Help Children
Love them
Saidia Watoto

Thursday, May 2, 2013

Wafugaji kupewa elimu Dodoma


ZAIDI ya wananchi laki tano wanaojihusisha na kilimo na ufugaji wa kuku wa kienyeji wanatarajiwa kunufaika na elimu iliyolenga kuwainua kiuchumi ifikapo mwaka 2016.

Elimu hiyo inayoendeshwa katika wilaya 20zilizopo katika mikoa nane ya kanda ya kati, inatolewa kupitia mradi wa ukuzaji wa masoko vijijini (RLDC) kwa ushirikiano na nchi ya Uswisi.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na elimu hiyo, Meneja wa mradi huo Francis Massawe alisema hatua hiyo inayotolewa kupitia kwa maafisa ugani, zaidi imejikita kutoa elimu inayowasaidia wakulima  na wafugaji wa kuku wa kienyeji kuwa na mbinu katika maeneo yao.

Alisema katika kufanikisha malengo hayo RLDC imekuwa ikiwawezesha wakulima na wafugaji hao kufuata njia sahihi zikiwemo za utumiaji wa mbinu za kisasa za kilimo  ili kupata mavuno yaliyo bora na hivyo kujiongezea kipato.

"Hii ni awamu ya nne ya utekelezaji wa mradi wetu tangu ulipoanzishwa mwaka 2005, malengo ni kuwainua wakulima kutoka mahali na kwenda mbali zaidi" alisema Massawe.

Alisema mradi huo umejikita katika mikoa ya kanda ya kati, kutokana na ukweli kuwa wananchi wa maeneo hayo wanakabiliwa na changamoto nyingi zinazowafanya washindwe kutekeleza ipasavyo shughuli za kilimo ikiwemo ukame.

"Tumejikita zaidi katika ukulima wa zao la alizeti, mpunga na ufugaji wa kuku wa kienyeji na tumeona maeneo hayo hayo yakisimamiwa ipasavyo yataweza kuwainua wananchi kutokana na umuhimu wake hasa kibiashara" alisisitiza meneja huyo.

Alisema utekelezaji wa awamu tatu zilizopita, umekuwa  na mafanikio makubwa hasa baada ya wakulima wengi kufanikiwa kupata mazao mengi yaliyowafanya baadhi yao kujenga nyumba za kisasa.

Alisema matarajio yao ifikapo mwisho wa utekelezaji wa awamu ya nne mwaka 2016,  wataweza kuwa wamewafikia wakulima na wafugaji karibu milioni moja na hivyo kuwa wamewasaidia kuwainua kiuchumi kupitia biashara za mazao yao.

Aidha alisema mradi huo unatekelezwa katika mikoa ya Morogoro, Singida, tabora, Shinyanga, Manyara, Simiyu na Geita.
MWISHO.

0 comments:

Post a Comment