ASASI ya utafiti ya TWAWEZA imetoa muhtasari wa utafiti wa Suti zaWananchi kuhusu kufeli kwa wanafunzi wa kidato cha nne mwaka jana na kusema, idadi kubwa ya waliohojiwa kuhusu sababu za matokeo mabaya waliitaja Serikali na walimu kuwa ndio chanzo.
Aidha, utafiti huo umeonyesha kuwa wazazi wana jukumu la kuhakikisha watoto wao walio shuleni wanajifunza hata kwa muda wa ziada, ingawa Serikali inajukumu la kuhakikisha wanapata nyenzo za kujifunzia kama vitabu vya kiada, huku walimu nao wakilipwa vizuri kutunza morali yao katika ufundishaji.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano wa utambulisho wa muhtasari huo Dar es Salaam jana, watafiti wa TWAWEZA, walioongozwa na Mtafiti Mkuu, Elvis Mushi walisema, maoni waliyoyakusanya kutoka kwa wananchi waliowahiji kwa njia mbalimbali, hayajajumuisha ya watafiti, bali ni sauti za watu kulingana na walichokizungumza.
Kwa mujibu wa Mushi, asilimia 70 ya wananchi waliohojiwa walisema kuwa Serikali na walimu wanahusika katika kufeli kwa wanafunzi hao na kwamba, ili tatizo hilo lisijirudie, italazimika kutatua matatizo ya walimu ikiwa ni pamoja na kuwalipa mishahara inayoendana na kazi yao, kwa muda unaostahili, pamoja na kuwapatia vitendea kazi.
"Serikali imetajwa zaidi kwa kushindwa kuhakikisha upatikanaji wa vitabu vya kiada kwa ajili ya wanafunzi wa shule za sekondari na wananchi waliohojiwa wameishauri izingatie masuala ya muhimu kama vile ukaguzi wa shule wa mara kwa mara, iongeze idadi ya walimu pamoja na kuhakikisha ubora wa miundombinu mbalimbali shuleni,"alisema.
Wakati akisema hivyo, Mtafiti mwingine, Costantine Manda alieleza kuwa walibaini kwamba wazazi wenye watoto wanaosoma katika shule za sekondari walihusika kuwasaidia kujifunza wakati wa muda wa ziada kwa kukagua madaftari yao na kuwahimiza wafanye majaribio na kazi za ziada walizopewa shuleni.
"Idadi kubwa ya wazazi ilieleza kuwa iliwasaidia watoto wao kujifunza nyumbani huku asilimia 41 ikieleza kuwa haijawahi kushughulika na suala hilo,"Manda alisema.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment