Help Children
Love them
Saidia Watoto

Sunday, April 21, 2013

Habari ya elimu kama ilivyojitokeza katika Habari Leo ya Leo

Serikali yarudi katika
mazungumzo na walimu
*Yaahidi mishahara bora watumishi wa chini
*Yahoji kuhusu nia njema ya Mukoba wa CWT
*Ni kwa kupotosha ukweli wa mazungumzo
Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imerejea katika meza ya mazungumzo na Chama cha Walimu Tanzania (CWT), pamoja na kutokuwepo kwa mazingira ya nia njema kutoka upande wawawakilishi wa walimu katika mazungumzo hayo.

Taarifa ya Ikulu iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, ilieleza kwamba Serikali imefikia hatua hiyo, ili kuonesha utayari na nia njema katika mazungumzo hayo.

Mbali na utayari, pia Serikali imetangaza kwamba kutakuwepo na nyongeza nzuri kwenye mishahara, hasa ya watumishi wa ngazi za chini katika mwaka ujao wa fedha. 
Kabla ya hatu hiyo, vyombo vya habari vilimkariri Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba
akisema kwamba Serikali imekataa kukaa meza moja na CWT, ili kuzungumzia nyongeza ya mishahara na posho za walimu, pamoja na kwamba chama hicho chenyewe kiko tayari kwa mazungumzo.

Mukoba pia alikaririwa akidai kwamba Serikali imepuuza amri ya Mahakama, inayotaka pande hizo mbili kukaa meza moja kujadili madai ya walimu.

Kutokana na madai hayo, Mukoba alilitaka Bunge na wazazi, kuingilia kati uamuzi wa Serikali kukataa kukaa meza moja na CWT.

Nia njema
“Serikali inapenda kuwafahamisha wananchi kuwa, madai haya yote hayana chembe ya ukweli, na hayana nia njema, maana yanaweza kujenga chuki na mazingira ya kuzua mgogoro mwingine na Serikali usio na sababu, wala maslahi kwa walimu wenyewe na Taifa,” imeeleza taarifa hiyo ya Ikulu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Serikali imeeleza kuwa haijakataa majadiliano na CWT, na wala haijapuuza amri ya Mahakama inayotaka pande zote mbili kurudi kwenye meza ya majadiliano. 

Tofauti na madai ya Mukoba, taarifa ya Serikali ilieleza kuwa tangu amri ya Mahakama itolewe, tayari vimefanyika vikao vinne vya Baraza la Majadiliano ya Pamoja katika utumishi wa walimu. 

“Vikao viwili vilifanyika mwaka jana Septemba 12, na  Desemba 5. Vikao viwili tayari vimefanyika mwaka huu Januari 9-10 na Machi 22,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo ilifafanua kwamba kilichochelewesha suala la mishahara na posho kujadiliwa katika vikao hivyo, si kwamba Serikali haikutaka mjadala huo. 

“Sababu hasa ni kuwa CWT ilikata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu, katika kesi Na. 96/2012, na Serikali iliwasihi viongozi wa CWT wafute rufaa hiyo, ili kuruhusu majadiliano ya mishahara na posho, lakini walikataa. 

“Kitendo hicho hakioneshi nia njema upande wao. Nia njema ni sharti muhimu kwenye majadiliano haya. Kwa upande wake, ili kuonesha utayari na nia njema, Serikali sasa imekubali majadiliano hayo yaendelee, licha ya CWT kukataa kufuta rufaa yao,” ilieleza taarifa hiyo. 

Serikali imeelezea sababu ya pili iliyochelewesha majadiliano ya maslahi ya walimu, kuwa ni madai ambayo awali viongozi wa CWT walikuja nayo kuwa iteuliwe timu maalum ya kuzungumzia maslahi, badala ya Baraza la Majadiliano ya Pamoja katika utumishi wa walimu, ambalo ndilo lipo kisheria kwa majadiliano hayo. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, CWT ilichelewa kurejesha majadiliano kwenye Baraza hilo, mpaka wakati wa kikao cha Januari 9 hadi 10, mwaka huu.

Uzushi wa Mukoba
Wakati Mukoba alikaririwa kwamba kikao kilichokataa kuzungumzia mishahara na posho za walimu, ni  kilichofanyika Aprili 2 mwaka huu, chini ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Serikali imepinga madai hayo.  

“Si kweli vilevile kuwa kikao kilichofanyika Ikulu, Aprili 2, mwaka huu chini ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi  Sefue, ndicho kilikataa majadiliano kuhusu maslahi ya walimu. 

“Kauli hiyo ni upotoshaji wa makusudi usio na nia njema. Viongozi wa CWT wanajua vema kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, si sehemu ya mfumo wa majadiliano kuhusu maslahi ya walimu. Hivyo, kikao kinachoongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi, hakiwezi kuwa mahali pa majadiliano ya mishahara, posho na maslahi ya walimu,” ilieleza taarifa hiyo. 

Ilifafanuliwa kwamba mkutano huo wa Aprili 2, uliitishwa na Katibu Mkuu Kiongozi kwa maombi rasmi yauongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), ambao walitaka kujulishwa jinsi utaratibu wa majadiliano ya mishahara ya wafanyakazi wote utakavyokuwa, kutokana na kuanzishwa kwa mzunguko mpya wa Bajeti ya Serikali.
Serikali imeeleza kuwa kikao hicho kisingeweza kugeuka na kuwa kikao cha kujadili mishahara na posho za walimu, kama alivyokaririwa Mukoba akidai.

“Tunapenda wananchi na walimu wajue pia kuwa Gratian Mukoba, hakuwepo kwenye hicho kikao cha Aprili 2, 2013. Aidha, kikao hicho kilikuwa cha Tucta, hakikuwa cha CWT,” ilideleza taarifa hiyo.

*Dhamira ya CWT
Serikali imeelezea kupata tabu ya kuelewa nia na dhamira ya viongozi wa CWT, kwa kupotosha kwa makusudi wananchi na walimu kwa mambo yaliyo wazi “Serikali imeonesha nia na dhamira ya wazi ya kujadiliana na CWT, pamoja na vyama vyote vya wafanyakazi, kuhusu maslahi ya wafanyakazi. 

Vikao vingi vilivyofanyika na vinavyoendelea kufanyika kwenye mabaraza ya kisekta na Baraza Kuu, ni ishara ya wazi ya nia njema ya Serikali. 

“Tunajiuliza, katika hali hiyo, juhudi hizi za viongozi wa CWT kuandaa mazingira ya mgogoro wa Serikali lengo lake ni nini hasa?” Ilihoji taarifa hiyo.

0 comments:

Post a Comment