Help Children
Love them
Saidia Watoto

Sunday, October 6, 2013

Madarasa yanayovuja Kunduchi yapatiwa msaada


Na Mdau wa Elimu
MADARASA matatu ya shule ya msingi Kunduchi iliyopo jijini Dar es Salaam yanavuja kiasi ambacho yamefungwa na kushindwa kuendelea kutoa huduma ya elimu kwa wanafunzi wa shuleni hapo.


Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Pelagia Mdimi aliyasema hayo kayika maadhimisho ya miaka 25 ya benki ya Eco Tanzania ambayo imetoa misaada mbalimbali kwa shule hiyo ambayo imegharimu Sh milioni 48.


Katika maadhimisho hayo benki ya ECo imetoa madawati 50, daftari 3000, viti na meza za walimu 50, penseli 2000 pamoja na kukarabai na kupaka rangi darasa la saba.


Akizungumza katika maadhimisho hayo Mwalimu Pelagia alisema madarasa yanayovuja ni matatu na kwamba yalijengwa kwa msaada wa serikali ya Japan mwaka 2002 ambapo kwa sasa hayatumiki kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa .


"Shule hii ina wanafunzi takribani 2099 na walimu 51 ambapo tatizo la ukosefu wa madarasa ni jambo ambalo limekuwa likitukwaza katika kutoa elimu iliyo bora kwa wanafunzi wetu" alisema Pelagia na kuongeza kuwa hata walimu hawana ofisi ya kufanyia kazi jambo ambalo limesababisha kuchukua darasa moja n akulifanya ofisi.


Alisema kutokana na kukabiliwa na ukosefu wa madarasa pamoja na hayo yanayovuja, wanatoa wito kwa wananchi kujitokeza kuchangia ili waweze kuendeleza juhudi za kutoa elimu iliyo bora kwa wanafunzi wa shule hiyo.


Kwa upande wake Ofisa Mkuu wa Fedha wa benki hiyo Isaac Chahe alisema katika kuadhimisha miaka hiyo benki hiyo imeazimia kuboresha elimu kwa kiwango chao huku wakilenga shule za msingi ili kuwajengea wanafunzi mazingira mazuri ya kupata elimu.


"Tunaamini  kuwa mchango wetu katika kutoa vifaa hivi utasaidia kwa kiasi kikubwa  kuboresha uelewa na hatimaye matokeo ya mtihani wa wanafunzi kwa mwaka ujao" alisema Chahe.


Hata hivyo aliahidi benki hiyo kuongeza jitihada ili kuleta maendeleo zaidi katika sekta ya elimu na hasa shule za msingi nchini kwani wanalo azimio la kuboresha uchumi na maendeleo katika nchi kupitia nyanja ya mbalimbali.
MWISHO.


0 comments:

Post a Comment