mujibu wa Kamanda Mwaruanda, siku hiyo Flora alikuwa na wanafunzi wenzake watatu, aliokuwa akiishi nao katika chumba hicho, maarufu geto.

Inadaiwa usiku mtu asiyefahamika, alivamia nyumba waliyokuwa wamepanga, akafunga vyumba vya wanafunzi wengine na kuingia katika chumba cha kina Flora akiwa ameshika kisu, na kuwatishia kuwa atakaye piga kelele atamuua kwa kumchoma kisu.

Kutokana na tishio hilo, inadaiwa wanafunzi hao walikaa kimya ambapo mvamizi huyo alimbaka Flora na mwenzake mmoja na kumuacha mwingine kabla ya kuondoka na kukimbilia kusikojulikana.  

Asubuhi ya siku hiyo, Flora alipoamka, inadaiwa alitoroka na kwenda katika moja ya duka lililopo kijijini hapo na kununua sumu ya panya.

Inadaiwa aliondoka na sumu hiyo kwenda katika pori lililopo nje kidogo ya Kijjiji  cha Kaengesa, ambapo hufanyika mnada wa hadhara na kuamua kukatisha maisha  yake  kikatili  kwa kunywa sumu hiyo na kufariki dunia.

“Uchunguzi wa awali wa Polisi unaonesha kuwa kifo hicho  kimesababishwa na hasira aliyokuwa nayo msichana huyo,  baada  ya kubakwa na mtu asiyejulikana hivyo akachukua  uamuzi huo mgumu wa kukatisha maisha  yake kwa kunywa  sumu inayosadikiwa kuwa ya panya,“ alisema Mwaruanda.

Kamanda Mwaruanda alisema mwanafunzi mwenzake aliyebakwa pamoja naye, alifikishwa katika kituo cha afya Kaengesa, ambapo alifanyiwa uchunguzi wa kitabibu kuthibitika kuwa alibakwa.

Katika kituo hicho cha afya, ndiko pia mwili wa marehemu ulipopelekwa kwa uchunguzi, ambako ilithibitika kuwa chanzo cha kifo hicho ni sumu ya panya.


Blog hii: inasikitishwa na tukio hilo la ubakaji na waharifu lazima wakamatwe
  


Elimu ya bongo inapoteza wenye ujuzi-- IUCEA

BARAZA la Elimu la Vyuo Vikuu vya Afrika  Mashariki (IUCEA) limesema  mfumo wa elimu nchini umekuwa ukipoteza watu wenye ujuzi wa mambo mbalimbali  kwa kigezo cha kushindwa katika mitihani ya kumaliza masomo.

Katibu Mtendaji wa wa baraza hilo, Profesa Mayunga Nkunya alisema wanafunzi wasihukumiwe kwa kushindwa mtihani bali aangaliwe upande mwingine, ni nini anaweza kufanya kuinua uchumi.

“Utaratibu wa sasa wa elimu unakotupeleka hakufai kabisa…kigezo cha kuangalia kufaulu ama kufeli tu kwa mwanafunzi sio suala jema kwani wapo wengi wanaokuwa wavumbuzi na wenye ujuzi mbalimbali ambao hawapewi nafasi,” alisema Profesa Nkunya na kutaja, Rwanda kwamba  wanaotekeleza mfumo unaompandisha mtu alipo bila kuangalia mtihani.

Profesa  Nkunya alisema hayo Dar es Salaam wakati akizungumzia ushirikiano uliopo kati yao na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) katika kupambana na  ukosefu wa ajira kwa vijana.

Mabaraza hayo yameandaa mkutano wa Afrika Mashariki wenye kujadili mahitaji ya soko la ajira kwa kuzingatia taaluma. Mkutano huo utafanyika Oktoba 24 na 26 jijini Nairobi, Kenya.

Alisema Baraza hilo litatayarisha mkakati wenye kujikita zaidi katika kuangalia ujuzi kwenye taaluma kama ilivyo Rwanda ambao utahakikisha suala la elimu linaendana na ajira katika nchi hizo.