SERIKALI imetaka wakuu shule kuwa mstari wa mbele kutatua baadhi ya changamoto zinazokabili shula na walimu wakati serikali ikiwa inashughulikia matatizo yao.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Consolata Mgimba alipokuwa akitoa salamu za Katibu Mkuu, Profesa Sifuni Mchome wakati wa kufunga kitaifa mafunzo ya wakuu wa shule za sekondari Tanzania bara kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES II).
Alisema serikali inatambua changamoto zinazokabili ikiwa ni pamoja na madeni, uhaba wa nyumba za walimu na kuwataka wakuu wa shule kuwa mstari wa mbele katika kutatua baadhi ya changamoto badala ya kuwa sehemu ya kuvunja moyo walimu.
Alisema ni imani yake kuwa wakuu wa shule watakuwa mstari wa mbele katika kutekeleza mkakati wa serikali wa Matokeo Makubwa ya haraka sasa (BRN) ili kuweza kuboresha ufaulu wa wanafunzi na kuinua kiwango cha elimu hapa nchini.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), Dk Sisten Masanja alisema mafunzo hayo yamefanyika baada ya kubainika kuwapo upungufu kwa baadhi ya wakuu wa shule katika uongozi na utawala, usimamizi na uandishi wa ripoti za matumizi ya fedha na ufuatiliaji na tathimini.
0 comments:
Post a Comment