Na Elimubora
WALIMU
watatu wa Shule ya Msingi Misingeni mkoani Kigoma Ujiji
wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao kufuatia kushambuliwa na kundi la
wazazi wenye watoto kwenye shule hiyo.
Habari
za uhakika zilizopatikana mjini hapa na baadaye kuthibitishwa na uongozi wa shule hiyo
zinaeleza kuwa uvamizi huo wa wazazi hao unafuatia kupiga kitendo cha mwalimu
mmoja wa shule hiyo kuwaadhibu watoto wao.
Hilda Msita ambae ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, alisema kuwa chanzo cha
mgogoro huo kinatokana na wazazi kupinga kitendo cha Mwalimu wa shule hiyo,
Mathias Banzi kuwaadhibu watoto wao kwa kuwachapa viboko kutokana na
utovu wa nidhamu.
Alisema baada ya kutokea vitendo hivyo vya utovu wa nidhamu kwa watoto
hao Mwalimu Banzi aliwachapa viboko wanafunzi hao na ndipo mwanafunzi mmoja
(Fadhili Mlibo) alikimbia na kwenda kutoa taarifa kwa wazazi wake kuhusu jambo
hilo.
Mwalimu Mkuu
wa shule huyo, Hilda Msita aliwataja walimu waliojeruhiwa kwenye sakata hilo
kuwa ni pamoja na Mathias Banzi, Barnabas Matalisi na Sikujua Bunoge ambao
baada ya kipigo cha wazazi hao walitibiwa katika hospitali ya mkoa Kigoma
Maweni na kuruhusiwa.
Alisema kuwa
baada ya kufika nyumbani na kutoa taarifa kwa wazazi wake, Mama wa mwanafunzi
huyo, Amina Rashidi aliwaeleza wazazi wengine wenye watoto shuleni hapo na
ndipo kundi la wazazi zaidi ya 20 walivamia shuleni hapo wakiwa na silaha za
jadi na kuwajeruhi walimu.
Kwa upande
wake Kaimu Kamanda wa polisi mkoa Kigoma, Mohammed Kihenya amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kwamba polisi inamshikilia Amina Rashidi mzazi wa
mmoja wa watoto walioadhibiwa katika sakata hilo.
Kamanda
Kihenya alisema kuwa pamoja na kumshikilia mzazi huyo kwa kufanya vurugu mahala
pa kazi na kujeruhi pia inawatafuta watu wengine ambao walihusika katika vurugu
hizo.
0 comments:
Post a Comment