Help Children
Love them
Saidia Watoto

Thursday, July 25, 2013

Uhaba wa mabweni: Mwanafunzi ajiua baada ya kubakwa


MWANAFUNZI wa kidato cha nne, Flora Athanas (18) wa shule ya sekondari Mzindakaya wilayani Sumbawanga mkoani
Rukwa, amejiua kwa sumu ya panya, baada ya kubakwa na mtu asiyefahamika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda, alisema jana kuwa mwanafunzi huyo alibakwa usiku wa kuamkia Jumanne ya wiki hii yeye na mwenzake mmoja, katika chumba kimoja walichopanga, kutokana na kukosekana kwa mabweni katika shule hiyo.

Kwa mujibu wa Kamanda Mwaruanda, siku hiyo Flora alikuwa na wanafunzi wenzake watatu, aliokuwa akiishi nao katika chumba hicho, maarufu geto.

Inadaiwa usiku mtu asiyefahamika, alivamia nyumba waliyokuwa wamepanga, akafunga vyumba vya wanafunzi wengine na kuingia katika chumba cha kina Flora akiwa ameshika kisu, na kuwatishia kuwa atakaye piga kelele atamuua kwa kumchoma kisu.

Kutokana na tishio hilo, inadaiwa wanafunzi hao walikaa kimya ambapo mvamizi huyo alimbaka Flora na mwenzake mmoja na kumuacha mwingine kabla ya kuondoka na kukimbilia kusikojulikana.  

Asubuhi ya siku hiyo, Flora alipoamka, inadaiwa alitoroka na kwenda katika moja ya duka lililopo kijijini hapo na kununua sumu ya panya.

Inadaiwa aliondoka na sumu hiyo kwenda katika pori lililopo nje kidogo ya Kijjiji  cha Kaengesa, ambapo hufanyika mnada wa hadhara na kuamua kukatisha maisha  yake  kikatili  kwa kunywa sumu hiyo na kufariki dunia.

“Uchunguzi wa awali wa Polisi unaonesha kuwa kifo hicho  kimesababishwa na hasira aliyokuwa nayo msichana huyo,  baada  ya kubakwa na mtu asiyejulikana hivyo akachukua  uamuzi huo mgumu wa kukatisha maisha  yake kwa kunywa  sumu inayosadikiwa kuwa ya panya,“ alisema Mwaruanda.

Kamanda Mwaruanda alisema mwanafunzi mwenzake aliyebakwa pamoja naye, alifikishwa katika kituo cha afya Kaengesa, ambapo alifanyiwa uchunguzi wa kitabibu kuthibitika kuwa alibakwa.

Katika kituo hicho cha afya, ndiko pia mwili wa marehemu ulipopelekwa kwa uchunguzi, ambako ilithibitika kuwa chanzo cha kifo hicho ni sumu ya panya.


Blog hii: inasikitishwa na tukio hilo la ubakaji na waharifu lazima wakamatwe
  


0 comments:

Post a Comment