Help Children
Love them
Saidia Watoto

Saturday, July 6, 2013

ELIMU YA BURE: kuweni makini katika kutumia dawa za miti shamba, hasa katika suala la nguvu za kiume

KUTOKANA NA uhitaji mkubwa wa dawa za asili bila ya kuzingatia umakini katika kutumia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), imewaonya wananchi kutotumia dawa za tiba mbadala, zikiwemo zile za kukuza maumbile, ambazo bado hazijasajiliwa na mamlaka hiyo baada ya kuchunguza usalama, ubora na ufanisi wa dawa hizo.

Akizungumza jana na waandishi wa habari, Msemaji wa TFDA, Gaudensia Simwanza, alisema kuwa mamlaka hiyo imetoa nafasi ya watoa tiba mbadala kwenda kusajili dawa zao, lakini mwitiko umekuwa hafifu.

TDFA yenye dhamana ya kusimamia ubora na usalama wa bidhaa za vyakula na dawa, ikiwa ni pamoja na dawa za mitishamba, vipodozi na vifaa tiba vinavyouzwa katika soko la Tanzania, imeeleza kuwa watoa huduma wa tiba mbadala, wengi  hawako tayari kubainisha aina ya mchanganyiko wa dawa hizo.

 “Tumekutana na changamoto kubwa katika usajili wa hizi dawa, ukiwauliza aina ya dawa zilizomo kwenye mchanganyiko wa dawa zao, wanasema ni siri. Pia ukiangalia uhalisia wa kile wanachokitangaza, hakuna ukweli wowote. Wananchi wanatakiwa kuwa makini na tiba za aina hii.

 “Ili kukomesha hali hii, tulipeleka waraka kwa wamiliki wa vyombo vya habari, kuwataka waache kutangaza tiba ambazo hazijathibitishwa na TFDA, lakini nalo limekuwa gumu, sasa tutaangalia uwezekano wa kwenda chombo kimoja baada ya kingine,” alisema.

Alipomuuliza Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsacris Mwamwaja, alimtaka mwandishi wizarani kupata maelezo zaidi.

Akizungumzia suala la kudhibiti vipodozi vyenye kemikali zizisofaa kwa matumizi ya binadamu, Simwanza alisema TFDA imejipanga kudhibiti soko la Tanzania, ili kuhakikisha vipodozi vilivyopigwa marufuku haviko tena sokoni.

*Vipodozi hatari

Alisema pamoja na juhudi hizo, bado bidhaa hizo zinaingia kupitia mianya ya uingizaji wa bidhaa hizo kwenye mipaka isiyo rasmi.

“Kwenye mipaka yetu tunawataalamu wetu wa kukagua, lakini kumekuwapo na mianya mingi ya bidhaa hizi kuingia kutokana na kuwapo mahitaji ya watumiaji ambao hawako tayari kuacha. Kwa sababu udhibiti wa mipaka ni mgumu, tunaimarisha ukaguzi katika soko la ndani,” alisema.

Uvumi dawa za maumivu

Kuhusu na taarifa ya kuwa dawa za maumivu za Diclopar na Diclofenac kuwa na hatari, Simwanza alisema mpaka sasa hawajapata taarifa ya hatari ya dawa hizo kutoka Shirika la Afya la Kimataifa (WHO), hivyo bado ni salama kwa matumizi na kuwataka wananchi kutumia dawa hizo kwa kuzingatia maelekezo ya daktari.

Aidha, Simwanza alisema tangu kuanzishwa kwa maabara ya TFDA mwaka 2003, sampuli mbalimbali zimechunguzwa zikiwemo za chakula sampuli 5,173, dawa sampuli 6,163, vipodozi sampuli 307 na vifaa tiba sampuli 36.

Alisema katika Mfumo wa Ufuatiliaji Dawa kwa Lengo la Kujiridhisha na Usalama, Ubora na Ufanisi wa Dawa (PMS), katika kipindi cha Julai 2008 hadi mwaka jana, sampuli 1,827 zilichukuliwa katika soko na kuchunguzwa katika maabara ya TFDA ambapo sampuli 1,670 zilikidhi vigezo.

Aidha, Simwanza alisema kupitia matokeo ya uchunguzi wa kimaabara katika kipindi cha takribani miaka 10, bidhaa mbalimbali duni na bandia, zilibainika na kutolewa katika soko zikiwemo za chakula (84), dawa (71), vipodozi 2,764 na kifaa kimoja cha tiba.

 (mwisho)

0 comments:

Post a Comment