Help Children
Love them
Saidia Watoto

Friday, October 19, 2012

NMB imefanikisha kwa kiasi kikubwa elimu kwa Mama Shujaa wa Chakula na shindano la Maisha Plus kwa ujumla

                                             Baadhi  ya watu waliohudhuria siku hiyo
                         Meneja Masoko wa NMB Imani Kajula akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Wizara ya Sayansi na Teknolojia January Makamba 
          Baadhi ya akina mama walioshiriki shindanoa hilo wakiwa wanasubira mshindi kutangazwa
Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia January Makamba akimkabidhi tuzo mshindi wa shindanoa la Mama Shujaa wa Chakula 2012 Sister Marta

Habari Kamili
Benki ya NMB imefanikisha upatikanaji wa elimu kwa washiriki wa shindano la Mama Shujaa wa Chakula lililokuwa liliendelea katiak shindano la Maisha Plus

Elimu iliyotolewa ni pamoja na elimu ya biiashara, kilimo, ujasiriamali na nyinginezo ambapo Meneja Masoko wa NMB, Kajula alisisitiza kuwa benki hiyo imekuwa ikitoa mikopo mingi sana kwa akina mama pia ili kuwawezesha zaidi kimaisha.



UTAMADUNI  wa kupika, kula, kulima na kumwagilia vijijini huku wakikutanishwa watu wa makabila, dini na mila tofauti ni utamaduni ambao ni mara chache kuukuta katika  jamii zetu.

Ikiwa ni kwa mara ya kwanza kutokea katika shindano la Maisha Plus,  ambapo kulikuwa na shindano ndani yake lililojulikana kama Mama Shujaa wa Chakula ndani ya shindano hilo la Maisha Plus.

Katika shindano la Mama Shujaa wa Chakula akina mama kutoka vijiji, wilaya na mikoa mbalimbali nchini,  walipata fursa ya kukaa, kulima, kumwagilia mazao na kula pamoja vyakula vya aina mbalimbali.

Utamaduni kama huu ni mzuri kwa wanajamii ya Tanzania, kwa kuwa ilikuwa ni sehemu mojawapo ya kujifunza masuala mbalimbali ya kijamii, hususan suala la kilimo.
Shindano hilo lililofikia tamati Jumanne iliyopita,  lilikuwa ni la kuvutia kwa kuwa akina mama hao kwa siku 14 walizokaa kijijini humo,  walipata nafasi ya kupewa elimu ya kilimo, ujasiriamali, haki za kumiliki ardhi, masuala ya afya na pia hata masuala ya katiba pia.

Akizungumza na gazeti hili, Mratibu wa Shindano hilo,  Masoud Ali Kipanya, anasema kuwa ameamua kuwashirikisha akina mama wanaojishughulisha na kilimo katika shindano la Maisha Plus 2012 kwa kuwa anatambua mchango wa kilimo katika maendeleo ya nchi.

Kipanya anasema kuwa ili kuongeza motisha ya kutambua, kupenda na kuendeleza kilimo kwa wananchi, ameona kuwa kupitia kipindi hicho ni muda muafaka wao kujionea na kujipatia elimu ya kilimo.

Anasema kuwa wakiwa kijiji hapo,  wanawake wamelima, kupanda  na kuotesha miche mbalimbali kwa msaada wa kitaalamu kutoka shirika la Oxfam.

“Najua tulizunguka mikoa na wilaya karibia zote hapa nchini kusaka hawa akina mama ambao wamekuja kushiriki katika shindano hili, tunashukuru msaada kutoka kwa shirika la Oxfam kwa kuwa wameonesha nia ya kweli ya kutusaidia katika kufanikisha hatua hii muhimu,” anasema Kipanya.

Jumanne iliyopita ambapo ilikuwa ndio Siku ya Chakula Duniani, washindi walitajwa na kupatiwa zawadi zao.

Mkulima Marta Waziri kutoka wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, ndiye aliyeshinda Tuzo ya kuwa Mama Shujaa wa Chakula mwaka huu.

Mwanamama huyo alipewa zawadi ya vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh milioni kumi, ambapo aliwashinda wenzake 14.

Aliyeshika nafasi ya pili ni Elimiana Eligaesha kutoka wilaya ya  Karagwe mkoani Kagera  na wa tatu ni Tatu Abdi. Wote watatu watapatiwa mafunzo ya kilimo na ujasiriamali.

 Utamaduni huo unaongeza hamasa kwa vijana na watu wengine waliofuatilia shindano hilo, kwa kuwa mchezo  huo wa runinga, ulikuwa unaburudisha na kuelimisha pia.

Kuna changamoto nyingi zinazowakabili wakulima vijijini hasa akina mama. Akinamama hao hawakusita kufikisha ujumbe wao kwa Rais Jakaya Kikwete, wakilalamikia matatizo  yanayowakabili.

Katika barua yao ya wazi kwa Rais Kikwete,  walilalamikia suala la wawekezaji kupewa kibali cha kumiliki ardhi kwa miaka 99,  ambapo walitaka miaka hiyo ipunguzwe hadi iwe miaka mitano.

Pia, walilalamikia kudharauliwa na mabwana shamba kwa kushindwa kwao kutekeleza majukumu yao. Pia, walitoa changamoto kwa waandishi wa habari na wadau wengine muhimu wa serikali, kuhakikisha kuwa wanawasaidia wakulima kiujumla.

Naibu Waziri wa Wizara ya Sayansi na Teknolojia,  January Makamba,  alikuwa mgeni rasmi katika utoaji tuzo huo. Anasema ili kumwezesha mwanamke kushiriki kikamilifu katika kilimo, anatakiwa kupewa moyo.

Anasema taasisi mbalimbali za kutoa mikopo ya pembejeo za kilimo,  asilimia moja ya akina mama ndio hunufaika na mikopo hiyo huku asilimia 99 ya wasiozalisha chakula ndio wanamiliki ardhi.

Anasema hata katika kilimo cha umwagiliaji,  wanaume ndio hunufaika zaidi,  ikilinganishwa na akinamama hao pia hupata shida katika kupatiwa huduma za ugani.
“Ni kwamba hawa wa akinamama wakulima wana majukumu makubwa na muhimu katika kuzalisha chakula hasa katika ngazi za vijijini, lakini utakuta akizalisha chakula na kuuza, lakini utakuta mume ndio huchukua faida yote na kuondoka nayo,” alisema Makamba.

Meneja Masoko wa Benki ya NMB ambao ni wadhamini wakuu wa shindano hilo,  Imani Kajula,  alisema kuwa benki hiyo mpaka sasa imeshatumia zaidi ya Sh bilioni 100 kusaidia kilimo.

Anasema kuwa wameweza kutoa elimu ya kilimo na ujasiriamali kwa akinamama, waliokuwepo katika shindano hilo na kwa wanawake wakulima.

Mkurugenzi Mkazi wa Oxfam, Monica Gorman,  anasema kuwa shirika lake linatambua namna ambavyo wakulima wanawake wanavyohangaika katika kujiendeleza.

Anasema kuwa wanatakiwa kupewa elimu ya kutosha, kusaidiwa kifedha kwa ku
pewa mikopo pamoja kutokatishwa tamaa.

Shirika lisilo la kiserikali la Kaluwa Development Trust Fund,  linahamasishwa na kuwasaidia wakulima wadogo, ambapo liliwakabidhi vifaa vya kilimo akinamama hao.
Shanila Habib Kaluwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo. 

Anasema kuwa wakiwa kama wadau wa kilimo mkoani Morogoro na Dar es Salaam,  wameshiriki katika kuwasaidia kielimu na kitaalamu akinamama shujaa hao na wengine wa mikoani.

“Najua huu kwanza wa kuwaweka akinamama hapa kijijini na kuwaendeleza kitaaluma katika kilimo ni kitu muhimu, hivyo sisi kama wadau tunatoa pampu za maji na bidhaa nyingine za kilimo na ni vema pia watu wengine wakajitokeza kusaidia suala hilo,” anasema Shanila.
Mwisho






0 comments:

Post a Comment