Maofisa na askari Polisi kote nchini wametakiwa kuendelea kutoa
huduma bora kwa wananchi kwa kuwa suala hilo siyo la hiari bali ni la lazima
kulingana na kanuni pamoja na taratibu za ufanyaji wa kazi za Polisi.
Hayo yalisemwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Said Mwema,
wakati wa kikao cha kikazi kilicho wakutanisha maofisa wa Polisi Makao makuu,
Kanda maalumu ya Dar es Salaam na Vikosi vya Jeshi hilo chenye lengo la
kuwajengea uwezo na kupeana mafunzo yatakayosaidia kufanya kazi kwa weledi
zaidi ili kuweza kukabiliana na vitendo vya uhalifu wa aina mpya unaojitokeza
hapa nchini katika sura mbalimbali.
Aidha, IGP Mwema alisema, kila ofisa na askari polisi anapaswa kutekeleza kwa
vitendo utoaji wa huduma bora ndani na nje, ikiwa na maana kwa askari wenyewe
na kwa wananchi, ili kuendana na maboresho yanayoendelea ndani ya Jeshi hilo na
kuweza kukabiliana na vitendo vya vurugu na matishio mengine ya kihalifu na
wahalifu yanayojitokeza hapa nchini.
Aliwatataka Makamanda na maofisa wa polisi wote kuendelea kuwa karibu na
wananchi ili kujua kero za kiusalama zinazowakabili na kwa pamoja kuweza
kuzitafutia ufumbuzi ili kuondoa hofu ya uhalifu kuanzia ngazi ya familia hadi
Taifa jambo ambalo litaendelea kuimarisha hali ya usalama hapa nchini.
Aidha Mwema, amesema Jeshi la Polisi halitasita kuwachukulia hatua kali
baadhi ya watu wanaotumia mwamvuli wa siasa au dini kama kisingizio cha
kufanya ama kuchochea vurugu hapa nchini kwa kuwa vurugu hizo ni kosa la
jinai kama yalivyo makosa mengine ya jinai.
“Hakikisheni mnawakamata wale wote wanaofanya vitendo vya vurugu kwa
visingizio vya siasa kwa kuwa siasa zao zinaishia pale tu wanapokuwa wamefanya
vitendo vya vurugu ambavyo ni kosa la jinai na sisi hatuwezi kuwafumbia macho”
Alisema Mwema.
IGP Mwema alisema Jeshi la Polisi litaendelea kufanya kazi zake kwa kufuata
kanuni, maadili na taratibu zinazoliongoza katika kuhakikisha amani na usalama
vinadumu hapa nchini na kusisitiza kuwa askari wa Jeshi la polisi si wanachama
wa chama chochote cha siasa japokuwa wanaruhusiwa kupiga kura.
0 comments:
Post a Comment