WIZARA
ya Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma imesema katika mwaka ujao wa fedha
2013/2014, imedhamiria kuhakikisha kuwa inashughulikia kikamilifu kero za
watumishi ikiwemo matatizo ya walimu.
Pamoja
na wizara hiyo, Wizara ya Nishati na Madini nayo imebainisha wazi kuwa katika
jitihada za kuondokana na tatizo la umeme, asilimia 90 ya bajeti ijayo itaenda
kwenye miradi ya maendeleo.
Akizungumza Dar es Salaam jana Waziri wa Utumishi wa Umma, Celina Kombani,
alisema katika mchanganuo wa makadirio wa bajeti ya wizara yake vipaumbele
vikuu ni kuimarisha mfumo wa taarifa za wafanyakazi pamoja na mishahara yao.
“Mfumo
huu tayari umeshaanza kufanyakazi na lengo lake hasa ni kuhakikisha
tunaondokana na malimbikizo ya madeni ya mishahara na posho, watumishi na
mishahara hewa lakini pia kuimarisha shughuli zote za kiutumishi nchini,”
alisisitiza Kombani.
Alisema
baada ya mfumo huo ulipoanza mapema mwaka huu ulianza na kuingiza taarifa za
walimu 16,000 wapya waliopatiwa ajira mwaka huu ambao wote walipata mshahara
wao wa kwanza kwa muda muafaka tofauti na ilivyokuwa zamani.
Aidha
alisema pia katika bajeti hiyo inayokadiriwa kuwa ni Sh bilioni 32 kipaumbele
kingine ni kuimarisha maslahi ya watumishi wa umma kwa kuangalia upya mazingira
wanayofanyia kazi, motisha na mazingira magumu kwa kila kada.
Aidha
alisema pia bajeti hiyo imezingatia eneo la kuimarisha tume ya utumishi wa umma
ambayo imeongezewa bajeti (hakuitaja) ili kuweza kukagua vyema utendaji wa watumishi
wa umma nchini.
“Tume
hii pia itaangalia na kuhakikisha inatatua matatizo ya walimu ambayo yamekuwa
kero kubwa kwa muda mrefu nchini, ambapo pia safari hii itaimarisha
sekretarieti ya ajira kwa kuiongezea kiwango cha bajeti,” alisema.
Alisema
pamoja na hayo kwa kuwa wizara hiyo ya utumishi wa umma ni ya muungano, katika
bajeti ya mwaka huu, wametenga fedha kwa ajili ya kujenga ofisi za wizara ya
utumishi wa umma Zanzibar ili kuhakikisha huko nako masuala ya utumishi na
ajira yanafanyiwa kazi vyema.
Kuhusu
kiwango cha fedha ambacho wizara hiyo ilipatiwa katika mwaka wa fedha unaoishia
baada ya miezi miwili ijayo, Kombani alisema wizara yake imepatiwa takribani
asilimia 86 ya bajeti nzima.
Kwa
upande wake Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema
bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha itakuwa ni ya kihistoria kwani
haijawahi kutokea dunia kote kwa nchi kutenga asilimia 90 ya bajeti ya wizara
ya nishati na madini katika eneo la miradi ya maendeleo.
“Jamani
sisi tunachotaka ni kuhakikisha haya matatizo ya umeme nchini tunayamaliza
kabisa, ila tunachowaomba watanzania wawe wavumilivu kwa sababu kwa takribani
miaka 30 sasa hatukuwekeza kwenye sekta ya umeme ndio maana matatizo mengi
yanatakumba,” alisema.
Alisema
katika kuhakikisha matatizo yaliyopo yanafanyiwa kazi, asilimia hiyo 90 ya
bajeti imewekwa kwenye miradi ya maendeleo na asilimia 10 imeenda kwenye
matumizi mengine. “Hakuna nchi yeyote duniani inayotenga katika wizara yake
asilimia 90 nzima ya bajeti iende kwenye miradi ya maendeleo,”
Alisema
pamoja na bajeti hiyo ambayo hakutaja imetengewa kiasi gani katika makadirio ya
mwaka ujao wa fedha, alisema kwa sasa hayuko nchini yuko Norway baadaye ataenda
Ubelgiji na Uholanzi ambako amealikwa ikiwa ni jitihada za Serikali za kutafuta
fedha za miradi ya maendeleo.
Kuhusu
kiasi cha fedha ambacho wizara hiyo imepatiwa katika bajeti inayoishia ya mwaka
2012/2013, Profesa Muhongo bila kutaja kiasi cha fedha walichopata hadi sasa,
alisema bajeti ya wizara hiyo imeenda vizuri na kwamba wao kama wizara hawawezi
kulalamika.
“Sisi
hatuwezi hata kidogo kulalamika hali yetu kiuchumi inafahamika lakini pia bado
mwaka haujaisha bado miezi miwili imebaki na bajeti inaendelea kutolewa,”
alisema.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment