Help Children
Love them
Saidia Watoto

Thursday, August 22, 2013

Wanafunzi elimu ya juu waonywa dhidi ya siasa






Na Mwandishi Wetu

WANAFUNZI wa vyuo vya elimu ya juu nchini wameonywa dhidi ya kuteua au kuchagua wajumbe wa kisiasa kugombea uongozi nchini.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu Mtendaji wa Taasisi ya Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso), Donati Salla, ilisema hilo ni jukumu la vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu na vinavyotambulika.

“Shughuli za serikali za wanafunzi katika vyuo vya elimu ya juu ni masuala ya wanafunzi na ubora wa taaluma itolewayo katika chuo husika na mengine ya kitaifa, lakini si kwa ushabiki wa kisiasa au kutetea kundi au maslahi ya watu fulani,” ilisema taarifa hiyo.

Ilisema vikao vyote vinavyohusu mjumuiko wa serikali za wanafunzi, vinapaswa kuitishwa na kuratibiwa na Tahliso na si taasisi nyingine yoyote.

Taarifa hiyo ilitolewa kutokana na mkutano wa baadhi ya viongozi wa serikali za wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini uliofanyika Morogoro, ukikutanisha baadhi ya viongozi waandamizi wa wanafunzi ukiandaliwa  na Taasisi ya Kupambana na Maadui Ujinga, Maradhi na Umaskini (FPID).

Mkutano huo ulijadili masuala ya utofauti wa kipato kwa Watanzania, ubora wa elimu hasa vijijini na fursa za ajira.

“Lakini kubwa lililoibuka katika mkutano huu na kuchukua uzito mkubwa ni suala la nani awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015,” ilisema taarifa na kuongeza kuwa Tahliso ilisikitishwa na kulaani matukio yaliyojitokeza katika mkutano huo, kwani ni kinyume na maadili ya elimu ya juu nchini.

Kutokana na hilo, Tahliso katika taarifa yake, ilitamka bayana kuwa mkutano ulioitishwa Morogoro ni batili na hautambuliki kwa mujibu wa sheria namba 7 ya vyuo vikuu ya mwaka 2005, sheria ya mashirika yasiyokuwa ya Serikali namba 24 ya mwaka 2002 na Katiba ya Tahliso.

Na ilitoa onyo kwa viongozi wa serikali za wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu ambao walishiriki mkutano huo na kutaka wasirudie, “na vinara wa wanafunzi ambao walikuwa mstari wa mbele kuchochea masuala ya kisiasa bila kufuata utaratibu watawajibishwa ipasavyo”.

Ilipiga marufuku  wanafunzi au makundi ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kuendesha harakati za siasa kwa kutumia jina la chuo, vyuo au taasisi yoyote inayoshughulika na elimu ya juu nchini.

“Tahliso itawaandikia barua waadili wote wa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu na kuwapa hadidu za rejea kuhusu utaratibu wa kubaini vikao halali na batili ili kuratibu vema ruhusa kwa viongozi wa serikali za wanafunzi, ili kuhudhuria mikutano ambayo iko nje na taratibu za chuo husika na inayohusu masuala ya wanafunzi kitaifa au vinginevyo,” ilisema taarifa.

Ilikumbusha wanafunzi wa elimu ya juu nchini jukumu lao la kusoma na kujifunza taaluma zao kwa taratibu zilizoainishwa na chuo husika. “Hicho ndicho kilichowapeleka chuoni, kwa hiyo wafanye masomo kwanza, chama chao ni taaluma, kisha siasa wafanye baadaye”.



 

0 comments:

Post a Comment