WAMILIKI wa shule Vyuo na shule binafsi nchini wameomba serikali kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule zake na kupeleka katika shule zao ambazo madarasa yako wazi.
Kutokana na hilo,Rais Kikwete alisema suala hilo lina changamoto zake kutokana na ukweli kwamba gharama katika shule zao ni kubwa hivyo wazazi au serikali hawataweza kumudu.
Hayo yalielezwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete wakati akifungua mkutano mkuu maalum wa Chama cha wamiliki wa shule Vyuo na shule binafsi (TAMONGSCO) uliofanyika mkoani Mbeya .
Alisema amesikiliza kwa makini hoja yao kutaka kushirikiana na Serikali kuondokana na msongamano wa wanafunzi katika baadhi ya shule zake.
“ Natambua kwamba wakati Serikali inahangaika kupunguza msongamano katika shule zake, baadhi ya shule zenu zina madarasa yaliyo wazi na zingependa kuletewa wanafunzi na Serikali,lakini Pamoja na uzuri wake, ukweli kwamba gharama katika shule zenu ni kubwa hivyo wazazi au Serikali hatutaweza kumudu,”alisema
Alisema kuwa elimu ni huduma muhimu na haki kwa mtoto hivyo si vyema kugeuzwa kuwa ni biashara ya kuleta faida kubwa.
Alisema uthamini wa ada kwa vyuo vya elimu ya juu umeishafanyika na mapendekezo ya gharama halisi yameandaliwa huku hatua za kumpata mtaalamu elekezi zimefanyika kwa ajili ya kutathmini gharama za uendeshaji kwa shule za sekondari
“ Ninalo ombi moja kwenu ambalo napenda mlijadili kwenye mkutano wenu, linahusu ada kubwa zinazotozwa na shule au vyuo vyenu,kwani wapo wananchi wengi wanaopenda kunufaika na elimu nzuri mnayoitoa lakini wanashindwa kutokana na ada inayotozwa kuwa kubwa”Alisema
Alifafanua kuwa siyo kwamba anataka ada zao zifanane na za shule za Serikali, lakini baadhi ya shule na vyuo vyao vinalalamikiwa na wananchi kwa kutoza ada kubwa na kwamba hazitabiriki kwani hupandishwa wakati wowote.
Wakati huo huo,Serikali imesema Sera mpya ya Elimu inatarajia kuanza kutumika mwishoni mwa mwaka huu na kwenda Sambamba na kupitia upya mitaala ya elimu ili kwenda sambamba na Sera hiyo mpya.
Rais alisema mchakato wa kutunga sera hiyo mpya ya Elimu baada ya ile ya mwaka 1995, umefikia katika hatua za mwisho na Kinachosubiriwa sasa ni maoni ya Wabunge ili Sera ikamilishwe.
“ Naamini kabla ya mwisho wa mwaka huu Sera itakuwa tayari kutumika,Tunaamini kuwa Sera hiyo mpya italeta mabadiliko katika uendeshaji wa mifumo yetu ya elimu hapa nchini na kutoa majibu kwa maswali mengi mliyoyauliza,”alisema.
Aidha, nafasi ya sekta binafsi katika kuchangia maendeleo ya elimu nchini itafafanuliwa kwa upana na kina zaidi.
Alisema wakati huo huo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania itaanza maandalizi ya kupitia upya mitaala ya elimu nchini ili nayo ilingane na malengo ya Sera Mpya ya Elimu.
Alisema mitaala itakayoenda sambamba na hali ya sasa na mahitaji ya maendeleo nchini na duniani,huku akiwahakikishia kutakuwepo na ushirikishaji wa wadau mbalimbali, wakiwemo wa sekta binafsi katika suala hilo.
Pia alisema uimarishaji wa Idara ya Ukaguzi wa Elimu nchini utapewa kipaumbele cha juu,huku wakitambua liwa hali ilivyo sasa hairidhishi hata kidogo na kwamba zipo changamoto nyingi ambazo lazima zipatiwe ufumbuzi.
“Serikali imeanza na inaendelea kuchukua hatua thabiti za kuimarisha ukaguzi wa shule na vyuo hapa nchini,miongoni mwa mambo yanayofikiriwa kufanywa ni kuibadili Idara ya Ukaguzi kuwa taasisi inayojitegemea na kuiwezesha kwa rasilimali watu, vitendea kazi na fedha,”alisema
Alisema anaaamini kwa njia hiyo wataimarisha utendaji wa kazi ya ukaguzi na matokeo yake yataonekana kwa muda mfupi na kuwakumbusha kuwa Mkaguzi wa kwanza wa shule ni Mkuu wa Shule.
“Yeye ndiye mwenye jukumu la kuhakikisha shule anayoiongoza inafuata miongozo iliyopo na inakidhi viwango vya ubora vilivyowekwa, Naomba jukumu hili mlitekeleze ipasavyo kwa wamiliki kuwa wakaguzi wakuu wa kwanza,”alibainisha
Pia alikubaliana nao kuwa ipo haja ya kupitia upya tozo ya vibali vya kufanya kazi kwa waalimu kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, hususan wa fani ambazo kuna upungufu mkubwa.
Rais alisema kuhusu utekelezaji wa sheria za kodi na gharama za kibali cha mgeni kufanya kazi nchini,Alihaidi kuangalia namna ya kupunguza urasimu katika utoaji wa misamaha ya kodi iliyoruhusiwa kisheria.
“ Tutazielekeza mamlaka zinazohusika yaani Hazina na TRA kuweka mfumo mzuri katika kutekeleza wajibu wake, Ninawaomba na nyie mhakikishe kuwa taarifa zinazotakiwa zinatolewa kwa usahihi”Aliwataka
Aliwaeleza kuwa wakati mwingine usumbufu wanaopata unatokana na hoja ya TRA kujiridhisha kabla ya kutoa misamaha kwani bila hivyo, taasisi zisizostahili zitajipenyeza kwa nia ya kujinufaisha kinyume cha sheria.
Rais alisema katika miaka ya hivi karibuni, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali hususan TAMONGSCO imeongeza sana uwekezaji katika maendeleo ya elimu nchini.
Alisema matokeo yake ni kuwa wamepanua sana fursa za elimu ya awali, msingi, sekondari, ufundi na elimu juu ambapo sasa kuna watoto 1,034,729 katika madarasa ya awali jambo ambalo halikuwepo wakati wa ukoloni.
“ni Sera ya Serikali kwamba kila shule ya msingi iwe na madarasa ya awali sera ambayo imekuwa inatekelezwa vizuri,”alisema
Kikwete alisema kwa elimu ya msingi idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 486,470 mwaka 1961 hadi 8,247,172 mwaka 2012,pamoja na elimu ya sekondari ambapo idadi ya wanafunzi iliongezeka kutoka 11,832 mwaka 1961 hadi 1,884,272 mwaka 2012.
Alisema pia kwa upande wa elimu ya juu imetoka kuwa nchi isiyokuwa na chuo kikuu hata kimoja na wahitimu wasiozidi 10 hadi kuwa na vyuo vikuu 48 vyenye wanafunzi 166,484 mwaka 2012.
0 comments:
Post a Comment