WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kupitia Mradi wa Sayansi Teknolojia na Elimu ya Juu (STHEP), inatarajia kuanzisha Taasisi itakayofanyia utafiti vyuo vikuu nchini ili kuona namna vinavyotoa elimu kulingana na soko la ajira.
Hayo yalibainishwa na Mratibu wa mradi huo Dk Kennedy Hosea, wakati akizungumza na gazeti hili juzi ambapo alisisitiza kuwa kwa sasa vyuo vingi nchini vinazalisha wahitimu ambao soko la ajira haliwataki.
Alisema kupitia taasisi hiyo kutakuwa na mtu ambaye kazi yake ni kuangalia soko la ajira nchini lilivyo na kulinganisha na elimu inayotolewa katika vyuo hivyo vya elimu juu ili kuona kama vitu hivyo viwili vinaendana na kupendekeza nini kifanyike.
“Tunatarajia kuipatia Serikali ripoti ya namna taasisi hiyo ya ambayo itajulikana kama Treasury Labour Market Observatory (TELMO), itakavyokuwa,” alisisitiza Dk Hosea.
Alisema kwa kuanzia taasisi hiyo itaanza kama ofisi ndogo na baadaye itaakuwa kama wakala ambaye kazi yake ni kutafiti na kushawishi vyuo vifundishe masomo yenye manufaa katika eneo la ajira na yapi yasifundishwe.
“Tunatarajia hadi kufikia Desemba mwaka huu, mchakato wa kuanzisha TELMO utakuwa umekamilika. Kwa sasa tayari kazi imeanza ya utafiti ambapo watalaamu kupitia mradi huo wa STHEP wameanza kuzungumza na baadhi ya vyuo na waajiri,” alisema.
Aidha Dk Hosea, alisema kupitia mradi huo pia kutaanzisha mfuko maalum kwa ajili ya kusaidiana na bajeti ya Serikali katika kugharamia utafiti na ufundishaji wa elimu ya juu.
“Mfuko huu utakuwa unachangiwa na wadau wa maendeleo nje ya Serikali, na lengo lake hasa ni kusaidia bajeti ya Serikali ili kuboresha sekta ya elimu nchini,” alisema.
Mradi wa STHEP unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, ulianza rasmi mwaka 2008 unaotekelezwa na takribani taasisi 15 za umma tayari utekelezaji wake umefikia asilimia 92 na unatarajiwa kukamilika rasmi Februari mwakani na gharama ya uendeshaji wake inakadiriwa kufikia dola za Marekani milioni 100.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment