Help Children
Love them
Saidia Watoto

Wednesday, February 15, 2012

Uhaba wa vitabu shuleni nini chanzo


WADAU wa elimu wamekuwa wakitoa sababu mbalimbali zinazopelekea wanafunzi kushindwa kufanya vema katika masomo pamoja na mitihani yao ya mwisho.

Ukosefu wa vitabu ni moja kati ya sababu za msingi ambazo zinasababisha wanafunzi kushindwa kufanya vema katika masomo yao.

nhjghjg.jpgLicha ya serikali kupitia wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kutoa ruzuku kwa shule mbalimbali za serikali kuanzia za msingi mpaka sekondari lakini bado hali sio shwari katika upatikanaji wa vitabu hivyo.

Ukosekanaji wa vitabu hivyo unasababaishwa na sababu mbalimbali moja wapo ikiwa ni mazingira tata ya upatikanaji wa tenda za kununulia vitabu hivyo.

Kuna tetesi kuwa wakuu wa shule ndio hutoa fedha za kununulia vitabu hivyo na hivyo kuwa katika mazingira ya kuwapatia tenda watu wao wa karibu na pengine wasiokidhi vigezo vya kupewa tenda hizo.


Matokeo yake watu hao huishia kununua vitabu pungufu na pengine kununua vitabu ambavyo haviendani na muda au mahitaji husika.


Mmiliki wa maktaba ya uuzaji wa vitabu ya Salamanda Clarence Mponda anasema kuwa awali wakati zabuni zikitolewa na Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Ufundi mfumo wa upatikanaji wa zabuni ulikuwa upo wazi na wa kuridhisha.

bnm.jpgAnasema kuwa ilikuwa ni rahisi kwa wazabuni wadogo pia kupata nafasi za kusambaza vitabu kwa kuwa walikuwa wakishindana.
Anasema kuwa kwa sasa suala la manunuzi ya vitabu lipo chini ya Tamisemi na kuongeza kuwa walimu wakuu wanakuwa na nguvu zaidi katika kununua vitavbu hivyo.

Anasema kuwa hali hiyo inaleta utata kwa kuwa mfumo wa upatikanaji wa zabuni sio wa wazi tena na inawawia vigumu wao kama wanunuzi wa vitabu kupata tenda za kununua vitabu hivyo.

“ Ni kwamba yani kwa sasa huu utaratibu ni kama vile sio mzuri kwa kuwa zamani ilikuwa rahisi mno sisi tulikuwa tunaenda moja kwa moja kugombania tenda katika Halmashauri za wilayani na mambo yalikuwa yanaenda vema sana” alisema Mponda.

Hata hivyo ofisa elimu wa wilaya ya Kinondoni Lucy Gurtu anapingana na hoja hiyo kwa kufafanua kuwa kwa kawaida walimu wakuu hawana idhini ya kununua vitabu moja kwa moja.

Anasema kuwa fedha za ruzuku za vitabu zinapotoka Tamisemi hufika kwanza katika ofisi ya wilaya na kisha kupangiwa matumizi kulingana na mahitaji ya shule husika.

Anasema kuwa kupitia wakaguzi wa elimu wa wilaya ofisi yake hugundua shule yenye uhaba wa vitabu na kuchanganua ni vitabu vya aina gani vinahitajika kwa muda huo.

Anasema kuwa pia walimu wenyewe hupeleka maombi kwa ofisa elimu wa wilaya kuelezea mahitaji halisi ya vitabu vinavyotakiwa.

Anasema kuwa kutokana na hilo kunakuwa hakuna mianya ya rushwa kwa kuwa walimu wakuu wanajengea hoja ya hitaji husika na kuliombea fedha.

Anasema kuwa wakuu wa shule huandika idadi ya vitabu inavyohitaji kwa kuchanganua ni vya aina gani na pia hata kama wakihitaji vifaa vya mahabara pia hutoa mapendekezo ya aina ya vifaa.

Anasema kuwa baada ya kutoa mchanganuo ofisi yake huwapatia fedha za kununulia vitabu husika na hivyo walimu hununua vitabu kulingana na mahitaji waliyohidhinisha.

Anasema kuwa iwapo walimu ikibainika kuwa hawakununua vitabu kulingana na makubaliano husika wakaguzi wa elimu wanalo jukumu la kuwachukulia hatua.


Anasema kuwa wakaguzi wa elimu kwa kushirikiana na wakaguzi wa ndani wa Manispaa huendesha zoezi la ukaguzi na kutoa ripoti kuhusiana na manunuzi ya vitabu husika.

“ Ni kwamba najua yani kunakuwa na changamoto mbalimbali ambazo kwa pamoja inatakiwa kushirikiana katika kuzitatua, mfano suala la kuwa na wakaguzi wa kutosha wa kukimbia huku na huko kukagua masuala muhimu ya elimu katika wilaya na mengineo” anasema Lucy.


Kutokana na hakli hiyo ya wakuu wa mikoa kupewa fedha za kununulia vitabu kulingana na mahitaji yao huenda ndilo linalopelekea mazingira ya rushwa katika kutoa zabuni hizo.


Naibu Katibu Mkuu wa ofisi ya waziri mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Jumanne Sajni anafafanua zaidi kuwa ofisi yake hupeleka fedha kwa ofisi za elimu za wilaya ambazo ndio huwa na jukumu la kununua vitabu.

hil.jpgAnasema kuwa walimu huwa na jukumu la kuidhinisha aina ya vitabu vya kununuliwa na kisha kupelekea maombi sehemu husika na pia ufuatiliaji wake hufanyika kiundani ili kuhakikisha kuwa vitabu vimenunuliwa.

“ Mimi ninchoweza kusema kuwa kama kuna walimu ambao wanachakachua ununuzi wa vitabu basi ni jukumu la kamati ya shule kuhakikisha kuwa linashughulikia suala hilo” alisema Sajni.

Alisema kuwa Mkuu wa shule husika anajadiliana na kamati ya shule katika kuamua aina ya vitabu vya kununua na
kisha kuanza kwa pamoja mchakato wa kununua vitabu hivyo.

Lakini hata hivyo alikiri kuwa huenda kukawepo kwa dalili za mazingira hayo ya rushwa na hivyo alitoa wito kwa maofisa wa elimu wa wilaya kushirikiana na maofisa ugavi na wakaguzi wa elimu kufuatilia manunuzi ya vitabu.
Mwisho

0 comments:

Post a Comment