Help Children
Love them
Saidia Watoto

Tuesday, April 9, 2013

Kushindwa kusoma na kuandika kunapelekea wazazi kushindwa kuchangia elimu



IMEELEZWA kutokana na asilimia kubwa ya wazazi kutojua kusoma na kuandika, wamekuwa wakishindwa kuchangia michango mbalimbali ya maendeleo ya elimu ili kukuza sekta hiyo ambayo imeonekana kushuka.

Hayo yameelezwa na mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Mercy Silla wakati wa ufunguzi wa bweni la wasichana katika sekondari ya Vianzi iliyopo tarafa ya Vianzi wilaya ya Mkuranga ambapo limegharimu Sh 88 milioni hadi kukamilika kwake.

Silla alisema asilimia 57 ya watu wazima katika wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani hawajui kusoma na kuandika  hali inayopelekea wazazi hao washindwe kuchangia maendeleo ya elimu kutokana na kutojua nini umuhimu wa elimu.

Alisema wazazi wanatakiwa kujenga utamamduni wa kuchangia maendeleo na sio kusubiri wahisani na wafadhili mbalimbali kuja kutoa misaada ya maendeleo ya elimu.

“ Huu ni wakati  kwa wazazi kujenga utamaduni wa kuchangia miradi ya maendeleo ya elimu na sio kusubiri misaada toka wahisani na wafadhili”alisema.

Naye Mkurungezi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu nchini(Tea) Rosemary Lulabuka alisema lengo la kujenga bweni hilo ni kusaidia watoto wa kike ambao wanapata shida ya kutembea umbali mrefu kutoka nyumbani hadi shuleni hapo.
Lulabuka alisema bweni hilo  lilikamilika mwishoni mwa mwaka juzi lakini halikuweza kutumika kutokana na uwezo mdogo wa wananchi katika kuchangia ununuzi wa vitanda na magodoro.

“Bweni lina jumla ya vitanda 36  vya juu na chini(Double decker) vyenye magodoro 72 na  linachukua wanafunzi 72 na lina mabafu matano na vyoo nyeye matundu matano, pia mamlaka yangu imejitolea kufunga umeme wa jua kwa ajili ya wanafunzi hao kujisomea wakati wa usiku” Alisema  Lulabuka.
Mwisho

0 comments:

Post a Comment