Help Children
Love them
Saidia Watoto

Tuesday, August 20, 2013

Mama Pinda asikitikia matunzo duni ya wanafunzi wa kike


MKE wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda amesema ipo haja ya kuweka juhudi za makusudi za kuwezesha wasichana nchini kuondokana na aibu zinazowazuia kuhudhuria masomo yao kila siku.

Alisema  kukosekana kwa vifaa vya kujisitiri miongoni mwa wasichana waliofikia balehe, ni miongoni mwa sababu zinazowafanya wakose masomo kati ya siku 30 hadi 70 kwa mwaka jambo ambalo linachangia kudorora kwa elimu miongoni mwao.


Alitoa kauli hiyo jana wakati akizindua Mradi wa Hakuna Wasichoweza katika Shule ya Msingi Chilongola, iliyoko Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkoani Mtwara.


Mradi huo unafadhiliwa na Taasisi ya T-MARC inayojihusisha na Masuala ya Afya na Maendeleo, umelenga kuwafikia wasichana 10,000 katika wilaya mbili za mkoa wa Mtwara, yaani Manispaa ya Mtwara Mikindani na Wilaya ya Mtwara Vijijini.


 “Wasichana wengi wanapopata siku zao, hushindwa kuhudhuria masomo yao kati ya siku tatu hadi saba kwa mwezi au siku kati ya siku 30 hadi 70 kwa mwaka. Hii husababishwa na wasichana hawa kukosa nyenzo za uhakika za kujisitiri wakiwa shuleni. Wengi wao huamua kubaki nyumbani hadi pale mzunguko wao utakapokwisha ili kuepuka kuaibika...,”  alisema.


Alisema usiri na ufahamu mdogo wa jamii kuhusu masuala ya hedhi na changamoto wanazozipata wasichana katika kipindi hiki pia ni tatizo kubwa.


“Wengi wetu katika jamii inayotuzunguka bado tunalichukulia suala la hedhi kuwa suala la aibu na la siri kubwa, kwa hiyo matatizo yanayotokana na hali hii ya kawaida hubaki bila kushugulikiwa, kwani kila mtu anaona aibu kusema wazi kuwa kuna tatizo,” aliongeza.


0 comments:

Post a Comment