MWANAFUNZI wa kidato cha
nne, Flora Athanas (18) wa shule ya sekondari Mzindakaya wilayani Sumbawanga
mkoani
Rukwa, amejiua kwa sumu ya
panya, baada ya kubakwa na mtu asiyefahamika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Rukwa, Jacob Mwaruanda, alisema jana kuwa mwanafunzi huyo alibakwa usiku wa
kuamkia Jumanne ya wiki hii yeye na mwenzake mmoja, katika chumba kimoja
walichopanga, kutokana na kukosekana kwa mabweni katika shule hiyo.
Kwa mujibu wa Kamanda Mwaruanda,
siku hiyo Flora alikuwa na wanafunzi wenzake watatu, aliokuwa akiishi nao katika
chumba hicho, maarufu geto.
Inadaiwa usiku mtu
asiyefahamika, alivamia nyumba waliyokuwa wamepanga, akafunga vyumba vya
wanafunzi wengine na kuingia katika chumba cha kina Flora akiwa ameshika kisu,
na kuwatishia kuwa atakaye piga kelele atamuua kwa kumchoma kisu.
Kutokana na tishio hilo,
inadaiwa wanafunzi hao walikaa kimya ambapo mvamizi huyo alimbaka Flora na
mwenzake mmoja na kumuacha mwingine kabla ya kuondoka na kukimbilia kusikojulikana.
Asubuhi ya siku hiyo, Flora
alipoamka, inadaiwa alitoroka na kwenda katika moja ya duka lililopo kijijini
hapo na kununua sumu ya panya.
Inadaiwa aliondoka na
sumu hiyo kwenda katika pori lililopo nje kidogo ya Kijjiji cha Kaengesa, ambapo hufanyika mnada wa
hadhara na kuamua kukatisha maisha
yake kikatili kwa kunywa sumu hiyo na kufariki dunia.
“Uchunguzi wa awali wa Polisi
unaonesha kuwa kifo hicho kimesababishwa
na hasira aliyokuwa nayo msichana huyo,
baada ya kubakwa na mtu asiyejulikana
hivyo akachukua uamuzi huo mgumu wa kukatisha
maisha yake kwa kunywa sumu inayosadikiwa kuwa ya panya,“ alisema
Mwaruanda.
Kamanda Mwaruanda alisema
mwanafunzi mwenzake aliyebakwa pamoja naye, alifikishwa katika kituo cha afya
Kaengesa, ambapo alifanyiwa uchunguzi wa kitabibu kuthibitika kuwa alibakwa.
Katika kituo hicho cha
afya, ndiko pia mwili wa marehemu ulipopelekwa kwa uchunguzi, ambako
ilithibitika kuwa chanzo cha kifo hicho ni sumu ya panya.
Blog hii: inasikitishwa na tukio hilo la ubakaji na waharifu lazima wakamatwe
0 comments:
Post a Comment