Help Children
Love them
Saidia Watoto

Saturday, July 27, 2013

Vyuo vikuu vya afya kutoa elimu ya tiba asilia

Na Mwandishi
WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imesema ipo haja siku zijazo kuanzishwa kwa vyuo vya elimu ya tiba ya asili na tiba mbadala ili kuwasaidia wananchi kupata huduma za afya kwa usalama zaidi.

Aidha, imewataka waganga wa tiba asili kuandika historian a taarifa za wagonjwa wanaowahudumia kwa lengo la kuwezesha kupata takwimu za kweli za wanaohudumiwa na maendeleo ya afya zao kupitia tiba hizo.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Tiba Asili na Tiba Mbadala, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Paulo Mhame aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akitoa semina kwa waandishi wa habari za afya jijini Dar es Salaam kuhusu hali ya tiba asili na tiba mbadala nchini.

Dk Mhame alisema Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala namba 29 ya mwaka 2002 iliwezesha kuundwa kwa Baraza la tiba hizo mwaka 2005 na mwaka 2010 fomu za usajili wa wanaotoa huduma hizo zikaanza kutolewa nchini ili kurasimisha huduma baada ya kuwepo waganga matapeli.

Kwa mujibu wa takwimu, mpaka sasa nchini kuna waganga 2,221 wa tiba asili waliosajiliwa, wengi wakiwa wamerithishwa tiba za kiutamaduni kutoka kwa jamii zao na waganga wasiozidi 12 wa tiba mbadala ambao hutumia vifaa kama vya hospitali.

“Nchi za wenzetu tiba za asili zinafundishwa vyuoni na kwa upande wa tiba mbadala, zipo ngazi za vyeti, stashahada na shahada ambapo mtu mwenye shahada ndio anayepaswa kupewa hadhi ya daktari lakini huku kwetu, vibao vimetapakaa kila kona vikieleza kuhusu madaktari bingwa wa tiba hizi, si sawa,” alisema Dk Mhame.

Alisema ni matarajio na dhamira ya serikali kuhakikisha kuwa, tiba inakuwa huduma kwa mwananchi na sio biashara, hivyo matarajio ya baadae ni kuona kuna vyuo vya kufundisha tiba mbadala na zile za asili, ili kukwepa madhara yanayoikumba jamii kwa sasa.

Kwa mujibu wa Dk Mhame, hivi sasa nchi za mashariki ya mbali na Asia, wanasoma darasani kuhusu tiba asili na zipo tiba zilizo rasmi kwa jamii ambazo zinatumiwa hata ngazi za kimataifa. Alisema ikiwa kwa maandishi ni rahisi kufuatilia matokeo ya tiba na afya ya mhudumiwa tofauti na ilivyo sasa.

“Natambua mnajua kila kitu kinachoitwa dawa, kina madhara, nimewahi kusikia watu wanapewa dawa za maji mpaka lita tano wakatumie, hii ni kosa kubwa kitabibu, hakuna daktari anayeweza kukupa dawa zaidi ya nusu lita, hasa hizi za kienyeji maana itachacha na kukuletea madhara, zile za kisasa zimewekewa kinga, nawaomba Watanzania muwe macho,” alisisitiza Dk Mhame.

Ingawa hakusema wazi kuwa vyuo vya elimu ya tiba asili nchini vitaanza lini, alisema ni matarajio ya mbele na kwamba jambo hilo kwa asilimia kubwa litaihusisha sekta binafsi ambayo ina waganga wengi wa tiba asili na serikali kama mtunga sera, itasimamia kama ilivyo kwa maduka ya tiba asili ambayo hivi sasa ni rasmi nchini.

Mwisho.

0 comments:

Post a Comment