SERIKALI imejipanga kuvikopa vyuo vikuu hapa nchini kwa ajili ya ada ya wanafunzi 1107 wa masomo ya kipaumbele waliokosa mkopo kutokana na fomu za maombi kuwa na dosari.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema hatua hiyo ni katika kutoa nafasi kwa wanafunzi hao hasa kutokana kompyuta kuwa na matatizo na baadaye kutoa fedha hizo kwa wanafunzi wengine.
“Ni kweli kosa limefanyika na Bodi, pamoja na kuwa na haki kisheria kuhamisha fedha kwa wanafunzi wengine walitakiwa kushauliana na Wizara kabla ya uamuzi huo ili kupata maoni ya nini kifanyike, hivyo tumefikia uamuzi wa kuwapa nafasi nyingine wanafunzi wenye masomo ya vipaumbele,” alisema.
Wanafunzi hao 1107 ni miongoni mwa wanafunzi 1661 ambao walikosa mkpo katika mwaka wa masomo 2013/2014 kutokana na kuwa na dosari mbalimbali.
Mulugo alisema tayari wameiagiza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kutafuta kiasi cha sh bilioni 2 kutoka kwenye makusanyo ya wadeni au fedha za matumizi mengine na wizara itatoa kiasi cha bilioni 1.1 ili kufikisha sh bilioni 3.1 zitakazotumiwa na wanafunzi hao.
Akitia mchaganuo huo, Mulugo alisema zaidi ya sh bilioni 1.9 zitatumika kwa ajili ya chakula na malazi, sh milioni 221.4 kwa ajili ya vitabu na viandikio, sh milioni 686.34 kwa ajili ya mafunzo ya vitendo na sh milioni 221.4 za mahitaji maalumu ya vitivo.
“ Katibu anakwenda kuviandikia vyuo kuwapokea wanafunzi hao na suala la ada liwe deni kwa serikali ambayo tutalilipa katika bajeti ijayo, tunaamini kuwa fedha hizi hazitavuruga matumizi ya vyuo kutokana na kuwa vyuo vingi vina idadi ndogo ya ya wanafunzi hawa,” alisema.
Mulugo alitaja wanafunzi watakaonufaika kuwa ni wanafunzi wa ualimu wa Hisabati(20), Sayansi(164), wanafunzi wa Sayansi na Tiba(111), uhandisi –umwagiliaji(7), ualimu (617), Sayansi ya kilimo(20), Uhandisi (70) na Sayansi (98).
“Wanafunzi ambao wanatakiwa kurekebisha dosari zao wakashindwa kufanya hivyo wakati huu, hakutakuwa na huruma tena na fedha tutawapa wahitaji wengine. Majina yao yatatolewa na bodi hivyo wazingatie hili,” alisema.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Asangye Bangu kutokana na bajeti iliyotengwa, wanafunzi 31,539 ambayi ni asilimia 99.6 kati ya wanafunzi 31,647 waliotarajiwa kupatiwa mikopo. Asilimia 83 ya wanafunzi hao wamedahiliwa katika kozi za kipaumbele na kayi yao asilimi 44 wamedailiwa katika kozi ya ualimu zisizo za sayansi.
Alisema asilimia 29 ya walimu waliodailiwa kwenye kozi za kipaumbele za kozi za sayansi ya tiba, ualimu wa hisabati, ualimu wa sayansi, uhandisi wa mwagiliaji, uhandisi na sayansi za wanyama wakati asilimia 17 ni wanafunzi wa kozi zingine zisizo za kipaumbele.
Bangu alisema katika mwaka wa masomo 2013/2014 Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi iliidhinisha jumla ya sh bilioni 325 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ambapo kiasi cha sh bilioni 306 zinatoka serikalini na sh bilioni 19 zinatokana na marejesho ya mikopo lengo likiwa ni kukopesha wanafunzi 94,023 ikiwa ni wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea na masomo.
Wizara ya elimu na uongozi wa HESLB walikutana na Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kufuatia wanafunzi wapatao 36 kwenda kuonana na kamati hiyo kuasilisha kilio chao cha kukosa mkopo.
(mwisho)
0 comments:
Post a Comment