Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesitisha kutoa udhamini wa elimu ya juu nje nchi, kwa wanafunzi kutoka Zanzibar, kutokana na gharama kubwa za udhamini.
Waziri wa Elimu ya Mafunzo ya Amali, Ali Juma Shamuhuna, alisema hayo katika Baraza la Wawakilishi, wakati alipokuwa akijibu swali la Mwakilishi wa Wawi, Saleh Nassor Juma (CUF)>
Mwakilishi huyo, alitaka kujuwa kwa nini Serikali inashindwa kuwapatia fedha kwa wakati wanafunzi wanaosoma nje ya nchi.
Shamuhuna alifafanua na kusema, Serikali imeamua kusitisha kusomesha nje wanafunzi wa Zanzibar, kwa sababu gharama za masomo nje ya nchi, ni kubwa wakati bajeti inayopewa wizara kwa gharama za wanafunzi nje ya nchi ni ndogo.
“Serikali imeamuwa kusitisha kugharamia mafunzo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wanaosoma nje ya nchi...kama masomo hayo yanapatikana Tanzania katika vyuo vya ndani, basi watasoma huko,” alisema.
Alitoa mfano wa gharama za masomo ya elimu ya juu kwa mwanafunzi mmoja China, kwamba muda wa miaka sita ni Sh milioni 56.
“Hizo ni fedha nyingi ambazo tunatakiwa kuzitumia kwa wanafunzi wanaosoma masomo yanayopatikana nchini au Tanzania Bara,” alisema Shamuhuna.
Awali alisema Bajeti ya Wizara ya Elimu kwa bodi ya mikopo, imeongezeka na kufikia Sh bilioni 8, kwa mwaka wa fedha 2012-2013.
Alisema bajeti hiyo kwa kiasi kikubwa, inaridhisha tofauti na bajeti ya miaka iliyopita, ambayo ilikuwa Sh bilioni 4, ambazo ni kidogo sana.
“Tunaipongeza Serikali kwa kuzingatia umuhimu wa Bodi ya Elimu ya Mikopo, kuipatia fedha nyingi za kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini,” alisema.
0 comments:
Post a Comment