Diwani wa
Kata ya Kipawa Bonah Kaluwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na
matembezi ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya elimu katika
kata hiyo
Home Shopping Center kwa muda mrefu wamekuwa wakisaidia masuala ya maendeleo ya elimu nchini na masuala mengine muhimu katika jamii ya watanzania.
SHILINGI Bilioni moja inahitajika
kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya elimu katika kata ya Kipawa iliyopo
wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Diwani wa kata hiyo, Bonah Kalua
kwa kushirikiana na Manispaa ya Ilala, wameandaa matembezi ya hisani kwa ajili
ya kuchangia madawati kwa ajili ya shule zilizopo katika kata hiyo.
Alisema kuwa Kata hiyo inakabiliwa
na changamoto mbalimbali lakini kwa sasa wameamua kuanza na sekta ya elimu kwa
kuboresha madarasa, vyoo na upatikanaji wa madawati lengo likiwa ni kuhakikisha
kila mwanafunzi anapata elimu bora katika mazingira bora.
Kalua alisema kuwa katika matembezi
hayo wanatarajia kukusanya sh bilioni moja na kuwataka wahisani na wananchi
kujitokeza kwa wingi ili kuweza kuchangia upatikanaji wa madawati ambapo kwa
sasa Kata hiyo ina upungufu wa madawati zaidi ya 3,000 katika shule zote.
Aidha alipoulizwa kwamba ni kweli
anauchungu na maendeleo ya wananchi wake au lengo lake ni kuvizia Jimbo la
Segerea katika uchaguzi ujao, Kalua alisema anachokifanya ni uwajibikaji na
anatekeleza wajibu wake kama kiongozi.
Kalua alisema matembezi hayo
yaliyodhaminiwa na Home Shopping Center yanatarajiwa kufanyika Jumamosi(Machi
17) kuanzia saa 12 asubuhi katika shule ya msingi Minazi Mirefu na Mgeni rasmi
anatarajiwa kuwa Mama Salma Kikwete.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la
Segerea, Dk. Makongoro Mahanga alimpongeza diwani huyo kwa kubuni mikakati ya
kuboresha elimu hasa kwa kuchangia madawati ambayo yamekuwa ni kero kubwa.
Pia aliitaka jamii kushirikia
kikamilifu katika kuchangia maendeleo yao kwa kuwa serikali pekee haiwezi
ambapo pia aliwasihi wananchi wenye uchungu na maendeleo ya elimu kujitokeza
katika matembezi hayo na kuchangia chochote
“Kumekuwepo na juhudi za kuongeza
madawati na mimi kupitia mfuko wa jimbo nimekuwa nikitenga fedha kwa ajili
hiyo... kwa sasa tuna upungufu wa madawati kwa asilimia 40 na kila kata imekuwa
ikibuni mbinu na taratibu zake ili kuhakikisha tatizo hili linakwisha” alisema.
Note: Mtandao huu unatoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kuungana na HOME SHOPPING CENTER katika kuisaidia kata ya Kipawa
0 comments:
Post a Comment