Wanafunzi wakifutalia kuhitimu mafunzo yao |
WAHITIMU wa kidato cha nne mwaka jana huenda wakajikuta katika hali tofauti za ama furaha au huzuni kutokana na uamuzi wa Serikali wa kufuta matokeo ya mitihani yao na kuandaliwa upya kwa utaratibu uliotumika mwaka juzi.
Kwa kuwa imeshaamuliwa hivyo, na Baraza la Mawaziri kubariki kutokana na matokeo ya Tume ya Uchunguzi wa Matokeo hayo, ni upo uwezekano wa baadhi ya walioshindwa kupata ahueni na kufurahi na waliofaulu kujikuta wakishuka na kuhuzunika.
Hiyo inatokana na uamuzi wa kutaka kusanifisha matokeo ya wanafunzi hao ili yalingane na juhudi walizoziweka katika kusoma kwa mazingira na hali halisi ya Tanzania, na uamuzi wa Taifa kuongeza shule na wanafunzi wakati uwekezaji katika ubora ukiendelea.
Hatua hiyo inasitisha utaratibu mpya wa kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya matokeo ya mitihani uliotumika mwaka 2012 na badala yake, Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) litumie utaratibu wa mwaka juzi kwa vidato vya nne na sita ukiwamo wa usanifishaji na kutoa matokeo mapya.
Akiwasilisha Kauli ya Serikali bungeni mjini hapa jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, alisema baada ya uchunguzi kufanywa kwa kuzingatia hadidu za rejea, Tume hiyo iliwasilisha mapendekezo ambayo yanatakiwa kufanyiwa kazi. Waziri Lukuvi alisema kuridhia kwa mapendekezo hayo kumelenga kutenda haki kwa walimu na wanafunzi ambao juhudi zao za kufundisha na kujifunza, zimepimwa kwa kutumia mfumo mpya ambao hawakupata fursa ya kushirikishwa na kuuandaa.
Hadidu za Rejea Tume ilipewa Hadidu za Rejea za kubainisha sababu za matokeo mabaya; kushuka kwa kiwango cha ufaulu; kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua ili kukabiliana na tatizo la mwenendo wa kushuka kwa kiwango cha elimu mara moja, kipindi cha muda mfupi, kati na cha muda mrefu.
Pia ilitakiwa kutathmini nafasi ya halmashauri katika kusimamia elimu ya sekondari katika halmashauri zake; kuainisha sababu nyingine zinazoweza kuwa zimechangia hali hiyo ya matokeo.
Na katika kutafakari, Tume ilijikita kujibu maswali ya kwa nini matokeo ya tangu mwaka 2008 yamekuwa na mserereko wa kushuka kuliko miaka iliyotangulia; sababu za wanafunzi wa kidato cha nne mwaka jana matokeo yao kuwa mabaya kuliko mwaka juzi na kushuka kwa ufaulu tangu mwaka 2008 na hatimaye kupendekeza nini kifanyike.
Matokeo ya mwaka jana yalionesha kuwa kiwango cha ufaulu kimeshuka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka ya hivi karibuni. “Matokeo yaliyotangazwa Februari 2012 yalionesha kwamba kati ya wanafunzi 367,756 waliofanya mtihani huo, 126,847 walifaulu. Katika idadi hii, waliofaulu katika daraja la kwanza hadi la tatu ni 23,520, (6.4%) na daraja la nne 103,327(28.1%). Watahiniwa 240,909 (65.5%) ya waliofanya mtihani huo walipata daraja sifuri,” alisema Lukuvi.
Waziri Lukuvi alifafanua, kwamba kushuka kwa kiwango cha ufaulu kilihusu shule za aina zote, yaani sekondari za serikali ikijumuisha zilizojengwa kwa nguvu za wananchi, shule binafsi na seminari. “Takwimu zinaonesha, kwamba ukilinganisha matokeo ya kidato cha nne mwaka 2011 na mwaka 2012, shule za wananchi matokeo yao yameshuka kwa asilimia 1.82; shule za umma za zamani kwa asilimia 6.43; shule binafsi kwa asilimia 6.39; na seminari kwa asilimia 7.29,” alisema Lukuvi.
Aidha, aliongeza kuwa hali hiyo inaonesha, kwamba matokeo katika shule za wananchi, yameshuka kwa kiwango kidogo ikilinganishwa na shule za umma za zamani, shule za binafsi na za seminari ambazo zilitazamiwa kufanya vizuri zaidi ya za wananchi, matokeo yao yameshuka zaidi kwa kati ya asilimia 6.4 na 7.3.
Changamoto Katika uchunguzi wake, Tume ilibaini kuwapo changamoto zilizotokana na mafanikio ya kuongezeka sana kwa idadi ya shule za msingi na sekondari hususan mwaka 2001 na sasa na hivyo kuwapo idadi kubwa ya wanafunzi shuleni.
