Help Children
Love them
Saidia Watoto

Monday, September 9, 2013

Mtihani wa darasa la pili umeanzishwa, nini maoni yako



Na Mwandishi Wetu
MTIHANI mpya wa Taifa, utaanzishwa kwa wanafunzi wa darasa la pili nchi nzima, ili kuchuja watakaoshindwa kusoma, kuandika na kuhesabu.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema hayo jana alipokuwa akitangaza kuanza kwa Mtihani wa wa Taifa wa Kumaliza Elimu ya Msingi Tanzania Bara.

Mtihani huo wa kumaliza elimu ya msingi, unatarajiwa kufanyika kesho na keshokutwa na kuhusisha watahiniwa 868,030 waliosajiliwa.

*Darasa la Pili
Akifafanua uamuzi wa kuanzishwa Mtihani wa Taifa wa Darasa la Pili, Mulugo alisema mtihani huo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Matokeo Makubwa Sasa katika sekta ya elimu.

Malengo ya mtihani huo kwa mujibu wa Mulugo ni kuondoa uwezekano wa kuwa na wanafunzi katika madarasa ya juu, wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu na ili kufikia malengo hayo, watakaoshindwa mtihani huo, watarudia mpaka wajue kusoma na kuandika.

Mwaka jana Aprili, Mulugo alipokuwa akizungumza na   wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), alikaririwa akikiri kuwa katika mtihani wa Taifa wa Kumaliza Elimu ya Msingi  wa mwaka juzi, kulikuwa na wanafunzi wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu, waliochaguliwa kujiunga na elimu ya Sekondari.

Kutokana na udanganyifu katika mitihani ya taifa, Mulugo alikaririwa akiagiza wanafunzi wote walioingia kidato cha kwanza wapimwe kwanza uwezo wao wa kusoma na kuandika na kuhesabu.

Alikaririwa akisema tathmini Mkoa wa Kilimanjaro uliongoza kwa kuwa na wanafunzi wengi wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu.

"Mkoa wa Kilimanjaro una wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika wapatao 660, Tanga 490 na Dar es Salaam 208," alikaririwa Mulugo bila kutaja matokeo ya mikoa mengine.

“Hili ndilo janga la kitaifa sasa. Siyo hayo mengine ambayo watu wanasema ni majanga ya kitaifa. Lazima tujiulize kwa nini watoto wanamaliza darasa la saba wakiwa hawajui kusoma wala kuandika na halafu wanafaulu?” Alihoji kuongeza:

“Je, siku hizi hakuna tena somo la kusoma na kuandika? Kwa nini mtoto amalize shule bila kuwa na maarifa ya KKK (Kusoma, kuandika na kuhesabu)?  

“Jambo la kusikitisha kuna mpaka baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tatu, ambao hawajui kusoma wala kuandika. Tulipofikia siyo pazuri hata kidogo, lazima tuwe makini jamani.

“Tuheshimu Baraza la Taifa Mitihani (Necta), tupate ufumbuzi wa mambo haya taifa hili ni letu sote, lazima tuhakikishe linasimama imara,” alikaririwa Mulugo.

*Darasa la saba
Akitangaza kuanza kwa mtihani wa darasa la saba kesho, Mulugo alisema kati ya watahiniwa wote,  wasichana ni wengi ambao ni 455,925 sawa na asilimia 52.52 ya watahiniwa wote na wavulana ni  412,105 sawa na asilimia 47.47.

Masomo yatakayotahiniwa ni Kiswahili, Kiingereza, Sayansi, Hisabati na Maarifa ya Jamii.
Alisema wanafunzi 844,810 wanatarajiwa kufanya mtihani  huokwa lugha ya Kiswahili, kati yao wavulana ni 400,335 na wasichana 444,475.

Wanafunzi 22,535, kati yao wavulana wakiwa 11,430 na wasichana 11,105, wanatarajiwa kufanya mtihani huo kwa lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo walikuwa wakiitumia kujifunzia.

Wanafunzi wasioona waliosajiliwa kufanya mtihani huo ni 88 wakiwemo wavulana 56 na wasichana 32 ambapo pia watahaniwa 597 wenye uoni hafifu ambao huhitaji maandishi makubwa wanatarajiwa kufanya mtihani huo.

Mulugo alisema maandalizi yote kwa ajili ya mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa karatasi za mitihani, kusambazwa kwa fomu maalum za OMR za kujibia mtihani na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo.

Alitoa mwito kwa maofisa elimu wote wa mikoa na halmashauri kuhakikisha utaratibu wote za mitihani unazingatiwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mazingira yanakuwa salama na tulivu pamoja na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha udanganyifu.

Pia alitoa wito kwa wasimamizi wote kufanya kazi yao  kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu kwa kuwa wapo baadhi ya wasimamizi wamekuwa wakishiriki kuwasaidia watahiniwa kufanya udanganyifu kwenye mitihani yao, na kuonya atakaebainika atachukuliwa hatua kali za kushetria.

 Wanafunzi watakaojihusisha na vitendo vyovyote vya udanganyifu wa mtihani, aliwaonya kuwa atawafutia matokeo yao na kuitaka jamii kutoa ushirikiano unaotakiwa katika kuhakikisha mtihani huo  unafanyika kwa amani na utulivu wa kutosha bila usumbufu wa shughuli za kijamii hasa katika maeneo ya jirani na shule.
Mwisho

0 comments:

Post a Comment