Help Children
Love them
Saidia Watoto

Wednesday, August 14, 2013

Watoto 562 Pemba warejeshwa shule

WATOTO 562 wanaoishi katika mazingira magumu Pemba yaliyosababisha waache shule, wametambuliwa na kusajiliwa.

Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa wa Jumuiya ya Piro, inaowatambua watoto hao, Said Mohamed alisema, baada ya kuwatambua, wamewaorodhesha ili kuwasaidia kuwarudisha shule watoto waliojiingiza katika ajira hizo.

“Jumuiya ya  PIRO ambayo imepewa jukumu la kuwasajili watoto wanaojiingiza katika ajira ngumu, imeorodhesha   watoto 562 katika kisiwa cha Pemba,” alisema.

Akifafanua zaidi alisema watoto 125 wamesajiliwa katika kijiji cha Kangagani,wakati watoto 125 wametambuliwa katika kijiji cha Kiuyu katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Aidha watoto wengine 187 wamesajiliwa na kuondolewa katika ajira ngumu ya watoto, katika wilaya ya Micheweni ambao walikuwa wakijishughulisha na kazi za kugonga kokoto
katika miamba ya mawe.

Mohamed alisema watoto 125 waliondolewa katika ajira ngumu za watoto, baada ya kugundulika wakifanya kazi hizo katika  kijiji cha vitongoji kwa kufanya kazi za uvuvi na kukata miti aina ya mikoko.

“Tumefanikiwa kuwaondowa katika ajira ngumu watoto 562 na kuwarudisha shule kwa ajili ya masomo...ajira mbaya kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa kuziondowa kisiwani Pemba,” alisema.

Ofisa huyo ameipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kwa  kukubali kuwapokea watoto walioanza masomo yao katika shule za msingi.

Alisema tayari wanafunzi 200 kutoka Pemba wamerudi shule na kuanza masomo baada ya kutoroka kwa zaidi ya miaka miwili na kujitumbukiza katika ajira ngumu.

“Tunaipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na Wizara ya Kazi Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ustawi wa Jamii, kwa kushirikiana na kupata ufumbuzi wa tatizo la ajira ngumu kwa watoto na kuwawezesha kuanza masomo,” alisema.

Alisema familia zipatazo 120 zimewezeshwa kwa kupewa vifaa mbali mbali pamoja na  madaftari kwa ajili ya wanafunzi waliorudi shule na kuanza masomo.

Mradi wa kuwarudisha wanafunzi shule waliotoroka unafadhiliwa na jumuiya ya Ulaya na
kusimamiwa na Shirika la watoto Save Children Fund ambapo jumuiya zisizokuwa za
kiraia pamoja na TAMWA NA PIRO iliopo Pemba ndiyo zinazosimamia utekelezaji wa mradi
huo.

0 comments:

Post a Comment