WANAFUNZI yatima na waishio kwenye mazingira
magumu 80 wilayani Kyela wamepewa msaada wa sare na vifaa mbalimbali vya shule
vikiwa na thamani ya jumla ya sh milioni nne.
Shirika la The Struggle for Community Support
Alliance(SCSA) lenye makao makuu yake wilayani hapa ndilo lililotoa msaada huo
uliokabidhiwa juzi ikiwa ni siku rasmi ya kuzinduliwa kwa mpango mkakati wa
miaka mitano wa shirika hilo.
Vifaa vingine vilivyotolewa kwa wanafunzi hao
ambao ni wa shule za msingi ni pamoja na daftari na kalamu za wino na risasi
huku pia shule ya awali ya Itunge Education Point ya wilayani hapa pia akipewa
msaada wa vitabu 20,mbao mbili za kuandikia na makasha ya chaki.
Kwa mujibu wa uongozi wa SCSA, wanafunzi
waliopata msaada huo ni kutoka katika kata kumi za wilayani hapa ambazo ni
pamoja na Makwale,Ndobo,Ipinda,Kyela mjini,na Ikana.
Kata nyingine ni Ipande,Ngana,Ikimba,Itope na
Katumba huku kata nyingine zinazosalia zikitarajiwa kunufaika na msaada kama
huo katika awamu nyingine zijazo.
Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo Abraham
Mwanyamaki alisema msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa
shirika wa mwaka 2013/2017 ambapo zaidi ya bilioni mbili zinataraajiwa
kutumika.
Mwanyamaki alisema mpango mkakati huo umejikita
katika progamu nne alizozitaja kuwa ni Huduma za elimu,Huduma za afya
vijijini,uwezeshaji jamii kiuchumi pamoja na uhifadhi wa mazingira.
“Tunaamini kuwa maendeleo ya wanakyela yataletwa
na sisi wenyewe. Ndiyo sababu tumejikita katika kutatua changamoto zilizopo
kwenye utekelezaji wa maendeleo wilayani hapa.Tulikwishatoa msaada wa dawati
100 na sasa tunaendelea”
“Tunapenda kuona wanakyela wananufaika na fursa
zilizopo kwenye maeneo yao.Lakini pia jamii itambue kuwa utekelezaji wa
shughuli za kimaendeleo umekuwa chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira
yetu.Tunataka mambo haya yaende sambamba na utunzaji mazingira” alisema.
Hata hivyo Mwanyamaki alisema utekelezaji wa
mpango mkakati wa SCSA kwa kipindi cha
miaka mitano unakabiliwa na changamoto nyingi zinazohitaji ushiriki wa wadau
mbalimbali kuzitafutia ufumbuzi.
Baadhi ya wanafunzi waliopokea msaada huo, Lucia Alphonce na Marium Benson walishukuru shirika
hilo kwa msaada wa vifaa vya shule wakisema itakuwa chachu ya wao kujituma
katika masomo yao kwakuwa watajiona hawako tofauti na wenzao.
mwisho
0 comments:
Post a Comment