SERIKALI imewataka wamiliki na wakuu wa vyuo vya elimu kuhakikisha wanasimamia ipasavyo mitihani inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni ili ifanyike kwa uaminifu na kuepusha udanganyifu ambao umekuwa ukiviharibia vyuo vingi sifa.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam, Theresia Mmbando aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika mahafali ya tano ya wahitimu 243 wa chuo cha ualimu cha Ebonite kilichopo Kimara katika mkoa huo.
Alisema kumekuwepo na udanganyifu ambao hufanywa na baadhi ya vyuo kwa malengo ya kuwasaidia wanafunzi wao lakini hali hiyo imekuwa ikiwaletea sifa mbaya baada ya kubainika na kukitaka chuo hicho kulinda sifa yake kwa kuzingatia uaminifu.
Aidha Mmbando aliwataka wahitimu kuzingatia maadili kazini kwa kuwa kwa sasa kumekuwepo na malalamiko mengi ya kuwepo kwa waalimu wasiozingatia maadili.
Pia alisema kuwa serikali ya mkoa huo ipo tayari kushirikiana na chuo hicho ili kuhakikisha kinafikia malengo yaliyokusudiwa ikiwemo kutoa elimu bora.
Mapema akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake, Hussein Mrisho alisema changamoto kubwa inayowakabili wanafunzi hao ni pamoja na ukosefu wa viwanja vya michezo na uhaba wa vifaa vya kufundishiwa.
Kwa upande wake mkuu wa Chuo hicho, Aziel Elinipenda alisema kuwa pamoja na mafanikio yaliyofikiwa tangu chuo hicho kilipoanzishwa 2007 lakini pia wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa viitabu vya ziada na kiada.
Alizitaja changamoto nyingine kuwa ni ukosefu wa shule ya mazoezi kwa ajili ya mazoezi ya wanafunzi wa chuo hichio na ukosefu wa majengo ya utawala.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment