Help Children
Love them
Saidia Watoto

Wednesday, July 17, 2013

Zanzibar viboko shuleni kama kawa


Na Mdau wa elimu, Zenji
 

JEURI za wanafunzi waliokosa nidhamu shuleni, zimesababisha wawakilishi kuitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali,  irudishe adhabu ya viboko kwa wanafunzi wa shule za Unguja na Pemba.

Mwakilishi wa Chonga, Juma Abdalla Juma (CUF) amesema uamuzi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuondoa adhabu ya viboko, umesababisha wanafunzi kujenga jeuri na
kuzorota kwa nidhamu.

Alisema utaratibu wa zamani uliowekwa katika shule mbalimbali za Unguja na Pemba, wa adhabu za viboko kwa wanafunzi, umesaidia kujenga tabia ya nidhamu.

“Mheshimiwa, sote hapa zamani tumesoma shule kwa kupigwa viboko na kujenga tabia nzuri ya nidhamu na heshima kuanzia shule hadi nyumbani kwetu...hivi sasa wanafunzi hawana nidhamu hata kidogo,” alisema.

Mwakilishi wa Kitope, Makame Mbarouk Mshimba (CCM),  aliitaka Wizara, kurudisha nidhamu kwa wanafunzi wa shule za
Unguja na Pemba.

Mshimba alisema kushuka kwa nidhamu ya wanafunzi kwa kiwango kikubwa, kumesababisha kupungua kwa uwezo wao wa kusoma na kufaulu katika mitihani ya taifa.

“Nidhamu ya wanafunzi kwa sasa imeshuka sana kwa sababu tumekuwa tukiiga utamaduni wa kigeni wa Ulaya, wa wanafunzi kutopigwa bakora,” alisema Mshimba.

Aidha Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu (CUF),
aliitaka Wizara kuacha kupokea maagizo yanayotolewa na washiriki wa maendeleo, kwa kuwa utamaduni kama huo wa kuondoa viboko, haufai kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Zanzibar.

“Mheshimiwa Naibu Spika naiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali,  kuacha kuiga maagizo yanayotolewa na
washiriki wa maendeleo...hivi sasa tumeamua kufuta adhabu za viboko kwa wanafunzi bila ya kufanya utafiti kuhusu athari zake,” alisema Jussa.

Serikali ipo katika mradi wa majaribio kwa baadhi ya
shule za Unguja na Pemba, ambako walimu wametakiwa kufundisha bila ya matumizi ya bakora kwa wanafunzi.

Heshima ya mwalimu
Naye Mwakilishi wa Wawi, Saleh Nassor Juma (CUF), aliitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kurudisha nidhamu na heshima ya kazi ya ualimu ambayo hadhi yake imeshuka.

Juma, ambaye ni mwalimu mstaafu wa masomo ya sayansi, alisema hivi sasa walimu wanakwenda shule wakiwa wamevaa viatu vya kanda mbili maarufu kwa jina la 'yeboyebo'.

“Mheshimiwa Naibu Spika wakati umefika kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kurudisha hadhi na heshima ya kazi ya ualimu ambayo imeshuka kwa kiwango kikubwa kwa sasa...walimu wanakwenda shule wakiwa wamevaa viatu vya kanda mbili? alihoji.

Mwisho…

0 comments:

Post a Comment