Waliofaulu kujiunga na masomo ya sekondari katika shule
za Serikali, lakini watalazimika kufanya mtihani mwingine wa taifa ili
kuwabaini wanafunzi ambao hawajui kusoma wala kuandika.
Mtihani huo kwa mujibu wa Waziri wa Elimu
na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa utatungwa na wizara hiyo na watafanya
wanafunzi wote watakaokuwa wameanza masomo ya sekondari na wale watakaobainika
hawajui kusoma wala kuandika, watafutiwa usajili wao.
WANAFUNZI hao ni 560,706 wa shule ya msingi sawa na
ongezeko la asilimia 8.8
Dk Kawambwa ambaye jana alitangaza matokeo
ya mtihani wa elimu ya shule ya msingi ambao uliofanyika Septemba mwaka huu,
alisema wizara imechukua uamuzi huo baada ya mwaka jana kupokea majina ya
wanafunzi wapatao 4,000 waliojiunga na masomo ya sekondari wakati hawajui
kusoma wala kuandika.
“Tutafanya hivyo kila mwaka ili
kuhakikisha wanafunzi wanaojiunga sekondari ni wale tu wenye uwezo ambao
wanastahili kujiunga na kiwango hicho cha elimu,” alisema Dk Kawambwa.
Mtihani wa
kuchagua
Wanafunzi hao waliofaulu walifanya mtihani
ulio kwenye mfumo wa maswali ya kuchagua ambao umekuwa ukilalamikiwa na wadau
wa elimu kuwa ni mfumo dhaifu unaosababisha wanafunzi wanaofaulu wasiwe na
uwezo wa kujieleza na kupambanua mambo.
Katika makongamano kadhaa ya elimu ya hivi
karibuni yakiwashirikisha walimu na wasomi wa vyuo vikuu, wadau walishutumu
mfumo huo kuwa unasaidia kufaulisha wanafunzi wasio jua kusoma na kuandika,
lakini pia wanafunzi wanakosa uwezo wa kujieleza kwa ufasaha.
Katika mikoa ya Dar es Salaam na Katavi,
baadhi ya wananchi na wanafunzi ambao walipata fursa ya kutoa maoni mbele ya
Tume ya Marekebisho ya Katiba nao walishutumu mfumo wa elimu na kutaka mitaala
irekebishwe ili kuwezesha wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi wawe na uwezo
wa kujiajiri na
kujieleza pia.
Lakini Dk Kawambwa alitetea mfumo huo kuwa
ni mfumo bora na umekuwa ukitumika miaka mingi na unawashirikisha walimu katika
kutunga maswali. Alisema mfumo huo unatoa fursa ya mwanafunzi kuchagua jibu
sahihi kati ya majibu manne yanayofanana kwa ukaribu.
“Sio mfumo rahisi kama unavyodai, ni mfumo
ambao mwanafunzi anatakiwa awe makini katika kuchagua jibu,” alisema Dk
Kawambwa na kujitetea kuwa sio Tanzania
pekee inayofuata mfumo huo.
Kompyuta
msahishaji
Waziri licha ya kutetea mfumo huo wa maswali
ya kuchagua, alisema mtihani huo ulikuwa wa kwanza nchini kusahihishwa kwa
kutumia teknolojia mpya ya Optical Mark Reader (OMR) ambayo kompyuta ilitumika
kusahihisha mtihani huo.
Mfumo huo wa usahihishaji kwa mujibu wa Dk
Kawambwa umesaidia kupunguza gharama kwani walimu wapatao 250 tu ndio
walishiriki kusimamia usahihishaji kwa wiki mbili wakati mwaka jana walitumia
walimu 4,000 kusahihisha mtihani kwa mwezi mzima.
“Hebu fikiria hizo gharama tulizokuwa
tunainga kuliweka kundi lote hilo
kambini kwa mwezi mmoja ni kipindi kirefu na fedha nyingi zinatumika,
teknolojia hii imesaidia kupunguza gharama kwa Serikali,” alisema Waziri.
Ufaulu wa
wanafunzi
Katika matokeo ya mtihani huo, Dk Kawambwa
alisema wanafunzi waliofaulu ni asilimia 64.74 ya wanafunzi 865,827 waliofanya
mtihani huo. Awali idadi ya wanafunzi ambao walisajiliwa kufanya mtihani
ilikuwa ni 894,839 hivyo idadi ya waliofanya ni asilimia 96.76.
Watahiniwa 29,012 sawa na asilimia 3.24
hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro, vifo na
ugonjwa. Kati ya hao wasichana ni 12,501 na wavulana ni 16,511.
Waziri alisema matokeo hayo yanaonesha
kuwa alama ya juu kabisa ilikuwa 234 kati ya 250 kwa wasichana na wavulana.
Alifafanua kuwa watahiniwa 3,087 walipata
alama A, wanafunzi 40,683 walipata alama B, wanafunzi 22,103 walipata alama C
wakati watahiniwa 73,264 walipata alama E.
Kati ya wanafunzi 560,706 ambao wamefaulu
kati ya hao wasichana ni 281,460 sawa na asilimia 50.20 na wavulana ni 279,246
sawa na asilimia 49.80.
Takwimu hizo zinaonesha pia kwamba idadi
ya waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza imeongezeka kwa asilimia 8.8
ikilinganishwa waliochaguliwa awamu ya kwanza mwaka jana.
Udanganyifu
wapungua
Dk Kawambwa amesema vitendo vya
udanganyifu vimepungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na mwaka jana. Alisema
mwaka huu, idadi hiyo imepungua hadi kufikia wanafunzi 296 tu ambao wamefutiwa
matokeo kwa udanganyifu wakati mwaka jana idadi hiyo ilikuwa ni 9,736.
“Serikali itawabaini wale wote waliohusika
katika udanganyifu huo na kuwachukulia hatua stahiki,” alisema Dk Kawambwa.
0 comments:
Post a Comment