Help Children
Love them
Saidia Watoto

Monday, December 12, 2016

Wanawake wajasiriamali 29 nchini wapewa mafunzo na Taasis ya Graca Machel

Mmiliki wa shule ya chekechea na msingi ya Barney, Marina Juma akifurahi baada ya kupewa cheti cha kuhitimu mafunzo ya miezi 10 ya kuwajengea uwezo wa wanawake wa kujiendeleza kiuchumi yaliyoratibiwa na Mfuko wa Graca Machel, kulia ni Meneja mradi wa mfuko huo  Korkor Cudjoe na katikati ni Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wanawake nchini, Jacqueline Maleko (Picha na Mpigapicha Wetu)
Na Mwandishi Wetu
WANAWAKE 29, wajasiriamali katika nyanja tofauti tofauti wamehitimu mafunzo ya miezi 10 ya ujasiriamali yaliyoandaliwa na Taasis ya Graca Machel.

 Mafunzo hayo yamehusisha wanawake wajasiriamali kuanzia ngazi ya chini ya kati na wajasiriamali wakubwa.

Akizungumzia kuhusiana na mafunzo hayo, mratibu wa mafunzo hayo, Vida Mndolwa alisema, wajasiriamali hao walikuwa wakisoma kila Alhamis ya mwisho wa mwezi na kuwa wapo wanafunzi ambao waliishia njiani kutokana na sababu mbalimbali.

Alisema kuwa kwa kipindi hicho chote wamefundishwa masuala mbalimbali yahusuyo biashara na kuwa washiriki walikuwa na nafasi ya kujifunza zaidi kwa vitendo pia.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika ufungwaji wa mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wanawake nchini (TWCC) Jacqueline Maleko, aliwataka wanawake hao kuwekeza zaidi kwenye mafunzo kama hayo.
Pia aliwataka wanawake kujenga utamaduni wa kufuatilia taarifa kuhusiana na masuala ya fursa za kibiashara ili kuzitumia katika kupanua wigo wa shughuli zao.

Jacqueline alisema kuwa wanawake wengi nchini wanashindwa kusonga mbele kibiashara kwa kuwa wanakosa taarifa ambazo zingetumiwa kuwawezesha kusonga mbele kibiashara.


Alisema kuwa ili kukabiliana na hali hiyo ni wakati mwafaka kwa wanawake kwenda kwenye vituo mbalimbali vya kiuchumi au wizara na kuomba kupewa taarifa kuhusiana na miradi ya kusaidia wanawake.

Alisema kuwa ipo miradi 19 ya kuwaendeleza wanawake na vijana kwa ujumla kiuchumi na kuwa kwa sasa hakuna uwazi wa kutosha kuhusiana na miradi hiyo.

"Ni wakati sasa kwa wanawake nchini kutafuta taarifa zitakazoinua biashara na hii ni hasa katika kupata habari za fursa za kibiashara, waende Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi kiuchumi kuna mengi yanayohusiana na miradi ya maendeleo yanayoweza kuwasaidia wwao kama wanawake" alisema Jacqueline.

0 comments:

Post a Comment