ZAIDI
ya wananchi laki tano wanaojihusisha na kilimo na ufugaji wa kuku wa kienyeji
wanatarajiwa kunufaika na elimu iliyolenga kuwainua kiuchumi ifikapo mwaka
2016.
Elimu
hiyo inayoendeshwa katika wilaya 20zilizopo katika mikoa nane ya kanda ya kati,
inatolewa kupitia mradi wa ukuzaji wa masoko vijijini (RLDC) kwa ushirikiano na
nchi ya Uswisi.
Akizungumza
na waandishi wa habari kuhusiana na elimu hiyo, Meneja wa mradi huo Francis
Massawe alisema hatua hiyo inayotolewa kupitia kwa maafisa ugani, zaidi
imejikita kutoa elimu inayowasaidia wakulima
na wafugaji wa kuku wa kienyeji kuwa na mbinu katika maeneo yao.
Alisema
katika kufanikisha malengo hayo RLDC imekuwa ikiwawezesha wakulima na wafugaji
hao kufuata njia sahihi zikiwemo za utumiaji wa mbinu za kisasa za kilimo ili kupata mavuno yaliyo bora na hivyo
kujiongezea kipato.
"Hii
ni awamu ya nne ya utekelezaji wa mradi wetu tangu ulipoanzishwa mwaka 2005,
malengo ni kuwainua wakulima kutoka mahali na kwenda mbali zaidi" alisema
Massawe.
Alisema
mradi huo umejikita katika mikoa ya kanda ya kati, kutokana na ukweli kuwa
wananchi wa maeneo hayo wanakabiliwa na changamoto nyingi zinazowafanya
washindwe kutekeleza ipasavyo shughuli za kilimo ikiwemo ukame.
"Tumejikita
zaidi katika ukulima wa zao la alizeti, mpunga na ufugaji wa kuku wa kienyeji
na tumeona maeneo hayo hayo yakisimamiwa ipasavyo yataweza kuwainua wananchi
kutokana na umuhimu wake hasa kibiashara" alisisitiza meneja huyo.
Alisema
utekelezaji wa awamu tatu zilizopita, umekuwa
na mafanikio makubwa hasa baada ya wakulima wengi kufanikiwa kupata
mazao mengi yaliyowafanya baadhi yao kujenga nyumba za kisasa.
Alisema
matarajio yao ifikapo mwisho wa utekelezaji wa awamu ya nne mwaka 2016, wataweza kuwa wamewafikia wakulima na
wafugaji karibu milioni moja na hivyo kuwa wamewasaidia kuwainua kiuchumi
kupitia biashara za mazao yao.
Aidha
alisema mradi huo unatekelezwa katika mikoa ya Morogoro, Singida, tabora,
Shinyanga, Manyara, Simiyu na Geita.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment