Help Children
Love them
Saidia Watoto

Saturday, December 22, 2012

Hii imekaaje eti waliofaulu darasa la 7 kufanya mtihani upya




Waliofaulu kujiunga na masomo ya sekondari katika shule za Serikali, lakini watalazimika kufanya mtihani mwingine wa taifa ili kuwabaini wanafunzi ambao hawajui kusoma wala kuandika.

Mtihani huo kwa mujibu wa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa utatungwa na wizara hiyo na watafanya wanafunzi wote watakaokuwa wameanza masomo ya sekondari na wale watakaobainika hawajui kusoma wala kuandika, watafutiwa usajili wao.
  
WANAFUNZI hao ni 560,706 wa shule ya msingi sawa na ongezeko la asilimia 8.8


Dk Kawambwa ambaye jana alitangaza matokeo ya mtihani wa elimu ya shule ya msingi ambao uliofanyika Septemba mwaka huu, alisema wizara imechukua uamuzi huo baada ya mwaka jana kupokea majina ya wanafunzi wapatao 4,000 waliojiunga na masomo ya sekondari wakati hawajui kusoma wala kuandika.

“Tutafanya hivyo kila mwaka ili kuhakikisha wanafunzi wanaojiunga sekondari ni wale tu wenye uwezo ambao wanastahili kujiunga na kiwango hicho cha elimu,” alisema Dk Kawambwa.

Mtihani wa kuchagua

Wanafunzi hao waliofaulu walifanya mtihani ulio kwenye mfumo wa maswali ya kuchagua ambao umekuwa ukilalamikiwa na wadau wa elimu kuwa ni mfumo dhaifu unaosababisha wanafunzi wanaofaulu wasiwe na uwezo wa kujieleza na kupambanua mambo.

Katika makongamano kadhaa ya elimu ya hivi karibuni yakiwashirikisha walimu na wasomi wa vyuo vikuu, wadau walishutumu mfumo huo kuwa unasaidia kufaulisha wanafunzi wasio jua kusoma na kuandika, lakini pia wanafunzi wanakosa uwezo wa kujieleza kwa ufasaha.

Katika mikoa ya Dar es Salaam na Katavi, baadhi ya wananchi na wanafunzi ambao walipata fursa ya kutoa maoni mbele ya Tume ya Marekebisho ya Katiba nao walishutumu mfumo wa elimu na kutaka mitaala irekebishwe ili kuwezesha wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi wawe na uwezo wa kujiajiri na
kujieleza pia.

Lakini Dk Kawambwa alitetea mfumo huo kuwa ni mfumo bora na umekuwa ukitumika miaka mingi na unawashirikisha walimu katika kutunga maswali. Alisema mfumo huo unatoa fursa ya mwanafunzi kuchagua jibu sahihi kati ya majibu manne yanayofanana kwa ukaribu.

“Sio mfumo rahisi kama unavyodai, ni mfumo ambao mwanafunzi anatakiwa awe makini katika kuchagua jibu,” alisema Dk Kawambwa na kujitetea kuwa sio Tanzania pekee inayofuata mfumo huo.

Kompyuta msahishaji

Waziri licha ya kutetea mfumo huo wa maswali ya kuchagua, alisema mtihani huo ulikuwa wa kwanza nchini kusahihishwa kwa kutumia teknolojia mpya ya Optical Mark Reader (OMR) ambayo kompyuta ilitumika kusahihisha mtihani huo.

Mfumo huo wa usahihishaji kwa mujibu wa Dk Kawambwa umesaidia kupunguza gharama kwani walimu wapatao 250 tu ndio walishiriki kusimamia usahihishaji kwa wiki mbili wakati mwaka jana walitumia walimu 4,000 kusahihisha mtihani kwa mwezi mzima.

“Hebu fikiria hizo gharama tulizokuwa tunainga kuliweka kundi lote hilo kambini kwa mwezi mmoja ni kipindi kirefu na fedha nyingi zinatumika, teknolojia hii imesaidia kupunguza gharama kwa Serikali,” alisema Waziri.

Ufaulu wa wanafunzi

Katika matokeo ya mtihani huo, Dk Kawambwa alisema wanafunzi waliofaulu ni asilimia 64.74 ya wanafunzi 865,827 waliofanya mtihani huo. Awali idadi ya wanafunzi ambao walisajiliwa kufanya mtihani ilikuwa ni 894,839 hivyo idadi ya waliofanya ni asilimia 96.76.

Watahiniwa 29,012 sawa na asilimia 3.24 hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro, vifo na ugonjwa. Kati ya hao wasichana ni 12,501 na wavulana ni 16,511.

Waziri alisema matokeo hayo yanaonesha kuwa alama ya juu kabisa ilikuwa 234 kati ya 250 kwa wasichana na wavulana.

Alifafanua kuwa watahiniwa 3,087 walipata alama A, wanafunzi 40,683 walipata alama B, wanafunzi 22,103 walipata alama C wakati watahiniwa 73,264 walipata alama E.

Kati ya wanafunzi 560,706 ambao wamefaulu kati ya hao wasichana ni 281,460 sawa na asilimia 50.20 na wavulana ni 279,246 sawa na asilimia 49.80.

Takwimu hizo zinaonesha pia kwamba idadi ya waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza imeongezeka kwa asilimia 8.8 ikilinganishwa waliochaguliwa awamu ya kwanza mwaka jana.

Udanganyifu wapungua

Dk Kawambwa amesema vitendo vya udanganyifu vimepungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na mwaka jana. Alisema mwaka huu, idadi hiyo imepungua hadi kufikia wanafunzi 296 tu ambao wamefutiwa matokeo kwa udanganyifu wakati mwaka jana idadi hiyo ilikuwa ni 9,736.

“Serikali itawabaini wale wote waliohusika katika udanganyifu huo na kuwachukulia hatua stahiki,” alisema Dk Kawambwa.



0 comments:

Post a Comment