CHUO Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili(MUHAS) kinaanza mwezi ujao kujenga chuo kipya kwa ajili ya mazoezi katika eneo la Mloganzila, Kibamba jijini Dar es Salaam.
Ujenzi huo unatarajiwa kuanza Agosti mwaka huu katika eneo hilo na kikimalizika, kitachukua wanafunzi 15,000 watakaosoma taaluma mbalimbali za afya.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye Maonesho ya 37 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu J. K Nyerere jijini Dares Salaam (sabasaba) ,Ofisa Mipango Mkuu wa chuo hicho Ulimbaga Kijobile alisema ujenzi wa chuo hicho, unakadiriwa kufanyika ndani ya mwaka mmoja na wanafunzi wa muhula wa kwanza wanatarajiwa kuanza chuoni hapo mwaka 2015.
Kijobile alisema uamuzi huo umetokana na ongezeko la wanafunzi hivyo kuwa wengi.
Alisema eneo hilo litawezesha wanafunzi hao kupata sehemu za kusomea kwa ufanisi kama vile maabara za kisasa, madarasa, na sehemu za kufanyia mazoezi.
“Tumeamua kuanzisha mradi kwa kujenga chuo kipya kwa sababu MUHAS ina sehemu ndogo na hatuwezi kuipanua kwa ajili ya kuongeza ukubwa wa chuo ili kuweza kutosha kwa wanafunzi” alisema Kajobile.
Aidha alisema wanafunzi hao , walikuwa wakipata tabu katika kufanya mazoezi ,hivyo hulazimika kwenda hospitali za Mwananyamala na Amana.
“Muda mwingine tunatumia hospitali nyingine ili kupata sehemu ya kutosha lakini hospitali hii itakayojengwa itasaidia kuchukua wanafunzi wote ili kuweza kufanya mazoezi yao bila usumbufu” alisisitiza Ulimbaga.
Alisema ujenzi wa chuo hicho, unakadiriwa kufanyika ndani ya mwaka mmoja,ambapo wanafunzi wa muhula wa kwanza wa mwaka 2015 wanatarajiwa kuanza.
Aliongeza kuwa kitatoa huduma za kiafya kama hospitali nyingine hivyo baada ya ufunguzi wake, wananchi watapata matibabu chuoni hapo
0 comments:
Post a Comment