SERIKALI imeshauriwa kuboresha mfumo wake wa utoaji elimu kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wengi kufanya vizuri katika masomo na hivyo kuondoa tatizo la vijana wanaohitimu katika ngazi mbalimbali hasa za Sekondari kuishia mitaani.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi inayojishughulisha na kuwaandaa wanafunzi kusoma nje ya nchi ‘Global Education Link’ (GEL) Abduimalik Mollel, alipokuwa akizungumza na gazeti hili kuhusu maendeleo ya sekta ya elimu nchini.
Alisema mfumo wa sasa wa elimu unaotolewa nchini, kwa kiasi kikubwa umekuwa ukiwaondolea uaminifu wazazi wengi hasa kutokana na matokeo yasiyo mazuri kwa watoto wao, suala alilosema pia linafanya wazazi hao hasa wenye uwezo kufikiria kuwapeleka watoto wao kusoma nje ya nchi.
Alisema kutokana na hali hiyo idadi ya wanafunzi kwenda kusoma nje ya nchi pia imekuwa ikiongezeka siku hadi siku tofauti na miaka ya nyuma , jambo alilosema kuwa limetokana na wazazi wao kukatishwa tamaa na mfumo huo.
“Hata hivyo siyo wazazi wote wana uwezo wa kuwapeleka watoto wao nje ya nchi kwa ajili ya kuendelea na masomo,cha muhimu ni Serikali kuangalia upya mfumo wake wa elimu ili kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi na kuondoa tatizo lililopo sasa” alisema Mollel
Alisema hata suala la tatizo la umri lililosababisha baadhi ya wanafunzi kukosa nafasi ya kujiunga na kidato cha tano halikuwa na msingi wowote kwa kuwa hata kabla ya kujiunga na kidato cha kwanza tayari umri wao ulijulikana hivyo walipaswa kuwekewa utaratibu unaotambulika tangu mapema.
Akitolea mfano wa wanafunzi waliofika katika taasisi yake kwa ajili ya kutafuta nafasi ya kwenda kusoma nje ya nchi tangu kutolewa kwa matokeo ya kidato cha nne, Mollel alisema idadi yao imeongezeka tofauti na miaka mitatu hadi minne iliyopita.
Alisema katika kipindi cha kuanzia Juni hadi sasa, taasisi yake imepokea maombi zaidi ya 800 ya wanafunzi waliomaliza kidato cha nne wanaotaka kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kuendelea na elimu katika vyuo mbalimbali.
Alisema hata idadi ya mawakala wanaohusika na utafutaji wa nafasi za vyuo nje ya nchi kwa ajili ya wanafunzi wanaotaka kwenda kujiunga pia imeongezeka na kuwa zaidi ya 20 ikilinganishwa na mawakala wawili miaka kumi iliyopita, suala alilosema limetokana na kuongezeka kwa mahitaji ya wanafunzi.
ends
|
0 comments:
Post a Comment