Serikali
yarudi katika
mazungumzo na
walimu
*Yaahidi mishahara bora watumishi wa chini
*Yahoji kuhusu nia njema ya Mukoba wa CWT
*Ni kwa kupotosha ukweli wa mazungumzo
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imerejea katika meza ya mazungumzo na Chama cha Walimu
Tanzania (CWT), pamoja na kutokuwepo kwa mazingira ya nia njema kutoka upande
wawawakilishi wa walimu katika mazungumzo hayo.
Taarifa ya Ikulu iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, ilieleza
kwamba Serikali imefikia hatua hiyo, ili kuonesha utayari na nia njema katika
mazungumzo hayo.
Mbali na utayari, pia
Serikali imetangaza kwamba kutakuwepo na nyongeza nzuri kwenye mishahara, hasa
ya watumishi wa ngazi za chini katika mwaka ujao wa fedha.
Kabla ya hatu hiyo, vyombo vya habari vilimkariri
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba
akisema kwamba
Serikali imekataa kukaa meza moja na CWT, ili kuzungumzia nyongeza ya mishahara
na posho za walimu, pamoja na kwamba chama hicho chenyewe kiko tayari kwa
mazungumzo.
Mukoba pia alikaririwa
akidai kwamba Serikali imepuuza amri ya Mahakama, inayotaka pande hizo mbili
kukaa meza moja kujadili madai ya walimu.
Kutokana na madai
hayo, Mukoba alilitaka Bunge na wazazi, kuingilia kati uamuzi wa Serikali
kukataa kukaa meza moja na CWT.
Nia njema
“Serikali inapenda kuwafahamisha wananchi kuwa, madai haya yote hayana
chembe ya ukweli, na hayana nia njema, maana yanaweza kujenga chuki na
mazingira ya kuzua mgogoro mwingine na Serikali usio na sababu, wala maslahi
kwa walimu wenyewe na Taifa,” imeeleza taarifa hiyo ya Ikulu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Serikali imeeleza
kuwa haijakataa majadiliano na CWT, na wala haijapuuza amri ya Mahakama
inayotaka pande zote mbili kurudi kwenye meza ya majadiliano.
Tofauti na madai ya
Mukoba, taarifa ya Serikali ilieleza kuwa tangu amri ya Mahakama itolewe,
tayari vimefanyika vikao vinne vya Baraza la Majadiliano ya Pamoja katika utumishi
wa walimu.
“Vikao viwili
vilifanyika mwaka jana Septemba 12, na
Desemba 5. Vikao viwili tayari vimefanyika mwaka huu Januari 9-10 na
Machi 22,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo
ilifafanua kwamba kilichochelewesha suala la mishahara na posho kujadiliwa
katika vikao hivyo, si kwamba Serikali haikutaka mjadala huo.
“Sababu hasa ni kuwa
CWT ilikata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu, katika kesi Na. 96/2012, na
Serikali iliwasihi viongozi wa CWT wafute rufaa hiyo, ili kuruhusu majadiliano
ya mishahara na posho, lakini walikataa.
“Kitendo hicho hakioneshi
nia njema upande wao. Nia njema ni sharti muhimu kwenye majadiliano haya. Kwa
upande wake, ili kuonesha utayari na nia njema, Serikali sasa imekubali
majadiliano hayo yaendelee, licha ya CWT kukataa kufuta rufaa yao,” ilieleza
taarifa hiyo.
Serikali imeelezea
sababu ya pili iliyochelewesha majadiliano ya maslahi ya walimu, kuwa ni madai
ambayo awali viongozi wa CWT walikuja nayo kuwa iteuliwe timu maalum ya
kuzungumzia maslahi, badala ya Baraza la Majadiliano ya Pamoja katika utumishi
wa walimu, ambalo ndilo lipo kisheria kwa majadiliano hayo.
Kwa mujibu wa taarifa
hiyo, CWT ilichelewa kurejesha majadiliano kwenye Baraza hilo, mpaka wakati wa
kikao cha Januari 9 hadi 10, mwaka huu.
Uzushi wa Mukoba
Wakati Mukoba
alikaririwa kwamba kikao kilichokataa kuzungumzia mishahara na posho za walimu,
ni kilichofanyika Aprili 2 mwaka huu, chini
ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, Serikali imepinga madai
hayo.
“Si kweli vilevile
kuwa kikao kilichofanyika Ikulu, Aprili 2, mwaka huu chini ya Katibu Mkuu
Kiongozi, Balozi Sefue, ndicho kilikataa
majadiliano kuhusu maslahi ya walimu.
“Kauli hiyo ni
upotoshaji wa makusudi usio na nia njema. Viongozi wa CWT wanajua vema kuwa
Katibu Mkuu Kiongozi, si sehemu ya mfumo wa majadiliano kuhusu maslahi ya
walimu. Hivyo, kikao kinachoongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi, hakiwezi kuwa
mahali pa majadiliano ya mishahara, posho na maslahi ya walimu,” ilieleza
taarifa hiyo.
Ilifafanuliwa kwamba mkutano
huo wa Aprili 2, uliitishwa na Katibu Mkuu Kiongozi kwa maombi rasmi yauongozi
wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), ambao walitaka kujulishwa jinsi
utaratibu wa majadiliano ya mishahara ya wafanyakazi wote utakavyokuwa, kutokana
na kuanzishwa kwa mzunguko mpya wa Bajeti ya Serikali.
Serikali imeeleza
kuwa kikao hicho kisingeweza kugeuka na kuwa kikao cha kujadili mishahara na
posho za walimu, kama alivyokaririwa Mukoba akidai.
“Tunapenda wananchi
na walimu wajue pia kuwa Gratian Mukoba, hakuwepo kwenye hicho kikao cha Aprili
2, 2013. Aidha, kikao hicho kilikuwa cha Tucta, hakikuwa cha CWT,” ilideleza
taarifa hiyo.
*Dhamira ya CWT
Serikali imeelezea
kupata tabu ya kuelewa nia na dhamira ya viongozi wa CWT, kwa kupotosha kwa
makusudi wananchi na walimu kwa mambo yaliyo wazi “Serikali imeonesha nia na
dhamira ya wazi ya kujadiliana na CWT, pamoja na vyama vyote vya wafanyakazi,
kuhusu maslahi ya wafanyakazi.
Vikao vingi vilivyofanyika na vinavyoendelea
kufanyika kwenye mabaraza ya kisekta na Baraza Kuu, ni ishara ya wazi ya nia
njema ya Serikali.
“Tunajiuliza, katika
hali hiyo, juhudi hizi za viongozi wa CWT kuandaa mazingira ya mgogoro wa
Serikali lengo lake ni nini hasa?” Ilihoji taarifa hiyo.
0 comments:
Post a Comment