“Kwa mfano, katika kipindi cha mwaka 1961 hadi 2001 idadi ya wanafunzi wa shule za msingi iliongezeka kutoka 486,470 (1961) hadi 4,875,764 mwaka 2001, sawa na ongezeko la wanafunzi 4,389,294 katika kipindi hicho cha takriban miaka 40.
“Hata hivyo, kati ya mwaka 2001 na 2012 wanafunzi waliongezeka kutoka 4,875,764 mwaka 2001 hadi 8,247,472 mwaka 2012, sawa na ongezeko la wanafunzi 3,371,708 katika kipindi cha takriban miaka 11 na hivyo kufanya jumla ya wanafunzi wote wa shule za msingi kuwa 8,247,472 mwaka 2012,” alisema Waziri Lukuvi.
Kuhusu sekondari, alisema idadi ya wanafunzi iliongezeka kutoka 11,832 mwaka 1961 hadi 289,699 mwaka 2001 sawa na ongezeko la wanafunzi 274,867 katika kipindi cha miaka 40. Lakini kati ya mwaka 2001 na 2012, idadi iliongezeka kutoka 289,699 (2001) hadi 1,884,270 mwaka 2012, sawa na ongezeko la wanafunzi 1,594,571 katika kipindi cha miaka 11.
“Juhudi hizi zilitokana na mipango iliyoandaliwa chini ya Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu mwaka 1999, ambayo ni pamoja na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) wa mwaka 2002 ambapo MMEM I ililenga kufungua shule zaidi ili wanafunzi wengi wa rika lengwa waweze kujiunga na elimu ya msingi.
“MMEM II ililenga kuboresha ubora wa elimu itolewayo katika shule za msingi; na MMEM III ililenga kuendelea kuimarisha ubora wa elimu ya msingi baada ya mafanikio ya MMEM I na MMEM II,” alisema.
Akizungumzia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) wa mwaka 2004 alisema MMES I alisema ililenga kufungua shule zaidi za sekondari katika ngazi ya kata ili wanafunzi wengi zaidi wanaomaliza elimu ya msingi wajiunge na sekondari huku MMES II ikilenga kuendelea kuimarisha ubora wa elimu ya sekondari kadri idadi ya wanafunzi wa sekondari wanavyoendelea kuongezeka.
Alitaja changamoto zinazoambatana na mafanikio hayo kuwa ni pamoja na mazingira yasiyoridhisha ya kufundishia na kujifunzia, ukiwamo upungufu wa miundombinu muhimu ya shule kama vile madarasa, maabara, madawati, maktaba, nyumba za walimu, hosteli na majengo mengine muhimu ya shule. “Vile vile, kuna tatizo la uhaba wa walimu, vitabu, zana za kufundishia na matatizo ya ukaguzi wa shule.
Vilevile, Tume imebaini kuwa mfumo wa elimu ya msingi na sekondari unakabiliwa na changamoto nyingine ambazo Taifa linapitia kwa sasa yakiwamo masuala ya kisera, kisheria, kimfumo, kimuundo pamoja na uhaba wa rasilimalifedha na rasilimaliwatu; ambapo Tume inaendelea kufanyia kazi maeneo haya kwa kushirikiana na wataalamu na wadau wengine,” alisema Waziri.
Kufeli Kuhusu kufeli kwa ujumla wake, Tume ilibaini kwamba ufaulu umeshuka zaidi kwa sababu ya mabadiliko ya mchakato wa kuandaa na kutoa matokeo ya mtihani kwa mwaka jana.
Mfumo uliotumika mwaka huo katika kupanga matokeo na madaraja ni tofauti na uliotumika mwaka juzi na miaka iliyotangulia.
Uchunguzi unaonesha kuwa mwaka juzi, Baraza la Taifa la Mitihani lilikuwa linachakata alama za mwisho kwa kutumia mfumo ambao ulikuwa unabadilika kutegemea hali ya ufaulu wa mwanafunzi (NMD).
Utaratibu huu ulitokana na tofauti ya wastani wa kitaifa wa alama za maendeleo kutoka alama za maendeleo endelevu (CA) za watahiniwa wote na wastani wa kitaifa wa ufaulu wa mitihani ya mwisho kwa somo husika.
Kila mtahiniwa aliongezwa NMD iliyokokotolewa katika alama za mtihani wa mwisho, ili kupata alama itakayotumika kupata daraja la ufaulu. Kimsingi, kila somo lilikuwa na NMD yake kulingana na CA zilivyo kwa mwaka husika.
”Lakini mwaka jana Baraza lilitumia mfumo mpya ambao ulikuwa haubadiliki kutegemea hali ya ufaulu wa mwanafunzi, yaani kuwa na viwango maalumu vya kutunuku. Tume imebaini, kwamba pamoja na kwamba mfumo huo uliandaliwa kwa nia nzuri, utaratibu huo mpya haukufanyiwa utafiti na maandalizi ya kutosha kabla ya kutumika,” alisema Waziri.
0 comments:
Post a Comment