SERIKALI ya Mapinduzi ya
Zanzibar, imesitisha kutoa udhamini wa elimu ya juu nje nchi, kwa wanafunzi
kutoka Zanzibar, kutokana na gharama kubwa za udhamini.
Waziri wa Elimu ya
Mafunzo ya Amali, Ali Juma Shamuhuna, alisema hayo katika Baraza la
Wawakilishi, wakati alipokuwa akijibu swali la Mwakilishi wa Wawi, Saleh Nassor Juma (CUF)>
Mwakilishi huyo, alitaka
kujuwa kwa nini Serikali inashindwa kuwapatia fedha kwa wakati wanafunzi
wanaosoma nje ya nchi.
Shamuhuna alifafanua na
kusema, Serikali imeamua kusitisha kusomesha nje wanafunzi wa Zanzibar, kwa
sababu gharama za masomo nje ya nchi, ni kubwa wakati bajeti inayopewa wizara
kwa gharama za wanafunzi nje ya nchi ni ndogo.
“Serikali imeamuwa
kusitisha kugharamia mafunzo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wanaosoma nje ya
nchi...kama masomo hayo yanapatikana Tanzania katika vyuo vya ndani, basi
watasoma huko,” alisema.
Alitoa mfano wa gharama
za masomo ya elimu ya juu kwa mwanafunzi mmoja China, kwamba muda wa miaka sita
ni Sh milioni 56.
“Hizo ni fedha nyingi
ambazo tunatakiwa kuzitumia kwa wanafunzi wanaosoma masomo yanayopatikana
nchini au Tanzania Bara,” alisema Shamuhuna.
Awali alisema Bajeti ya
Wizara ya Elimu kwa bodi ya mikopo, imeongezeka na kufikia Sh bilioni 8, kwa
mwaka wa fedha 2012-2013.
Alisema bajeti hiyo kwa
kiasi kikubwa, inaridhisha tofauti na bajeti ya miaka iliyopita, ambayo ilikuwa
Sh bilioni 4, ambazo ni kidogo sana.
“Tunaipongeza Serikali
kwa kuzingatia umuhimu wa Bodi ya Elimu ya Mikopo, kuipatia fedha nyingi za
kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini,” alisema.
0 comments:
Post a Comment