SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Village Education Project
Kilimanjaro(VEPK) limeiomba serikali na wadau mbalimbali kushirikiana ili
kuhakikisha wanafunzi wa shule ya msingi wanajifunza na kuielewa lugha ya
Kiingereza ili waweze kufanya vizuri wanapojiunga na elimu ya Sekondari.
Aidha shirika hilo limeomba waalimu wanaofundisha katika
shule za msingi wasaidiwe kwa kuwezeshwa vifaa na kuendelezwa kielimu kwa kuwa
wao ndo kitovu cha maendeleo ya elimu nchini.
Mkurugenzi wa VEPK, Katy Allen aliyasema hayo jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuhusu tatizo
linalochangia wanafunzi kutofanya vyema katika masomo yao hasa katika mitihani
ya Taifa.
Alisema kuwa pamoja na kwamba wapo wanafunzi wengi ambao
wanamaliza elimu ya msingi hawakijui kiingereza lakini pia wapo waalimu wengi
ambao hawaijui lugha hiyo na wanahitaji
kusaidiwa.
Alisema kutokana na changamoto hiyo shirika hilo limeandaa
vitabu kwa ajili ya darasa la tatu hadi la saba vitakavyosaidia walimu na
wanafunzi kujifunza lugha hiyo lakini changamoto wanayokabiliana nayo ni jinsi
ya kuviingiza katika mtaala.
Alisema wameshazungumza na viongozi mbalimbali na tayari
vitabu hivyo vimeshafanyiwa majaribio na hivyo kuiomba serikali iviangalie upya
ili kuweza kusaidia wanafunzi kuielewa lugha ya kiingereza.
Kwa Upande wake mratibu wa shirika hilo, Dilly Mtui alisema
kuwa shirika hilo limelenga kukifanya kiingereza kuwa lugha rahisi ili kila mtu
akifahamu.
“Tatizo letu kubwa ni kwamba hatupendi mabadiliko, tunajenga
msingi wetu kwa kutumia matope mwishowe nyumba inaanguka, hivyo vitabu hivi ni
dawa ya kukifanya kiingereza kuwa lugha rahisi” alisema.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment