Help Children
Love them
Saidia Watoto

Friday, March 14, 2014

Serikali kutoa msimamo wake kuhusiana na suala la ada

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI iko katika mchakato wa kuja na bei elekezi ya ada kwa wajili ya shule za msingi na sekondari hapa nchini.

Hatua hiyo ya serikali imetokana na kukamilisha mfumo wa gharama halisi ya ada kwa mwanafunzi kwa elimu ya juu katika vyuo vikuu hapa nchini ambao utaanza kutumika mwaka ujao wa fedha.


Akizungumza jana wakati wa uzinduzi, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema mfumo huo utasaidia wanafunzi, wazazi na wafadhili kujua ada halisi kwa kozi husika


Alisema pia mfumo huo utasaidia kuongeza ufanisi wa utoaji mikopo kwa wanaufunzi unaofanywa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.


 “Kuzinduliwa kwa mfumo wa gharama halisi ya mafunzo ya elimu ya juu, litatufanya mimi na (Profesa Sifuni) Mchome kulala usingizi, kwa sasa tuko kwenye mchakato wa kuja na mfumo kwa ajili ya shule za msingi na serkondari,” alisema.


Mfumo wa gharama halisi ya masomo kwa mwanafunzi, unajumuisha gharama zote za kuendesha kozi husika kwa mwaka, ikiwa ni gharama za mishahara ya wafanyakazi wote wa vyuo, ghara za kozi na huduma nyingine.


Tathimini ya Habarileo imebaini kuwa kuanza kutumika kwa mfumo huo, kuna baadhi ya gharama kwenye vyuo ikapungua au kuongezeka kidogo kulingana na aina ya chuo, gharama za uendeshaji na idadi ya wanafunzi.


Pia gharama ya kozi ya aina moja inaweza kutofautina chuo cha umma na binafsi, kutokana na baadhi ya gharama katika vyuo vya umma kubebwa na serikali.


Aidha, Kawambwa alisema kutokana na mchakato huo kuwa na wigo mpana wa ushirikishwaji wa wadau, hivyo ni imani yake kuwa utatekelezwa kikamilifu na wadau hao.


“ Ni imani yangu kuwa mfumo utatumika kama mwongozo kwa serikali na taasisi za elimu ya juu nchini katika kubuni na kuamua gharama za kuendesha programu na kuweka ada moja.


“ Hii itapunguza au kuondoa kabisa malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusiana na gharama za elimu ya juu hapa nchini.”
Aidha, Kawambwa alisema Serikali inaelewa changamoto za kifedha zinazokabili taasisi za elimu ya juu na kuzitaka taasisi hizo kutafuta vyanzo vingine vya fedha badala ya kutegemea serikali na ada.


Kawambwa pia alizitaka taasisi za elimu ya juu, kuwa makini katika matumizi nafuu katika shughuli za kila siku ikiwa ni pamoja na kutumia rasilimali kwa mambo ambayo yanaleta faida na kuwa na utawala mzuri wa fedha.


Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Profesa Magishi Mgasa, alisema mfumo huo ambao mchakato umefanywa na wataalamu wazawa umepitia hatua mbalimbali na kushirikisha wadau wa elimu ya juu katika kila kozi.


“ Baada ya kukamilika kwa mfumo huu, ni lazima taasisi za elimu ya juu zikapitia upya suala zima la ada katika kozi husika,” alisema.


Alisema kwa sasa TCU ina kazi ya kutoa elimu kwa taasisi za elimu ya juu ili waweze kutumia mfumo huo kikamilifu katika taasisi zao na kupitia upya ada katika mwaka ujao wa fedha.


Aidha, Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini Dar es Salaam, Profesa Uswege Minga, alisema kuanzishwa kwa mfumo huo kunaziondoa kwenye giza taasisi za elimu ya juu husani zile za binafsi kutokana na kuwapo kwa malalamiko ya kuonekana kutoza ada kubwa.


“ Ninamini katika kupitia mchakato huu mmezingatia utoaji wa elimu bora,” alisema.
(mwisho).
 

0 comments:

Post a Comment