Mkurugenzi wa Bendi ya African Stars Twanga Pepeta, Asha Baraka akichangia jambo wakati wa semina fupi ya viongozi na wamiliki wa Bendi za jijini Dar es Salaam.
Meneja wa Bendi ya Mapacha Watatu, Khamis Dakota akizungumzia tatizo la wanenguaji kushusha nguo zao mara wanapopandwa na mizuka jukwaani. Alishauri vikundi visivyosajiliwa vifuatiliwe.
Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego (kulia) akionesha kitabu cha Sera ya Taifa ya Utamaduni kwa viongozi na wamiliki wa Bendi za jijini Dar es Salaam kwenye semina iliyofanyika mwishoni mwa wiki hii. Kulia ni Mkurugenzi wa Ukuzaji Sanaa, BASATA Bi. Vivian Shalua.( Picha na Aristieds Kwizela)
Na Aristides Kwizela, (ofisa habari Basata)
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
mapema wiki hii limeendesha semina kwa viongozi na wamiliki wa bendi nchini ili
kusisitiza maadili na utambulisho wa Taifa miongoni mwa bendi hizo.
Akizungumza kwenye semina hiyo
iliyofanyika kwenye Ukumbi wa BASATA ulioko Ilala Sharif Shamba, Katibu
Mtendaji wa baraza hilo Ghonche Materego alisema kuwa, ni lazima sasa wasanii
wawe kweli kioo cha jamii, wawe vielelezo na wabebe utambulisho wa mtanzania.
“Ni lazima bendi na wasanii wetu kwa
ujumla wajiulize hivi kweli wao ni kioo cha jamii? Wanatoa kweli utambulisho wa
mtanzania? Ni vielelezo vya mtanzania? Tukijiuliza maswali haya tutaweza kujua
nini tunafanya katika kulinda utamaduni wetu” alisema Materego.
Aliongeza kuwa, wasanii hawana budi
kujua jinsi ya kuitumia Sanaa kulingana na hadhira pia wakati lakini zaidi
waweze kuhakiki kazi zao za Sanaa kabla ya kuzipeleka kwa walaji.
Akinukuu baadhi ya vipengele kutoka
kwenye sera ya Taifa ya Utamaduni, Bw. Materego alisema kuwa, BASATA kama moja
ya mtekelezaji wa sera hiyo ya utamaduni litahakikisha shughuli zote za
burudani nchini hazipotoshi maadili ya taifa.
“Sera ya Utamaduni katika sura ya 9
inaeleza haja ya kuchukua hatua kali dhidi ya wasanii na vikundi vya sanaa vinavyokiuka
maadili ya taifa. Tumeona tuwaite tukumbushane haya kabla hatujafikia hatua
hii” alisisitiza Materego.
Aliongeza kuwa, Sanaa ni kazi na
Baraza lisingependa kukatisha ajira za Wasanii lakini akasisitiza kuwa, hatua
iliyofikia sasa kunahitaji mabadiliko vinginevyo hatua zitachukuliwa ili
kudhibiti udhalili kwenye sekta ya Sanaa.
Kwa upande wake wamiliki na viongozi
wa Bendi walisema kuwa, kumekuwa na tatizo la wanenguaji wenyewe kushusha nguo
zao wanapokuwa kwenye maonyesho lakini wakaahidi kudhibiti hali hiyo.
“Ni kweli kuna tatizo hilo la uvaaji
hovyo kwenye maonyesho lakini nashauri Baraza liwe na mfano wa mavazi
yatakayotumiwa na wanenguaji lakini pia lifuatilie vikundi ambavyo
havijasailiwa na vinafanya maonyesho yanayovuruga maadili ya taifa” alishauri
Asha Baraka ambaye ni Mkurugenzi wa Bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’
0 comments:
Post a Comment