Help Children
Love them
Saidia Watoto

Sunday, November 10, 2013

Mwalimu Mkuu matatani kwa ubadhilifu

Mwalimu Mkuu Shule ya Mirerani alalamikiwa kwa ubadhirifu 
MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Mirerani, Wilaya ya Simanjiro mkoani
Manyara,  Magreth Galibona analalamikiwa kufuja fedha na kudaiwa kuendesha shule hiyo namna anavyotaka.

Anadaiwa kuchangisha wanafunzi wa darasa la saba fedha kwa ajili ya picha kwa miaka miwili mfululizo pasipo halali.

Hata hivyo mwalimu huyo, amejibu shutuma hizo akisema wazazi walikubali kupitia kikao halali cha mkutano wa wazazi na walezi kulipa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya maendeleo ya shule yao hivyo hakuna tatizo juu ya hayo.

“Mimi nafanya kazi yangu siangalii majungu ya walimu wanavyosema hivyo endapo kuna watu wanaendelea na majungu yao watajua wenyewe ila mimi naendelea kufanya kazi yangu wasubiri wanachotaka,” alisema Mwalimu Galibona.  

Baadhi ya waliozungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa, walidai wanafunzi zaidi ya 150 waliamriwa kulipa Sh  2,100 kila mmoja kwa mwaka jana ili wapige picha za kufanyia mtihani ili hali halmashauri ya wilaya hiyo ilishagharimia picha hizo.

Walidai Mwalimu Galibona aliwachangisha wanafunzi 1,300 Sh 1,000 kila mmoja kwa ajili ya kutengeneza sanduku la kuhifadhi mitihani wakati fedha za ruzuku zilitengwa kwa ajili ya kazi hizo.
Kwa mujibu wao, akisikia wakaguzi wanakuja kukagua shule hiyo mwalimu huyo huwa na mtindo wa kunakilisha wanafunzi wa darasa la tatu ubaoni kwa siku moja kwa tarehe tofauti na kuwaandikia majibu ubaoni ili waonekane wana akili.
“Pia anakumbatia madaraka kwani yeye ndiye mwalimu mkuu na mtunza vifaa, fedha na chakula na ukimpinga tu anaongea na wilaya unahamishwa,” alisema mmoja wa waliozungumza na gazeti hili na kutaja baadhi ya walimu waliodaiwa kuhamishwa.

Ofisa Elimu Msingi wilayani Simanjiro Silvanus Tairo alizungumza na mwandishi wa habari hizi alisema atafuatilia malalamiko yote yaliyotolewa  yapatiwe ufumbuzi kwa manufaa ya kunyanyua elimu katika wilaya hiyo.
Tairo alisema ni mgeni kwenye wilaya hiyo ila atafuatilia suala la wazazi kuchangishwa fedha za mitihani kwani Serikali ilishalipa gharama za huduma za picha na sanduku la mitihani.

0 comments:

Post a Comment