WAKATI taifa linatafuta ‘dawa’ kukomesha udanganyifu katika mitihani na kughushi vyeti, kashfa imeibuka ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzannia (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani huku baadhi ya wachungaji wakituhumiwa kujipatia nafasi za utumishi pasipo kuwa na sifa za kitaaluma.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kwamba zaidi ya wachungaji 20 ambao hivi sasa wanatumikia sharika mbali mbali nchini walidanganya juu ya ufaulu wao katika kidato cha Nne na cha Sita.
Kati ya watumishi hao ambao wamehitimu katika vyuo mbali mbali hapa nchini, inadaiwa kuwa watano wanahudumu katika sharika za hapa jijini Dar es Salaam.
Vyanzo vya habari vimebainisha kuwa wachungaji hao ambao walijiunga na vyuo vya Theolojia vya Mwika (Kilimanjaro), Kidugala (Iringa) vyote vikiwa chini ya Chuo Kikuu cha Tumaini baadhi yao wamepewa likizo ya lazima ya miezi miwili kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu.
Sakata hilo la kusaka uhalali wa vyeti vya wachungaji hao lilianza miezi sita iliyopita na kusababisha wawili kati ya watumishi hao kuondolewa kwenye utumishi.
Pia imebainika kuwa hivi karibuni msako uliendelea na kubaini kuwa wapo wachungaji wengine ambao ni watuhumiwa lakini bado wanaendelea na kazi ikidaiwa kuwa wanakingiwa kifua na baadhi ya viongozi wa juu wa kanisa hilo kwa misingi ya ukabila.
Imeelezwa kuwa baadhi ya watuhumiwa hao walitengeneza vyeti kuonyesha matokeo bandia tofauti na matokeo yao halisi wakati ambapo wengine hawakufika kidato cha Nne au cha Sita kabisa.
“Unakuta mtu anataka kwenda kusoma diploma ya Theolojia awe mchungaji wakati yeye amemaliza darasa la saba, anatengeneza cheti cha kidato cha nne ili apate sifa ya kwenda chuoni. Wengine wanatengeneza vyeti na kujiwekea alama mfano ‘B’ kuonyesha ufaulu mzuri kumbe sivyo. Kamisheni ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na vyuo walivyosoma vinapaswa kufuatilia uhalali wa diploma zao na kuchukua hatua stahiki,” chanzo kimebainisha.
Kufuatana na Sheria ya Vyuo Vikuu ya mwaka 2005 nafasi ya masomo inapatikana kwa wanafunzi waliokidhi vigezo vyote vya kujiunga na chuo baada ya udahili.
Pia ni marufuku kwa mwombaji yeyote kudanganya katika ufaulu wake katika ngazi zote hususan shule za sekondari.
Chanzo kingine cha habari hizo kimebainisha kuwa umekuwepo mvutano wa ndani kuhusu namna ya kulitatua tatizo hilo ambapo vyeti vya watuhumiwa vilibainika kuwa na kasoro ila wawili tu ndio wameondolewa kwenye utumishi na wengine kuendelea kukingiwa kifua na baadhi ya wakubwa.
Imebainika kuwa walioathirika na sakata hilo wanalalamika kuwa haki haijatendeka maana wapo wachungaji waliodanganya katika vyeti vyao lakini bado wanaendelea na kazi.
Mwumini mmoja Rabison Hojo (56) mkazi wa Kipawa, jijini Dar es Salaam ameshauri umakini katika udahili wa wanafunzi katika vyuo vyote hapa nchini kwa sababu wale wanaoghushi vyeti wanaziba nafasi za wale wanaostahili.
“Inasikitisha zaidi suala la kughushi linapojitokeza katika madhehebu ya kidini. Wachungaji ambao wanawatangazia watu msamaha wanategemewa kuwa waaminifu na wakweli katika mwenendo wa maisha yao. Tuhuma hizi ni nzito tena ni lazima zifuatiliwe kikamilifu,” amesema Hojo.
Alipohojiwa juu ya sakata hilo Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Tumaini ambaye pia ni Mkuu wa KKKT nchini, Askofu Dk Alex Malasusa amesema yeye hana habari kabisa na uwepo wa wachungaji walioghushi vyeti na angependa kulijua zaidi jambo hilo.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya KKKT, Bw Ibrahim Kaduma amesema kamati yake ambayo imeundwa hivi karibuni na yeye kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wake ingependa kushughulikia kikamilifu malalamiko yoyote ya waumini ili kuepuka kulipaka matope kanisa hilo.
“Ningependa kujua zaidi undani wa jambo hili na kamati yangu itafuatilia kwa karibu sana kubaini ukweli wa tuhuma hizo,” amesema Kaduma.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment