UTEUZI
wa Tume ya Kuchunguza Matokeo ya Kidato cha Nne, umeamsha mjadala kuhusu muda
uliotolewa kukamilisha kazi hiyo na aina ya wajumbe wanaopaswa kutekeleza
majukumu yake.
Wakizungumza
na gazeti hili jana, baadhi ya wasomi walisifu hatua ya Serikali kuteua Tume hiyo
ili kuondoa mkanganyiko uliopo, kuhusu chanzo cha matokeo mabaya ya kidato cha
nne yaliyotangazwa hivi karibuni.
Mhadhiri
wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, Dk Ayub Rioba, alisema wazo la Serikali ni zuri kwa kuwa
litaondoa mkanganyiko huo.
“Kama
alivyosema Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake na pia Waziri Mkuu Mizengo
Pinda, matokeo ya Tume yatasaidia kuondoa watu wanaoongea ovyo bila uhakika.
Kila jambo lina sababu, mambo hayatokei hivi hivi lazima kuna chanzo,” alisema
Dk Rioba.
Hata
hivyo, alionesha wasiwasi wake kuhusu muda wa wiki sita uliotolewa kwa Tume
hiyo ya wajumbe 15, wakiongozwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU),
Profesa Sifuni Mchome na kupendekeza usingekuwa chini ya miezi miwili.
“Ili
kupata matokeo ya kina, ni wazi muda waliopewa ni mdogo, maana ukiangalia
hadidu za rejea wanahitaji kwenda mbali zaidi, si kuangalia matokeo ya mwaka
huu pekee bali zaidi ya hapo, ila pengine kwa sababu utafiti mbalimbali upo,
wanaweza kuutumia na muda ukatosha,” alisema Dk Rioba.
Kuhusu
wajumbe wa Tume hiyo iliyoteuliwa na Pinda juzi, Dk Rioba alisema hana shaka
nao, ni watu wenye weledi na uzoefu mkubwa wa masuala ya elimu. Alitoa mfano
Profesa Mchome, kuwa ni msomi na Mwanasheria aliyebobea na mwenye weledi.
Dk
Rioba pia alisifu hatua ya Serikali kuchanganya wajumbe wa Tume na kuwaweka
wanaotoka asasi za kiraia ikiwemo Twaweza, inayowakilishwa na Mwenyekiti wake,
Rakesh Rajab, kwa kuwa ni watu wanaojihusisha na utafiti mbalimbali kuhusu
elimu hapa nchini.
“Sina
wasiwasi kabisa na wajumbe wa Tume walioteuliwa, wengi ni wazoefu na
wanawakilisha jamii, ninavyoelewa maana ya Tume ni mkusanyiko wa watu wenye
mchango na uelewa fulani katika eneo linalohitajika.
“Si
lazima wawe moja kwa moja wahusika wa eneo hilo, wanachotakiwa ni kupata maoni ya walimu
wakongwe wa sekondari na shule za msingi,” alisema Dk Rioba.
Dk
Bana na wajumbe
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na
Utawala, Dk Benson Bana, naye aliipongeza Serikali kwa hatua hiyo na wazo zuri
la kutafuta suluhu ya tatizo la kushuka kwa elimu nchini.
Hata
hivyo, Dk Bana alisema wazi kuwa pamoja na kwamba muda hautoshi, hana imani na
baadhi ya wajumbe.
“Ni hatua nzuri Serikali imechukua ili
ituridhishe wananchi, lakini binafsi sijaridhika na uteuzi na weledi wa
wajumbe, ilipaswa iwe na walimu waliobobea katika elimu ya sekondari nchini,
sioni kama wana uzoefu na uchungu wa elimu ya sekondari, hawatakuja na jipya.
“Baadhi ya wajumbe ni wanaharakati, unawekaje
mwanaharakati kama Mbatia (James, Mbunge Mteule na Mwenyekiti wa Taifa wa
NCCR-Mageuzi) au Rakesh (Mwenyekiti-Taasisi ya Twaweza)?
“Pia
hii si tume ya maprofesa na madokta wa vyuo vikuu, kuna tofauti ya mhadhiri na
mwalimu, sina hakika kama Mwenyekiti, Profesa Mchome amewahi kufundisha
sekondari,” alisema Dk Bana.
Kuhusu
muda, Dk Bana alisema wiki sita zilizotolewa kwa Tume hiyo aliyoiita ‘Tume ya
Mitihani’, hautoshi hata kupata jawabu
la matokeo mabaya mwaka huu.
Alisema
tatizo la elimu halipo katika shule za msingi na sekondari pekee, bali mpaka
vyuo vikuu kuna madudu makubwa.
Msomi
huyo alipendekeza Tume hiyo ifanye kazi kwa miaka miwili na si vinginevyo kama
ilivyokuwa Tume ya Elimu ya Makwetta (marehemu Jackson), aliyewahi kushika
nyadhifa mbalimbali, ikiwemo Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu kati
ya 1995-1998.
Waliopata
sifuri
Mbatia
jana alipotafutwa kueleza hatima yake katika Tume hiyo baada ya kuonekana kajitoa
katika Tume, alisema leo atakutana na waandishi wa habari kueleza kila kitu.
Tume
“Tumepokea
uteuzi, kuna kazi kubwa mbele yetu, tutawashirikisha watu wengi kadiri
iwezekanavyo ila ni mapema kusema tutakaozungumza nao, hilo la muda tuachwe
tuanze kazi kwanza ndipo tutajua huko mbele, sina wasiwasi na wajumbe,
tutafanya kazi pamoja,” alisema Mushashu.
Mkuu
wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu hakutofautiana na wasomi kuhusu muda
kuwa mdogo na kuitaka Tume kufika mpaka vijijini waliko walimu wazoefu zaidi ya
miaka 25 hadi 30, ili kupata maoni yao kuhusu elimu ya sasa.
“Isiishie
katika matokeo, binafsi naomba wafike vijijini kuliko na matatizo ya
miundombinu na kwenye uhaba wa walimu hasa wa Sayansi, ipo shule hapa
mwanafunzi anatembea kilometa 24 kwenda na kurudi, huyu unataka afaulu kweli?”
Alihoji Muhingo ambaye kitaaluma ni mwalimu na mwandishi wa habari.
Muhingo
aliiomba Tume iangalie upya utaratibu wa ufundishaji wa walimu vyuoni, hasa
wanaochukua shahada ambao alidai wengi wanalalamikiwa kutokuwa na maadili, wala
uchungu na elimu ya watoto wanaowafundisha.
Mbali
na Profesa Mchome na Mushashu, Tume hiyo imeshirikisha wajumbe kutoka Zanzibar
na Tanzania Bara kutoka taasisi binafsi, serikalini na vyuo vya elimu ambao
wote ni wadau katika elimu nchini.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment