Help Children
Love them
Saidia Watoto

Friday, November 1, 2013

Daraja 0 sasa limekuwa daraja la 5, hizi ni siasa au ndo mabadiliko makubwa sasa


WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imefanya mabadiliko ya mitihani ya elimu ya sekondari katika eneo la upangaji wa viwango vya alama ikiwa ni pamoja na kufuta daraja la sifuri na daraja hilo sasa kuwa daraja la tano ambalo litakuwa la mwisho katika ufaulu.

Pia wizara hiyo, katika mabadiliko hayo yatakayoanza kutekelezwa rasmi kwa mtihani wa kidato cha nne unaotarajiwa kuanza Novemba 4 hadi 21, mwaka huu, mfumo wa tathmini endelevu (CA) nao utaanza kutumika kwa ajili ya kuamua kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi husika.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Sifuni Mchome, alisema kuanzia mwaka huu kidato cha nne na cha sita mitihani yao itatumia alama za A, B, C, D, E na F ambapo muachano wa alama kati ya kundi moja hadi jingine utafanana.

Aidha alisema katika alama hizo, ni alama ya B pekee ndio itakuwa na nyongeza ya chanya na hivyo kuwa na alama za B+ na B na kufuta alama hizo zilizokuwa kwenye mfumo unaotumika sasa kwa alama ya A na hivyo alama hiyo itajitegemea.

“Katika alama hii ya B kundi la kwanza la B litakuwa na la wanafunzi waliopata alama kuanzia 50 hadi 59 na lingine la B+ litakuwa la wale waliovuka uwigo wa 50 hadi 59 na kufikia uwigo wa 60 hadi 74,” alisisitiza Mchome.

Alisema pamoja na kuwa na muachano wa alama 26 alama A kwa miaka mingi imekuwa ikianzia alama ya 75 hadi 100 ambapo pamoja na uwigo huo wanaofaulu kwa kiwango hicho ni wachache na hivyo, Serikali imeona hakuna haja ya kubadili alama hiyo.

Alisema katika mabadiliko hayo, alama F itaendelea kuwepo na itakuwa ya ufaulu wa chini kabisa, itaanzia alama 0 hadi 19 na E ambayo ni alama ya ufaulu hafifu itaanzia alama 20 hadi 29 na D ambayo ni ufaulu wa wastani itaanzia 30 hadi 39.

Alama nyingine ambazo ni C yenye maana ya ufaulu mzuri itaanzia 40 hadi 49, B ambayo ni ufaulu mzuri sana itaanzia alama ya 50 hadi 59, B+ ambayo ni ufaulu bora sana itaanzia alama 60 hadi 69 wakati A ambaye itakuwa ni ufaulu wa uliojipambanua itaanzia 70 hadi 100.

“Katika mabadiliko haya C itakuwa ndio alama ya ufaulu mzuri usiohitaji urekebu wa lazima wakati D na E ni alama ambazo zinahitaji urekebu kadri mwanafunzi atakavyoendelea na masomo ili kuthibitisha kama mlengwa anaweza kulingana na mahitaji ya eneo husika,” alisema.

Aidha alisema alama F ni alama ambayo inahitaji urekebu wa hali ya juu ili mwanafunzi aweze kumudu masomo kadri anavyoendelea kukua kielimu au atakapoingia katika ulimwengu wa kazi.

Profesa Mchome, alisema katika mabadiliko hayo, wizara hiyo imeamua makundi hayo mapya ya alama yatajumuisha mfumo wa CA kwa kiwango cha asilimia isiyozidi 40, na mtihani wa mwisho kwa asilimia isiyozidi 60 kwa makundi yote ya watahiniwa ikiwemo wa kujitegemea.

Alisema mfumo huo wa CA umepangwa kwa kidato cha nne utokane na mtihani wa kidato cha pili alama 15, matokeo ya kidato cha tatu alama tano kwa kila muhula na hivyo jumla alama 10, mtihani wa Mock alama 10 na kazi za mradi alama tano wakati kwa kidato cha sita CA itaendelea kama muundo wa sasa ulivyo.

Pia alisema mfumo huo wa CA utatumika hadi kwa wanafunzi wa kujitegemea ambapo zitatokana na matokeo ya mitihani ya wanafunzi hao ya awali.

Akizungumzia muundo wa wastani wa alama katika ufaulu (GPA), alisema mchakato wa kuanza kutumia mfumo huo unaendelea ambapo watalaamu wa mifumo ya mitihani wanalifanyia kazi, utakapokamilika kabla ya kutumika wananchi wataelimishwa kwanza.

Alisema kupitia mfumo huo wa GPA, mfumo wa sasa wa ufaulu hautokuwa na daraja la sifuri na badala yake, mfumo wa ufaulu utaanzia daraja la kwanza hadi la tano ambalo ndio la mwisho kwa ufaulu.

Katika mabadiliko hayo, Profesa Mchome, aliwatahadharisha wadau wote wa elimu kuhakikisha kuwa wanafuata taratibu zote kwa mujibu wa sheria na kanuni na kutotumia vibaya mabadiliko hayo kwa maslahi yao kwani hatua kali zitachukuliwa dhidi yao watakapobainika.

Wakati huo huo, Jumla ya watahiniwa 427,906 ambao kati yao 367,399 ni watahiniwa wa shule na 60,507 ni watahiniwa wa kujitegemea wanatarajiwa kufanya mtihani wa kidato cha nne utakaoanza rasmi Novemba 4 hadi 21, mwaka huu.

Mchome alisema idadi hiyo ya watahiniwa ni pungufu ya watahiniwa 53,508 sawa na asilimia 11.1 ikilinganishwa na watahiniwa 481,414 walioandikishwa kufanya mtihani huo mwaka jana.

Mwisho

0 comments:

Post a Comment